Jinsi ya kuandaa juisi ya ‘Strawberry’, embe na nanasi

Na Fatuma Hussein
25 Nov 2024
Juisi hii ni chanzo cha vitamini na madini katika mwili.
article
  • Juisi hii ni chanzo cha vitamini na madini katika mwili.

Wakati wa msimu wa sikukuu watu wengi hupendelea kuandaa juisi za matunda zinazowawezesha kuburudisha watu wengi kwa wakati mmoja huku zikiwapatia virutubisho muhimu kwa ajili ya miili yao.

Wengine huzitumia juisi hizo kama mbadala wa vinywaji vyenye sukari nyingi ikiwemo soda ambazo hutumika sana katika sikukuu au sherehe.

Leo  jiko point tumekusogezea maandalizi ya juisi yenye mchanganyiko wa matunda ambayo ni embe, ’strawberry’ na nanasi unayoweza kuandaa katika msimu huu wa sikukuu.

Utakachohitaji ni maembe makubwa mawili ikiwa unatengena juisi kwa ajili ya watu wachache, strawberries nne, nanasi moja dogo, tangawizi, na sukari au nanasi kama unapendelea.

Maandalizi

Osha Strawberry vizuri, kisha ondoa vikonyo na ukate vipande vidogo, baada ya hapo menya maembe, tangawizi na nanasi na uyakate vipande vidogo vidogo

Unaweza pia kutumia maganda ya nanasi kama utapendelea ambapo itakulazimu uyachemshe kwanza kisha uchuje maji yake na uyatumie kusagia juisi unayoiandaa.

Hatua inayofuata weka vipande vya embe, Strawberry, na nanasi kwenye blenda, ongeza glasi moja ya maji baridi au juisi ya maganda ya nanasi iliyochemshwa hapo awali na Tangawizi.

Saga mchanganyiko huo kwa dakika tano hadi 10 au mpaka utakapopata juisi itakapochanyika vizuri na matunda yote kusagika kama inavyotakiwa.

Kwa wale wasiopenda juisi yenye mabaki, tumia chujio kuchuja juisi ili kuondoa mabaki na kuifanya iwe laini na nzuri kwa matumizi.

Ukishamaliza hatua hizo ongeza asali au sukari kwa kiasi unachotaka kulingana na ladha yako, kisha koroga vizuri tia barufu kupata ubaridi kama hauna jokofu.

Mpaka hapo juisi yako itakuwa tayari kwa matumizi ila kumbuka wengine huona ni vyema zaidi sukari kuisaga moja kwa moja wakati wanasaga matunda.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa