Mapishi ya mboga ya bilinganya na nyama ya kusaga

Na Fatuma Hussein
18 Jan 2024
Jikoni kwetu leo tunaandaa mboga ya bilinganya iliyochanganywa na nyama ya kusaga ili kuongeza ladha na mvuto zaidi kwa walaji.
article
  • Pishi hili linatumia dakika 45 tu hivyo kukupa nafasi ya kupika chakula kingine.
  • Mbogahii inaweza kuliwa na aina yoyote ya chakula.

Ukiwa jikoni hutakiwi kuishiwa mapishi mapya yatakayowafanya walaji wako kuvutiwa zaidi na chakula unachokiandaa kila siku.

Jikoni kwetu leo tunaandaa mboga ya bilinganya iliyochanganywa na nyama ya kusaga ili kuongeza ladha na mvuto zaidi kwa walaji.

Kwa wasiofahamu, bilinganya ni miongoni mwa viungo ambavyo hutumika kwenye mboga na mapishi mengine mengi kama ilivyo kwa nyanya chungu, pilipili hoho na bamia.

Kuhusu muda wala usijai, pishi hili linatumia dakika 45 tu hivyo kukupa nafasi ya kupika chakula kingine au kufanya shughuli za nyumbani.

Namna ya kuandaa

Anza kwa kuandaa bilinganya, zioshe vizuri na ukipenda unaweza kumenya maganda ya juu, ukimaliza katakata vipande vidogo weka kwenye bakuli na uweke chumvi kidogo.

Baada hapo mimina maji ya baridi kwenye bilinganya zako ili kuzifanya ladha yake isiwe na chumvi kupitiliza kisha chuja maji yake na uziweke pembeni.

Osha nyama ya kusaga na uweke viungo (marinate) kama unapendelea au unaweza kuweka viungo wakati wa kukaanga.

Endelea na mapishi kwa kubandika sufuria jikoni, weka mafuta ya kupikia kiasi kisha mimina nyama ya kusaga na uipike kwa dakika tano mpaka saba.

Bilinganya pia hutumika kuongeza uzito wa mchuzi katika mboga mbalimbali.Picha|Pngtree.

Baada ya hapo weka kitunguu swaumu, tangawizi na  kitunguu maji kisha uchanganye kwa dakika mbili na  umalizie kwa kuweka nyanya ya kopo au nyanya za kawaida zilizosagwa na ufunike ziive.

Zikiiva ongeza bilinganya,hoho, karoti, chumvi kiasi,na uchanganye ichanganyike vizuri na mboga, ongeza maji kiasi na  ufunike kwa dakika 10 au mpaka pale yatakapopungua.

Ukiridhishwa na kiwango cha rojo iliyojitengeneza kwenye mboga yako, unaweza kuepua na itakuwa tayari kwa kuliwa na aina yoyote ya chakula.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa