Miongoni mwa vyakula vyinavyopendwa zaidi wakati huu wa Mwezi mtukufu wa Ramadhani uji wa muhogo. Kinywaji hiki kinatoa virutubisho vingi muhimu mwilini ikiwemo vitamini na wanga ambavyo vinaweza kuimarisha kinga ya mwili.
Lakini kwa nini hupendwa zaidi? Moja kati ya sababu ya kinywaji hiki kutumiwa sana kipindi cha Mwezi mtukufu wa Ramadhani ni uwezo wake wa kuupa mwili nguvu hususani kwa wanaoswali sala ndefu (taraweh).
Katika kipindi hiki uji huu huwekwa manjonjo zaidi ikiwemo pilipili manga na ukwaju ambao huchangamsha mwili dakika chache tu baada ya kuutumia.
“Asikudanganye mtu, wewe kunywa Uji wa Pilipili Manga uone ndani ya dakika 10 kama utakuwa haujachangamka,” anasema Mwanahamisi Gumbo, Mama Lishe mzoefu Jijini Dar es Salaam.
Mama lishe huyo anasema wateja wake hupendelea uji wa moto hasa ukiwa umekolea ndimu, ukwaju na sukari inayoongeza ladha.
Sasa tuachane na simulizi za mama lishe huyo tuingie jikoni kuandaa uji wa muhogo wenye ladha adimu.
Namna ya kutayarisha
Hatua ya kwanza ya kuandaa uji wa muhogo ni kuhakikisha unauchekechakwa chekeche ya matundu madogo ili kuondoa uchafu wowote uliopo.
Andaa maji ya uji
Baada ya hapo sasa weka maji kwenye sufuria na ubandike jikoni rasmi kwa ajili ya kuanza mapishi ya uji huu ambao utachukua dakika mpaka 20 hivi kuiva.
Weka unga kiasi
Kabla maji hayajachemka, koroga unga kiasi kwenye bakuli au kikombe kwa ajili ya kukorogea kwenye maji yako uliyobandika jikoni.Ukishamimina koroga bila kuachia kwa dakika mbili ili unga uchanganyike na maji vizuri.
Koroga mpaka uji uvutike
Uji wa muhogo huwa na kawaida ya kuvutika hivyo koroga bila kuachia mpaka uone uji wako umeshikana na unavutika.
Baada ya hapo loweka ukwaju kwenye maji na utengeneze juisi yake nusu kikombe. Changanya vijiko viwili vya maji ya ndimu na pilipili manga kiasi kisha uweke kwenye uji wako.
Baada ya hapo koroga na uache uji wako uive kwa dakika tano.Katika hatua hii unaweza kuongeza sukari kiasi unachopendelea..
Mpaka hapo uji wako utakuwa tayari kwa ajili ya kutumiwa kwa ftari au kwa kifungua kinywa wakati wa asubuhi.