Chai ya limao: Kinywaji cha kukata kitambi kwa haraka

Na Lucy Samson
31 May 2022
Inasaidia kuongeza kasi ya kuyeyusha mafuta mwilini. Unaweza kuitengeneza mwenyewe nyumbani. Licha ya kitambi kuwa na madhara ya kiafya kwa binadamu, bado kuna maoni tofauti kuhusu hali hiyo ya kuwa na tumbo kubwa miongoni mwa watu. Wapo ambao wanafikiri kitambi ni fahari au alama ya mtu mwenye pesa na wengine humuona mtu mwenye kitambi kuwa […]
article
  • Inasaidia kuongeza kasi ya kuyeyusha mafuta mwilini.
  • Unaweza kuitengeneza mwenyewe nyumbani.

Licha ya kitambi kuwa na madhara ya kiafya kwa binadamu, bado kuna maoni tofauti kuhusu hali hiyo ya kuwa na tumbo kubwa miongoni mwa watu.

Wapo ambao wanafikiri kitambi ni fahari au alama ya mtu mwenye pesa na wengine humuona mtu mwenye kitambi kuwa ana muonekano usiovutia.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa kitambi kina madhara mbalimbali ikiwemo kansa ya via ya uzazi kwa wanawake na kwa wanaume kushindwa kuzalisha, kisukari na shinikizo la damu.

Kwa mujibu wa wataalam wa afya, kitambi  ni hali ya mwili kuwa na mkusanyiko mwingi wa mafuta usio wa kawaida. Hali hiyo husababishwa maumbile ya asili, jinsi, vichocheo vya homoni na ulaji wa vyakula usiofaa.

Kama haupendelei kitambi kwa sababu kinakukera, zipo njia mbalimbali za kukiondoa ikiwemo kufanya mazoezi na kutumia baadhi ya vinywaji ambavyo unaweza kutengeneza nyumbani. 

Chai ya limao

 Chai ya limao imethibitishwa na wataalam wa afya kuwa ina mchango mkubwa katika kupunguza kitambi.

Dk George Munisi, mtaalamu wa masuala ya lishe, anasema chai ya  limao au ndimu ina umuhimu mkubwa kwenye  kwenye kupunguza kitambi. 

“Chai ya Limao ina  viungo ambavyo vinaenda kuyeyusha mafuta mwilini,sambamba na limao kuna tangawizi, mchaichai na mdalasini,” anasema Dk Munisi.

Utaitengenezaje? Tiririka nasi uweze kutengeneza kinywaji hiki chenye mahitaji machache kinachoweza kubadili muonekano wako.

Maandalizi ya chai ya limao

Mshauri wa tiba asilia kutoka kampuni ya Healing at Home Consultancy (MSI),  Matilda Kambangwa, anaeleza hatua kwa hatua jinsi ya kuandaa kinywaji hiki.

Hatua ya kwanza ni kuweka tayari jiko kwa ajili ya kuchemshia maji, au kama unatumia jagi la kuchemshia (heater) liandae.

Ukimaliza andaa ndimu/limao kwa kuiosha  kisha ukate katikati na ukamue kutengeneza maji ya ndimu yasiyokuwa na mbegu.

Saga mdalasini kwa blenda ndogo ya vitu vikavu  au utwange kwenye kinu ili kupata mdalasini wa unga, au kama unaweza kupata mdalasini wa unga itakuwa vizuri.

Maandalizi ya vitu hivyo yakikamilika, washa jiko na injika maji au uchemshe kwenye jagi kisha ongeza mdalasini, na tangawizi yakichemka yaepue na uweke kwenye  kikombe.

ukisha chuja vizuri unaweza ongeza ndimu au limao uliyokwisha kuichuja, ongeza na asali vijiko viwili au sukari kiasi, wengine hunywa hivyo hivyo.

Mpaka kufikia hapo chai ipo tayari kwa kunywa, hakikisha unakunywa mchanganyiko huu dakika arobaini au zaidi kabla ya kupata kifungua kinywa cha asubuhi.

Kuondoa kitambi ni zaidi ya chai ya limao

Mtaalam huyo wa afya anasema sio chai ya limao pekee itakayokuondolea kitambi lakini kuna mambo ya ziada ya kufanya.

“Jizoeshe kupunguza kula vyakula vya mafuta na kutumia chakula cha wanga kwa kiasi kidogo, ongeza matunda na mboga mboga zaidi kwenye mlo wako,” anasema Kambangwa.

Sasa unaweza kufurahia maisha bila kitambi wala kujibana bana na mikanda.

Je, kuna kitu kingine unatamani kujifunza kupika kwa mbinu nyingine mpya? Tufahamishe tukuhudumie na tujifunze kwa pamoja. Namba ni moja tu! +255 677 088 088.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa