Fahamu chanzo na jinsi ya kujikinga na bawasiri kwa kutumia matunda na chakula

Na Mwandishi Wetu
22 Aug 2023
Vyakula vya ngano hukwangua utelezi uliopo ndani ya utumbo hivo husababisha bawasiri
article
  • Lishe isiyofaa ndio sababu
  • Wataalamu wa afya wanasema lishe bora inaweza kukukinga na bawasiri

Bawasiri ni miongoni mwa magonjwa ambayo baadhi ya watu huona aibu kusema kwa wataalamu wa afya ili wapate tiba, hivyo baadhi yao huugulia maumivu kimya kimya na kusababisha madhara kuwa makubwa zaidi.

Ugonjwa huo huambatana na maumivu wakati wa kujisaidia haja kubwa, kutembea au kukaa na kuwafanya wagonjwa kukosa furaha huku wengine wakihangaika kutafuta suluhu bila mafanikio.

Kwa mujibu wa tovuti ya mayo clinic bawasiri isipotibiwa kwa wakati huweza kusababisha mgonjwa kupoteza damu nyingi na kuganda kwa damu.

Lishe isiyofaa ndio sababu

Daktari Joshua Robert kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, anasema lishe isiyofaa ikiwemo matumizi ya vyakula vya wanga kama ngano kwa kipindi kirefu ndiyo chanzo kikubwa cha bawasiri ambayo huwatokea watu wazima zaidi.

“Vyakula vya ngano hukwangua utelezi uliopo ndani ya utumbo hivo husababisha bawasiri” ameongeza daktari huyo.

Vyakula vingine vinavyochangia kutokea kwa bawasili ni pamoja na wali mweupe, vyakula vya haraka (fast food) na vyakula vingine visivyo na nyuzi nyuzi ambavyo husababisha mgandamizo katika utumbo unaopasua mishipa midogo midogo iliyopo sehemu ya haja kubwa.

Ujauzito

Ujauzito ni miongoni mwa sababu zinazopelekea bawasiri, hii ni kutokana na mabadiliko ya homoni na maumbile ya mwili wa mjamzito yanayopelekea ongezeko la mzunguko wa damu kwenye nyonga. 

Bawasili hutokea miezi mitatu ya mwisho wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua,”inasema tovuti ya afya ya Healthline.

Hata hivyo, tovuti hiyo inasema ugonjwa huo huisha bila matibabu mara baada ya kujifungua kutokana na homoni na kiwango cha damu kukaa sawa.

Matumizi ya vyakula nyuzi nyuzi kama mboga mboga na matunda ni vema kwa ajili ya mmengenyo mwepesi wa chakula. Picha|Unsplash  

Jinsi ya kujitibu na kuepukana na bawasiri 

Matibabu ya bawasiri hutegemea na aina na kiwango cha athari cha ugonjwa huo, kuna inayoweza kujitibika nyumbani kwa kutumia chakula na matunda pamoja na ile inayohitaji tiba ya wataalamu wa afya.

Dkt Joshua anasema ili kujikinga na bawasili ni vyema  kubadilisha mtindo wa maisha kwa kula mlo kamili pamoja na mazoezi.

Kuongeza vyakula vya nyuzi nyuzi kama mboga mboga, matunda, mbegu jamii ya karanga/korosho na maji katika mlo wako wa kila siku kunaweza kufanya kinyesi kuwa laini hivyo kukupunguzia hatari ya  bawasiri.

“Tumia mboga mboga na matunda yasiyosagwa kwa kuwa vinachelewa kuchakatwa, hivi vinasaidia kulainisha choo kwa kukusanya chakula chote kilichotangulia tumboni”

 Hivyo basi husaidia kurejesha utelezi ndani ya utumbo ili usichubuke na kusababisha kuvimba kwa bawasiri. 

Sambamba na hayo daktari huyo ameshauri ufanyaji wa mazoezi kila siku, unywaji wa maji mengi,kuepuka kukaa chini na kusimama muda mrefu ili kuepuka ugonjwa wa bawasiri.

“Shughuli hizi huchochea mgandamzo kwenye eneo la tumbo ilikusupport mwili hatimaye kuvimba kwa bawasiri.” anasema Dkt.Robert 

Ikiwa unahisi dalili za ugonjwa huu ni vyema kutembelea kituo cha afya kwa vipimo zaidi ili ufahamu aina ya bawasiri uliyonayo kabla ya kutumia tiba ya matunda na lishe.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa