Unavyoweza kuandaa mojito ya komamanga

Na Fatuma Hussein
6 Jan 2025
Ni chanzo cha nyuzinyuzi, vitamini, na madini muhimu ambavyo husaidia kuimarisha mwili.
article
  • Kinywaji hiki kinatumiwa na watu wa rika zote na wakati wowote.
  • Ni chanzo cha nyuzinyuzi, vitamini, na madini muhimu ambavyo husaidia kuimarisha mwili.

Komamanga ni tunda la kale linalojulikana kwa uwezo wake wa kustawi hata katika mazingira magumu. 

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya afya ikwemo tovuti ya  UCLA Health na Healthline, komamanga ni tunda lenye kalori na mafuta kidogo, lakini limejaa nyuzinyuzi, vitamini, na madini muhimu ambavyo husaidia kuimarisha mwili.

Mbegu za komamanga (arils) zilizopo ndani ya tunda moja la wastani zina kalori 234, protini gramu 4.7, mafuta gramu 3.3, wanga gramu 52, nyuzi nyuzi gramu 11.3, vitamini C asilimia 32, folate asilimia 27, magneziamu asilimia 8, fosforasi asilimia 8 na potasiamu asilimia 13. 

Kutokana na faida hizo jiko point imekuletea maandalizi rahisi ya mojito ya komamanga yenge faida kiafya na ladha nzuri.

Kwa wasiofahamu mojito ni kinywaji kinachohusisha mchanganyiko wa matunda, sirapu na aina nyingine ya vinywaji visivyotumia pombe.

Jinsi ya kuandaa hatua kwa hatua

Hatua ya kwanza ya uandaaji wa kinywaji hiki ni kuandaa juisi ya komamanga ambayo unaweza kutumia blenda ya kawaida kusaga ama kutumia blenda maalumu kwa matumizi ya juisi.

Baada ya kupata juisi ya komamangaiweke pembeni kisha andaa glasi (highball glass), weka sukari, majani ya mnanaa, na vipande vya limao.

Hatua inayofuata tumia “muddler” au kijiko kukandamiza mchanganyiko huo mpaka sukari iyeyuke kabisa.

Mchanganyiko ukiyeyuka vizuri ongeza juisi ya komamanga kwenye glasi hiyo kisha tia barafu kwa juu.

Hatua ya mwisho mimina maji ya soda (soda water) juu ya mchanganyiko na ukoroge taratibu kwa kutumia kijiko ili kuchanganya viungo.

Ikiwa hauna soda water unaweza kutumia soda za kawaida ikiwemo Sprite ili kuongeza ladha katika kinywaji chako.

Mpaka hapo mojito yako itakuwa tayari kwa kunywa hivyo unaweza kupamba glasi kwa kuweka mbegu za komamanga na kipande cha limao juu na kuongeza majani ya mnana ili kuleta harufu safi na muonekano wa kuvutia.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa