Je unajua utamu wa juisi ya parachichi na nazi?
Kama bado ni muhimu kuelewa kuwa juisi ya parachichi na nazi ni kinywaji cha asili chenye ladha tamu na manufaa kwa afya yako.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) juisi ya matunda halisi huupatia mwili vitamini na makapimlo yaliyo kwenye matunda halisi husaidia kupunguza uwezekano wa kuugua saratani ya utumbo.
Matunda haya licha ya kutumika katika mazingira ya kila siku yana wingi wa vitamini E, K, B na C, na madini ya potasiamu. Husaidia kudumisha afya na kudhibiti shinikizo la damu na kufanya mapigo ya moyo kuwa ya kawaida.
Na leo ndani ya jikopoint.co.tz tunaenda kujifunza namna ya kuandaa juisi hii ambayo ni fursa kwa wafanyabiashara na matumizi ya nyumbani.
Hatua kwa hatua
Hatua ya kwanza katika utengenezaji wa juisi hii ni kuosha matunda kwa kutumia maji safi na salama ili kuondoa uchafu. Menya parachichi na uondoe mbegu kisha kata vipande vidogo ili iwe rahisi kusaga.
Hatua inayofuata tengeneza tui la nazi kulingana na kiasi cha juisi. Hakikisha unapata tui zito.
Andaa blenda ya kusaga kisha weka vipande vya parachichi na ongeza tui la nazi, asali na maji ya ndimu au limao. Ukipenda unaweza kuongeza unga wa mdalasini.
Ukimaliza hatua hiyo saga mchanganyiko wote kwa sekunde 30 hadi 60 mpaka uwe laini na ikiwa unataka juisi iwe nyepesi ongeza maji kiasi kisha saga kwa dakika 3 hadi 5.
Mpaka hapo juisi ya parachichi na nazi inakuwa tayari kwa kunywa. Unaweza kuongeza vipande vya barafu au kuweka kwenye jokofu kwa ajili ya matumizi ya baadaye.
Usisubiri kusimuliwa tengeneza leo ufurahie ladha tamu!