Zifahamu kanuni 7 za matumizi sahihi ya microwave

Na Fatuma Hussein
6 Dec 2024
Hakikisha unaitumia katika mazingira ya usafi huku ukifuata maelekezo ya matumizi yake.
article
  • Hakikisha unaitumia katika mazingira ya usafi huku ukifuata maelekezo ya matumizi yake.
  • Tumia vyombo sahihi vya kipashia chakula.

Chakula kikipoa wakati mwingine hukosa mvuto mlaji. Njia rahisi ya kukipa radha ni kukipasha. 

‘Microwave’ ni moja ya kifaa kinachotumika kupashia chakula na watumiaji wake hupenda kukuita kipashia chakula.

Licha ya kuwa microwave kuwa sehemu ya vifaa muhimu vya kielekroniki jikoni, bado baadhi ya watu hawatumia kwa usahihi. 

Uelewa mdogo wa matumizi wa kifaa hiki unaweza kusababisha kufa mapema na hasara kwa mmiliki.

Leo tunaangazia mambo/kanuni za kufuata wakati unatumia kifaa hicho ili kifanikishe shughuli zako kwa usahihi.

Aina za microwave 

Kwa mujibu wa mfanyabiashara wa vifaa vya nyumbani Kariakoo jijini Dar es Salaam, Yasin Mushi amebainisha kuwa kuna aina kuu mbili za mashine za kupashia chakula ambazo ni za kidijitali na ‘manual’ (mwongozo).

‘’Kuna ‘digital’ kuna ‘manual’, hiyo hiyo ‘manual’ kuna ya kupasha na kuchoma nyingine kuna ya kupasha peke yake ila nyingi za digital ni za kupasha na kuchoma,’’ amesema Mushi.

Kwa kutumia aina hii ya microwave unaweza kudhibiti kwa usahihi jinsi chakula chako kinavyopikwa. Picha / B&Q.

Mushi pia amesema kuwa mara nyingi kwa wafanyabiashara wengi ni vigumu kutoa elimu ya matumizi sahihi ya kifaa hiki muhimu jikoni kwa sababu ya mazingira ya kugombania wateja ingawa ni wateja wachache tu wanaopata elimu.

Microwave hii inafaa hata kwa matumizi ya kibiashara. Picha / Gammo.

Zingatia kanuni hizi wakati ukitumia microwave nyumbani:

Soma maelekezo ya mtengenezaji kabla ya kutumia

Kabla ya kutumia microwave yako, hakikisha unasoma maelekezo yaliyoandikwa na mtengenezaji. Hii inakupa uelewa wa vipengele muhimu vya kifaa, matumizi yake na tahadhari zinazotakiwa kuchukuliwa.

Muongozo huu humsaidia mtumiaji kuelewa hatua kwa hatua ya matumizi ya kifaa hiki. Picha / whirlpool.

Hakikisha mashine ni safi kabla na baada ya matumizi

Safisha microwave yako mara kwa mara ili kuzuia uchafu au mabaki ya chakula. Futa sehemu ya ndani na nje kwa kitambaa safi na usitumie maji. Hii itahakikisha microwave inabaki katika hali bora na pia hupunguza hatari ya bakteria.

Futa sehemu za ndani za microwave kwa spongi yenye unyevu iliyolowekwa kwenye maji ya moto kiasi. Picha / Amazon.

Tumia vyombo vinavyofaa kwa microwave

Wakati wa kupasha chakula, usitumie vyombo vya chuma, kwani vinaweza kusababisha cheche za moto. 

Badala yake, tumia vyombo vilivyoandikwa “salama kwa microwave” (microwave-safe). Ikiwa huna uhakika kuhusu chombo, ni bora kutokikitumia.

Unaweza kutumia sahani au bakuli la kioo wakati wa kupasha chakula, husaidia kuzuia kisikauke, na pia kioo hakitoi kemikali hatari kwenye chakula.

Kifuniko hiki cha microwave huzuia kwa ufanisi madoa na matone ya chakula, huku kikihifadhi microwave yako ikiwa safi na isiyo na harufu. Picha / Amazon.

Funika chakula kwa kifuniko
Kufunika chakula kwa kifuniko kunasaidia kuzuia chakula kisimwagike na kuweka microwave safi. Hakikisha kifuniko unachotumia hakina kemikali hatari zinazoweza kuyeyuka kwenye joto la juu.

Kila kifuniko cha aina  hii kina shimo la mvuke lililojengewa ndani ili kuzuia matone huku likiruhusu mvuke kutoka, likihifadhi microwave yako ikiwa safi na chakula chako kupashika vizuri. Picha / Walmart.

Ongeza kioevu kabla ya kupasha chakula

Ili kuzuia chakula kukauka, ongeza kioevu kama maji au mchuzi kabla ya kupasha. Hii husaidia chakula kubaki na unyevu na ladha bora.

Kioevu kinaweza kuwa mchuzi au maji ambao utarahisha upashaji wa chakula kwa haraka. Picha / Ubuy.

Fuata muda wa kupasha chakula uliopendekezwa

Usipashe chakula kwa muda mrefu kuliko ulivyoshauriwa. Angalia maelekezo ya muda wa kupasha na tumia kengele ya muda ili kuhakikisha chakula chako hakiungui. 

Kagua maelekezo kabla ya kuanza kupasha na weka kengele ya muda ili usisahau.

Hii sio tu inaongeza urahisi kwenye jikoni mwako bali pia husaidia kukujulisha mapema munatumia muda kiasi kupika chakula. Picha / Samsung.

Microwave huokoa muda na kurahisisha upashaji wa chakula. Ni muhimu kufahamu kuwa kifaa hiki pia kinaweza kupika chakula na hii ni mada ya siku nyingine.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa