Baada ya saa kadhaa za kufunga, si kila kinywaji kinaweza kukuburudisha na kupa mwili wako virutubisho vinavyouhitaji ili kujiandaa kwa ajili ya kufunga kwa siku nyingine.
Kubali au ukatae ila vinywaji ndiyo vinaweza kurudisha nguvu iliyopotea mwilini kwa haraka ikiliandaa tumbo kwa ajili ya kupokea chakula kizito hususani kikiwa cvha moto.
Miongoni mwa vinywaji hivyo ni uji wa ulezi wenye tende na maziwa uliosheheni virutubisho vingi ambavyo vitauimarisha mwili wako vikiliandaa tumbo kupokea futari nzito iliyoandaliwa.
Kwa mujibu wa tovuti ya masuala ya afya ya Healthline, ulezi husaidia kudhibiti kiwango cha sukari kweye damu, kupunguza lehemu (cholesterol) pamoja na shinikizo la damu.
Pia, kinywaji hicho kikichanganywa na maziwa kinaweza kuimarisha afya ya mama mjamzito pamoja na mtoto anayeanza kula kutokana na wingi wa madini chuma na kalsiamu.
Ili kupata faida hizo za kiafya, jikopoint imekuandalia hatua za maaandalizi ya uji huo unaoweza kuutumia wakati wa mfungo huu wa Ramadhani kwa waislamu na mfungo wa kwaresma kwa wakristo.
Hatua za kuandaa uji wa tende na maziwa
Anza kwa kuondoa mbegu katika tende kisha ziosha uloweke kwenye maji kwa dakika 30 ili zilainike. Baada ya hapo, saga hadi upate uji mzito wenye ladha tamu asilia.
Htua inayofuata ni kuandaa uji ambapo tutatumia maziwa badala ya maji, ambapo utabandika maziwa jikoni ikifuatiwa na uji wa tende na kabla hayajachemka changanya unga wa ulezi na maji katika kikombe au bakuli pembeni na kisha umimine jikoni.
Koroga bila kuachia kwa muda wa dakika 10 kwa moto mdogo mdogo hadi uji uoneshe dalili za kuanza kuchemka na uongeze robo kijiko cha hiriki kama unapendelea.
Kama hupendelei maziwa ya ng’ombe unaweza kuchemsha uji wako kwa kutumia maji ya kawaida au ukatumia aina nyingine ya maziwa ikiwemo ya almondi.