Juisi (sharubati) ya Lozera ni moja kati ya vinywaji maarufu katika maeneo mengi nchini Tanzania.
Kwa miaka mingi kinywaji hicho kimetumika zaidi majumbani, lakini kwa sasa unaweza kununua hotelini, migawahani au sehemu mbalimbali mahususi kwa ajili ya kuuza sharubati.
Ubunifu zaidi umeongezwa katika kinywaji hicho ambapo kwa sasa juisi ya rozela huchanganywa na matunda mengine kama nanasi, chungwa, limao, ubuyu pamoja na viungo mbalimbali.
Wataalamu wa afya wanasema utumiaji wa juisi hii unaweza kuongeza damu ikiwa utatumiwa mfululizo kwa angalau wiki mbili.
Emmanuel Shayo ambaye ni tabibu katika zahanati ya Taifo iliyopo jijini Dar es Salaam amesema kuwa sharubati ya lozera ina uwezo wa kuongeza damu mwilini kutokana na kusheheni kiwango kikubwa cha madini chuma.
“Ni kweli juisi ya rozella inaongeza damu ila inatakiwa unywe angalau kwa siku 14…hii inatokana na uwepo wa kiasi kikubwa cha madini ya chuma katika kinywaji hicho,” amesema Dk.Shayo
Tovuti ya masuala ya afya ya afyayako.com inabainisha kuwa madini ya chuma (iron) ni ya lazima katika utendaji kazi wa hemoglobin, ni aina ya protini inayohitajika katika kusafirisha oksijeni katika damu na ni muhimu katika shughuli muhimu za mwili.
“Upungufu wa madini ya chuma katika damu unaweza kuleta matatizo kadhaa ya kiafya, ikiwa ni pamoja na upungufu wa damu (iron deficiency anemia),” inaeleza tovuti hiyo.
Baada ya kufahamu faiza za kiafya sasa tuangalie namna ya kuandaa juisi ya rozela iliyochanganywa na nanasi, maganda ya nanasi, tangawizi pamoja na mdalasini.
Maandalizi
Baadhi ya watu huyaloweka majani ya rozela kwa muda mfupi kisha huchuja na hapo inakuwa tayari kwa kunywa lakini leo tuangazia njia nyingine ya kuchemsha.
Hatua ya kwanza ya uandaaji wa juisi ya lozera ni kuandaa jiko utakalotumia kuchemshia kinywaji hicho kisha bandika maji kiasi kutokana na wingi wa majaini ya lozera uliyonayo kisha yaache yapate moto kidogo.
Maji yakishapata moto, weka majani ya lozera kiasi upendacho, ongeza maganda ya nanasi, tangawizi, mdalasini na iriki kama unapendelea, kisha acha yachemke.
Ili kufurahia utamu wa juisi ya rozela baadhi ya wapishi na wauzaji wa kinywaji hicho wanashauri kuchemsha kwa muda mfupi ili kuepuka juisi hiyo kukosa ladha.
Huwa nawafundisha wanafunzi wangu wa mapishi wakiona majani ya rozella yamebadilika rangi na kuwa ya pinki hivi au ile rangi yake ya kukolea imepungua basi wajue hapo ipo tayari,” anasema Eva Jacob mkufunzi binafsi wa mapishi Dar es Salaam.
Hatua inayofuata baada ya kuchemka ni kuchuja na kuongeza sukari au asali kama unapendelea na juisi yako itakuwa tayari kwa kunywa.