Kwanini glasi za mvinyo zinaumbo tofauti na glasi zingine?

Na Rodgers George
1 Feb 2022
utofauti wa glasi za mvinyo (wine) na glasi zingine una makusudi yake. kuanzia bakuli, shingo na ukingo wa glasi hizo, zote zina maana yake.
article
  • Tofauti na glasi zingine zenye sehemu tatu, glasi za mvinyo zina sehemu nne.
  • Ni Ukingo, bakuli, shingo na kitako.
  • Kila sehemu inakazi zake na endapo ukitumia mvinyo kwenye glasi isiyo yake, hautofurahia.

Kwa wapenzi wa mvinyo (wine), bila shaka unafahamu heshima yake ni kutengwa kwenye glasi ndefu yenye shingo ambayo ni tofauti na glasi zingine kama za maji, bia na hata juisi.

Umewahi kujiuliza kwanini glasi hiyo ni tofauti na glasi zingine? Upo mahala sahihi kujifunza kama ni jambo geni kwako.

Glasi za wine zimebuniwa kwa umaridadi huku kila sehemu yake yaani kitako, shingo, bakuli na ukingo vikiwa na kazi zake. Kazi hizo zinafanya glasi hizo kuwa na muonekano tofauti na zingine zilizopo sokoni.

Kitako cha glasi ni kwa ajili ya pozi

Mtaalamu wa mvinyo, Andi Healey katika andiko lake kwenye tovuti ya kampuni ya The Riedel Shop ya nchini Uingereza ameandika kuwa kazi ya kitako ni kusaidia glasi isianguke. 

Licha ya kuwa zipo baadhi ya glasi ambazo hazina kitako kabisa, lakini kwa mtumiaji wa mvinyo bila shaka unafahamu umuhimu wa kunywa mvinyo kidogo na kuweka glasi yako pembeni ukisikilizia mvinyo huo ushuke taratibu.

Huenda kitako ni sehemu ya kila glasi isipokuwa zile zilizobuniwa kushikiliwa mwanzo mwisho lakini kwa kinachofuata, huenda ukaanza kuelewa somo.

Fahamu kuwa, kuna aina tofauti tofauti za mvinyo na zote huwa na glasi zake. Picha| The Denver Post.

Shingo ya glasi na kuzuia joto

Shingo ya glasi za mvinyo ni sehemu nyembamba zaidi kwenye glasi hiyo. Eneo hilo ndilo humuwezesha mtumiaji ashikile glasi yake kwa vidole.

Katika kushika glasi ya mvinyo, shingo imewekwa ili kuzuia mnywaji wa wine kushika sehemu ya bakuli. 

Muonja mvinyo, Lauren Volper kupitia ukurasa wake wa medium ameandika, siri nyuma shingo hiyo ni kuwa, unaposhika sehemu ya bakuli na kunywa mvinyo, utanusa mikono yako, kitu ambacho mafuta, bakteria, manukato yaliyopo kwenye mikono yako yataingiliana na wewe kufurahia mvinyo huo.

Unaposhika glasi ya wine kwenye shingo, unaweka mkono wako mbali na mvinyo na hivyo unapokunywa wine hiyo utapata harufu ya wine na wine yenyewe.

Bakuli pana kuruhusu mzunguko

Bila shaka umewahi ona baadhi ya watu wakizungusha wine kwenye glasi kabla ya kunywa. Hiyo hupandisha harufu ya mvinyo juu na kumpa hamasa fulani mnywaji. Glasi ya mvinyo kuwa na muundo wa bakuli lenye ukingo (rim) mdogo lii kuruhusu mzunguko huo umalizike bila kumwaga mvinyo huo.

Healey amesema, umbo hilo pia limewekwa ili kuruhusu wine kuwa nyingi kwenye glasi kwani inashauriwa kujaza glasi ya wine kwa kiasi cha theluthi ili  nafasi inayobaki itumike na mnywaji kuzungusha wine yake wakati ukinywa.

Udogo wa kingo ya glasi husaidia mnywaji kupata harufu ya mvinyo. Picha| The New York Magazine.

Ukingo ni kwa ajili ya kunywea

Sehemu hii ndipo mvinyo hukutana na mdomo wa mnywaji. Kwenye glasi za wine, ukingo ni mdogo kuliko sehemu ya bakuli. 

Hii mtaalamu Jeff Flowers kwenye andiko lake na tovuti ya Wine Cooler Direct amesema udogo wa ukingo unasaidia kutunza harufu ya mvinyo na kumpatia mnywaji uwezo wa kunusa harufu hiyo wakati akinywa fundo la mvinyo wake.

Usipozingatia hii, ndio mwanzo wa kuona mvinyo wako hauko sawa kumbe tatizo ni kuwa unaweza kuwa umekunywa mvinyo kwenye glasi ya bei chee iliyokuharibia uzoefu wa kunywa mvinyo wako.

Katika andiko lijalo, tutaangalia tofauti ya mvinyo mwekundu na mweupe na faida zake. Endelea kubaki na Jiko Point.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa