Mbinu za kutengeneza juisi ya maganda ya nanasi

Na Lucy Samson
13 Sept 2022
Maganda ya nanasi yanaweza kutoa juisi ama sharubati tamu zaidi sawa kabisa na tunda lenyewe.
article

  • Maganda ya nanasi yanaweza kutoa juisi tamu kushinda tunda lenyewe.
  • Juisi hii inafaa sana kutengeneza hata kama hakuna umeme.

Juisi ya maganda ya nanasi ina wingi wa vitamin C,pia inasaidia kuongeza kinga ya mwili.Picha|Urlife Blog.

Hapana shaka  wengi wetu baada ya kumenya nanasi maganda yake kuwa tunayatupa tukifikiri ni uchafu na kazi yake imeisha. Hapana. 

Utamu wa tunda hilo tunaoufaidi kwenye juisi au kula lenyewe unafanya tusahau kuhusu maganda ya tunda hilo. Ila ambacho hatufahamu ni kuwa maganda nayo yana faida lukuki mwilini na yana ladha ya kipekee.

Hivyo kama ulikuwa hujui ngoja leo nikujuze.  Maganda ya nanasi yanaweza kutoa juisi tamu pengine hata kulizidi tunda la nanasi lenyewe.

Fuatana nami katika makala hii fupi mpaka mwisho ujifunze kisha hamishia ujuzi huu nyumbani kwako.

Mahitaji

  • Maganda ya nanasi kiasi cha juisi unayotaka
  • Sukari kutokana na kiwango cha juisi na unavyopendelea
  • Maji safi
  • Sufuria itakayoweza kuhifadhi kiwango cha juisi utakayotengeneza
  • Jiko, 
  • Chujio, 
  • Tangawizi moja na,
  • Ndimu au limao.

Maandalizi

Osha maganda ya nanasi na tangawizi kwa maji safi kisha katakata na uweke kwenye sufuria tayari kwa kuchemsha.

Washa jiko, bandika sufuria yenye maganda ya nanasi na tangawizi. Weka maji kiasi chako( kutokana na wingi wa maganda ya nanasi) kwenye sufuria yako kisha ufunike uache ichemke kwa dakika 30 hadi maji yatakapobadilika na kuwa na rangi ya njano.

Maandalizi ya juisi hii ni rahisi hayahitaji blenda inayotumika wakati wa kusaga aina nyingine za juisi, hivyo hata kama umeme umekatika bado unaweza kutengeneza juisi  hii na kufurahia pamoja na uwapendao. 

Ikichemka hadi kiwango unachohitaji ipua juisi yako na uache ipoe vema. Baada ya hapo ichuje na uweke kwenye jagi au glasi unayotaka kutumia kunywa juisi yako au chombo chochote ulichokiandaa. 

Ongeza maji ya limao au ndimu na vipande vya barafu, mpaka hapo juisi yako ipo tayari kwa kunywa. Iwapo hupendi barafu, endelea kufurahia ikiwa ya moto. 

Hapana shaka umeona namna unavyoweza kuongeza thamani maganda ya nanasi na kutengeneza juisi ama sharubati murua. 

Una maswali au una mrejesho baada ya kutengeneza juisi hiyo tucheki Whatsapp kupitia +255 677 088 088 au Twitter, Facebook na Instagram kupitia @JikoPoint au @officiallupah. 

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa