Unavyoweza kuandaa juisi (sharubati) ya stafeli na tende

Na Lucy Samson
9 Oct 2023
Mbali na utamu, juisi hii imesheheni Vitamini za kutosha zitakazo ufanya mwili wako kuwa na afya njema.
article
  • Ina wingi wa vitamini na madini yanayoweza kuimarisha afya.
  • Miongoni mwa faida ni kuimarisha mifupa na kuongeza damu.

Tende ni miongoni mwa matunda yaliyothibitishwa na wataalamu wa afya kuwa na faida lukuki mwilini mwa binadamu hasa pale linapotumiwa ipasavyo.

Licha ya baadhi ya watu  kutumia tunda hilo kama chakula kamili, kifungua kinywa au kutengeneza sharubati yake, limekuwa pia likitumika katika utengenezaji wa juisi (sharubati)  za matunda mengine ikiwemo stafeli.

Bila shaka unafahamu vyema utamu wa stafeli, sasa fikiria yachanganywe pamoja na tende utamu wake utakuwaje?

Mbali na utamu, matunda hayo yamesheheni Vitamini za kutosha zitakazo ufanya mwili wako kuwa na afya njema.

Tovuti ya afya ya Healthline inalitaja tunda la stafeli kuwa na wingi wa Vitamini C, Protini, madini chuma, ‘potassium’ na ‘magnezium’ huku  tende zikiwa na wingi wa Vitamin B6 na madini chuma yanayosaidia katika utengenezaji wa damu.

Makala hii inaangazia kwa undani jinsi ya kuandaa mchanganyiko wa matunda haya ili kutoa juisi tamu yenye ladha ya kipekee kulinganisha na aina nyingine ya vinywaji ili uweze kufaidi virutubisho vyake.

Hatua za utengenezaji wa juisi ya tende na stafeli

Maandalizi ya juisi ya stafeli na tende yaanaanzia kwa kuosha stafeli na kuchambua mbegu zote zilizopo katika tunda hilo.

Katika hatua hii umakini unahitajika kwani stafeli lina mbegu nyingi zilizojificha ambazo zisipotolewa zinaweza kuharibu blenda wakati wa kusaga.

Kisha maliza kuchambua mbegu kwenye stafeli, rudia zoezi hilo kwenye tende halafu uziloweke kwa nusu saa au zaidi kabla ya kuanza kusaga.

Baada ya kumaliza maandalizi andaa blenda kisha umimine stafeli ulilochambua mbegu, tende na kiasi cha maji.

Una2eza kutumia kisu kuchambua mbegu zilizopo ndani ya stafeli au ukatumia mikono kuhakikisha mbeguhizo haziingii katika kifaa cha kusagia.Picha|Galla plant.

Hapa unaweza kuamua kutumia stafeli nusu, tende ukapima kwenye kiganja kimoja cha mkono na maji ukaweka vikombe viwili au vitatu kutegemea uhitaji wako.

Saga vyote kwa pamoja mpaka vilainike, ikiwa unatumia blenda ya kawaida (isiyo na uwezo wa kusaga vitu vigumu) pumzisha blenda kila baada ya dakika mbili ili kuepusha kuungua au kuharibika mapema.

Hatua hiyo ikimalizika unaweza kuchuja juisi yako na ukaongeza sukari kiasi, au ukaamua kunywa bila kuchuja au kuongeza sukari kwani matunda yote tuliyotumia yana sukari.

Mpaka hapo kinywaji chako kitakuwa tayari kwa kunywa, unaweza kuongeza barafu au majani ya mnanaa (mint) kuongeza harufu na ladha.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa