Njia rahisi za kutengeneza juisi ya tikiti

Na Lucy Samson
28 Oct 2022
Tikiti maji kama wengi wanavyopenda kuliita ni tunda ambalo limeundwa na asilimia 91 za maji. Lina faida nyingi kwenye mwili wa binadamu.  
article
  • Ni moja kati ya juisi rahisi unazoweza kutengeneza nyumbani
  • Haina haja ya kuongeza sukari kwenye utengenezaji wa juisi hii kwani tikiti lina wingi wa sukari ya asili

Tikiti maji kama wengi wanavyopenda kuliita ni tunda ambalo limeundwa na asilimia 91 za maji. Lina faida nyingi kwenye mwili wa binadamu.  

Faida za kula tunda hili kama zilivyoainishwa na jarida la healthline ni pamoja na kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo pamoja na kuboresha afya ya ngozi.

Juisi ya tikiti maji ni moja kati ya aina za juisi unazoweza kutengeneza kwa urahisi ukiwa nyumbani.

Fuatana nami kwenye makala haya ujifunze namna ya kutengeneza juisi ya tunda hili lenye ladha ya aina yake inayoweza kuburudisha kipindi hiki cha jua kali.

Maandalizi

Maandalizi ya kinywaji hiki yanaanza kwa kuliosha tunda lako na kulikata vipande vidogo kiasi.

Toa ganda gumu la nje kama inavyoonekana kwenye picha hapo chini.

Ukimaliza kutoa maganda katakata vipande vidogo, weka kwenye blenda na usage kwa sekunde 30 mpaka dakika moja kutegemea wingi wa matikiti yako.

Hamna haja ya kuongeza maji kwani tunda hili lina wingi wa maji yanayotosha kulifanya lisagike kwa urahisi bila maji ya ziada. Pia hakuna ulazima wa sukari kwenye juisi hii labda kama unapenda sukari nyingi.

Ukimaliza kusaga, chuja juisi yako na andaa maji ya limao au ndimu kwa ajili ya kuongeza ladha.

Ukishatengeneza maji ya ndimu vijiko vitano mimina kwenye juisi yako iliyokwisha kuchujwa na ukoroge.

Mpaka hapo juisi yako itakuwa tayari unaweza kuiweka kwenye friji, au kuongeza vipande vya barafu na majani ya mnaanaa(mint)kwaajili ya kuongeza harufu na ladha kisha ukaanza kuifurahia.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa