Katika msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka watu wengi hujaribu kuandaa vyakula na vinywaji vya tofauti ili kuvutia wageni na wanafamilia ambao hujumuika pamoja kwa ajili ya kusherekea.
Kati ya vinywaji vingi vilivyopo duniani unavyoweza kuandaa katika msimu basi Mocktail ya Blue Ocean ndiyo yenyewe.
Kinywaji hiki ambacho hakitengenezwi na aina yoyote ya pombe huvutia wengi kutokana na rangi yake ya kuvutia inayotokana na shira ya Blue Curaçao yenye ladha ya machungwa pamoja na soda au juisi nyingine za machungwa.
Jiko Point leo imekusogezea njia rahisi ya kutengeneza mocktail ya Blue Ocean ukiwa nyumbani ambapo unaweza kuokoa Sh 12,000 mpaka 20,000 kwa kila glasi kama ungenunua kinywaji hicho katika maeneo ya starehe
Kama ulikuwa hujui Mocktail ni mchanganyiko wa vinywaji na viungo
Hatua ya kwanza ni kuandaa mahitaji ikiwemo glasi au chombo chochote kikubwa utakalolitumia kuwekea kinywaji chako mara baada ya kuiandaa, kisha andaa vipande vya barafu (kulingana na mahitaji), shira ya Blue Curaçao juisi ya machungwa na soda ya limao.
Shira ya Blue Curaçao inapatikana katika maduka yote yanaouza vinywaji na huuzwa kuanzia Sh18,000 mpaka Sh36,000 kulingana na ujazo.
Katika maandalizi anza kwa kuweka vipande vya barafu kiasi katika glasi au chombo kikubwa utakachokitumia ikifuatiwa na shira ya Blue Curaçao mililita 30 na juisi ya machungwa mililita 30 kisha malizia na soda ya limao au soda ya sprite mililita 90.
Baada ya hapo koroga taratibu mchangavyiko wako mpaka kinywaji chako kichanganyike vizuri na kupata rangi nzuri ya blue bahari kisha kitakuwa tayari kwa kunywa,
Pamba glasi yako kwa kipande cha chungwa kufanya kinywaji chako kuwa na muonekano wa kuvutia.