Jinsi ya kutengeneza ‘cappuccino’ nyumbani

Na Lucy Samson
7 Oct 2024
Ili kuandaa kinywaji hiki utahitaji kahawa iliyosagwa (instant coffee) maziwa, sukari pamoja na maji safi.
article
  • Ili kuandaa kinywaji hiki utahitaji kahawa iliyosagwa (instant coffee) maziwa, sukari pamoja na maji safi.

Kwa wapenzi wa kahawa bila shaka wanafahamu kinywaji maarufu aina ya ‘cappuccino’ ambacho hutengenzwa kwa kutumia kahawa na maziwa.

Kinywaji hicho kimejizolea umaarufu katika nchi nyingi ikiwemo Tanzania na kuwafanya baadhi ya watumiaji wake kutoboa mifuko yao zaidi ya wanywaji wa kahawa ya kawaida ili kukipata.

Jambo la kufurahisha ni kwamba unaweza kuandaa kinywaji hiki nyumbani hata kama hauna vifaa au mashine ambazo mara nyingi hutumika katika migahawa kuandaa kinywaji hicho.

Utakachohitaji ili kuandaa kinywaji hiki ni kahawa iliyosagwa (instant coffee) maziwa, sukari pamoja na maji safi.

Muonekano wa kahawa ya kusaga {instant cofee) ambayo pia huuzwa madukani kwa bei ya rejereja.Picha| Eater.

Maandalizi

Anza kwa kuandaa kahawa pamoja na sukari kiasi unachopendelea au kulingana na mahitaji yako ila kwa maandalizi ya kikombe kimoja utahitaji kijiko kimoja cha kahawa pamoja na kijiko kimoja cha sukari.

Weka kahawa na sukari katika kikombe kikubwa kisha uongeze maji robo kijiko na uanze kukoroga.

Koroga kama vile inavyofanyika wakati wa kuchanganya sukari na siagi katika maandalizi ya keki huku ukiongeza maji kidogo kidogo.

Wakati ukiendelea kuchanganya kahawa itaanza kubadilika rangi kutoka rangi ya kahawia iliyokolea hadi kahawia iliyopauka huku ikitengenza mchanganyiko mzito (creamy).

Hakikisha umechanganya hadi umepata mchanganyiko mzito (kama inayoonekana hapo chini) kisha ubandike maziwa jikoni na uache hadi yachemke.

Mchanganyiko wa kahawa maji kiasi pamoja na sukari ukiwa tayari kwa ajili ya kuandaa kinywaji aina ya ‘cappuccino. Picha|feel Good Foodie.

Yakichemka ongeza katika kikombe ulichokuwa unaandalia kahawa na taratibu utaanza kuona kahawa na maziwa inatengeneza mchanganyiko mzito wenye mapovu kwa juu.

Ukifika hatua hiyo koroga vizuri ili maziwa na kahawa ichanganyike vizuri na kinywaji chako kitakuwa tayari.

Ikiwa utependa cappuccino yako iwe na maua au michoro ya kupendeza kwa juu unaweza kutumia ‘chocolate syrup’ au aina yoyote ya ladha utakayopendelea.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa