Namna ya kuandaa chai ya rozela (choya)

Na Fatuma Hussein
18 Sept 2024
Ikiwa wewe ni mpenzi wa chai najua utakuwa unaumiza kichwa ni ubunifu gani unaweza kuongeza katika kinywaji hicho ili kuongeza mvuto na ladha tamu zaidi. Mbali na chai ya viungo, chai ya maziwa, chai ya nazi, kuna aina mpya ya kuandaa chai kwa kutumia majani ya rozela au wengine huziita choya. Kwa muda mrefu, mmea […]
article
  • Unaweza kuchanganya chai hii na viungo vingine ili kupata ladha zaidi.
  • Unashauriwa kunywa  angalau vikombe vitatu vya chai ya rozela kila siku.

Ikiwa wewe ni mpenzi wa chai najua utakuwa unaumiza kichwa ni ubunifu gani unaweza kuongeza katika kinywaji hicho ili kuongeza mvuto na ladha tamu zaidi.

Mbali na chai ya viungo, chai ya maziwa, chai ya nazi, kuna aina mpya ya kuandaa chai kwa kutumia majani ya rozela au wengine huziita choya.

Kwa muda mrefu, mmea huo umekuwa ukitumika kutengeneza juisi au sharubati ambayo huchanganywa na matunda mengine ikiwemo nanasi, limao au machungwa jambo linaloongeza ladha kwa watumiaji wa kinywaji hicho.

Lakini unaweza pia kutumia mahitaji hayo hayo kuandaa chai ya rozela ambayo ina faida sawa na juisi yake ikiwemo kuongeza damu kama anavyoeleza daktari Emmanuel Shayo  kutoka zahanati ya Taifo iliyopo jijini Dar es Salaam.

“Ni kweli juisi ya rozela inaongeza damu ila inatakiwa unywe angalau kwa  siku 14…hii inatokana na uwepo wa kiasi kikubwa cha madini ya chuma katika kinywaji hicho,” amesema Dk.Shayo. 

Tovuti ya afya ya Uly clinic inafafanua kuwa kunywa vikombe vitatu vya chai ya rozela kila siku husaidia kudhibiti mapigo ya moyo, kupunguza lehemu (cholesterol) na mafuta kwenye damu, hivyo kulinda mishipa ya damu na kupunguza hatari ya shinikizo la juu la damu.

Baada ya kufahamu faida za kiafya za kutumia chai ya rozella, tuingie jikoni ambapo tutajifunza hatua kwa hatua jinsi kuandaa ya kinywaji hicho. 

Namna ya kuandaa

Hatua ya kwanza ni kuchukua sufuria safi au jagi la kuchemshia chai kisha chemsha nusu kikombe cha majani ya rozela haya yanaweza kuwa majani mabichi au yaliyokaushwa.

Unaweza kutumia lita mbili za maji kwa kila nusu kikombe cha chai cha majani ya rozela ili kupata ladha na virutubisho vinavyotakiwa.

Katika sufuria hiyo hiyo au jagi unalotumia kuchemshia unaweza kuongeza mdalasini, hiriki, karafuu, vipande vya chungwa lililomenywa, majani ya nana, maganda au vipande vya nanasi ili kuongeza ladha.

Baada ya chai kuchemka kwa dakika kwa muda wa dakika tano hadi 10 unaweza kuchuja ili kuondoa majani na mabaki ya matunda uliyoyatumia ambayo hayahitajiki tena katika hatua zinazofuata.

Unaweza ongeza utamu kwa kuweka asali kijiko kimoja cha chai kwenye kila kikombe cha chai au unaweza kutumia sukari na juisi ya limau ili kuongeza ladha na utamu.

Mpaka kufikia hatua hii chai itakuwa tayari kwa matumizi na familia yako au kuifanya kuwa fursa mpya ya biashara. 

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa