Namna ya kutengeneza juisi ya miwa nyumbani

Na Lucy Samson
21 Nov 2022
Utakachohitaji ni miwa, limao na kiasi kidogo cha maji.
article
  • Unahitaji blenda yenye uwezo wa kusaga vitu vigumu.
  • Utakachohitaji ni miwa, limao na kiasi kidogo cha maji.

Juisi ya miwa ni moja kati ya kinywaji pendwa kwenye mitaa mbalimbali jijini Dar es Salaam. Hii ni kutokana na urahisi wa upatikanaji wake na faida nyingi za kiafya zilizopo kwenye kinywaji hicho.

Kwa mujibu wa tovuti ya healthifyme, juisi ya miwa ina faida nyingi kwenye mwili wa binadamu ikiwemo kusaidia mfumo wa mmeng’enyo wa chakula, kusaidia mwili kupambana na ugonjwa wa kansa na magonjwa ya mfumo wa mkojo.

Mbali na hayo juisi hiyo pia inaupa mwili nguvu, inaboresha afya ya figo na kupunguza kasi ya maambukizi ya njia ya mkojo (UTI’s).

Licha ya faida nyingi zilizopo kwenye kinywaji hicho watu wengi hawawezi kutengeneza nyumbani kwa kisingizio cha kukosa mashine ambazo mara nyingi zinatumiwa na wafanyabiashara wa juisi hizo.

Juisi hiyo yenye sukari ya asili inaweza kutengenezwa nyumbani na kuipa familia  faida nyingi zilizopo kwenye kinywaji hicho.

Fuatana nami kwenye makala haya ujifunze namna ya kuandaa kinywaji hiki.

Mahitaji

  • Miwa iiyokomaa miwili
  • Maji safi vikombe viwili
  • Vipande vya barafu
  • Ndimu mbili
  • Blenda

Maandalizi

Hatua ya kwanza ni kuimenya miwa na kuikatakata vipange vidogo vidogo.

Ukimaliza vioshe uviweke kwenye chombo kisafi tayari kwa ajili ya kusaga.

Andaa blenda utakayoitumia kusaga miwa yako, kisha uanze kuweka vipande vichache vya miwa na maji robo kikombe kisha uanze kusaga.

Hakikisha blenda yako ina uwezo wa kusaga vitu vigumu (heavy duty blender) ukitumia blenda ya kawaida basi kata miwa kwa vipande vidogo vidogo zaidi na maji yawe mengi na uipumzishe kila baada ya dakika mbili ili kuzuia isiungue.

Kwa blenda yenye uwezo mkubwa saga kwa dakika tano mpaka saba kutengemea na wingi wa vipande vya miwa ulivyoweka.

Kwa blenda ya kawaida, saga kwa dakika mbili na kupumzisha blenda mpaka miwa ikisagika umimine kwenye chomo kisafi.

Unaweza kuongeza tangawizi wakati wa kusaga kama unapendelea.

Ukimaliza kusaga ichuje na uweke maji ya limao ulizoandaa mwanzoni.

Juisi hii haihitaji sukari hivyo mpaka hapo juisi yako itakuwa tayari kwa kunywa.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa