Vinywaji vitano vya kutumia wakati wa baridi

Na Lucy Samson
29 Jun 2022
Vinywaji hivyo ni pamoja na juisi ya limao, tufaa, zabibu, chungwa na chai ya tangawizi. Vinasaidia kuupa mwili joto.
article
  • vinywaji hivyo ni pamoja na juisi ya limao, na chai ya tangawizi
  • vipindi vya baridi vinatarajiwa kuwepo hadi Agosti

Kufuatia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutahadharisha  uwepo wa upepo mkali na hali ya ubaridi katika mikoa mbalimbali nchini ukiwemo Njombe kwa kipindi cha Juni hadi Agosti mwaka huu, zipo njia zinazoweza kutumika kujikinga na hali hiyo.

TMA katika tahadhari hiyo hivi karibuni katika uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa pamoja na hali ya hewa inayotarajiwa katika msimu wa kipupwe katika kipindi cha Juni hadi Agosti (JJA), 2022.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk  Ladislaus Chang’a alisema kwa kawaida, kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti (JJA), huwa ni kipindi cha baridi na upepo kwa maeneo mengi ya nchi. 

“Katika kipindi cha JJA, 2022 hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo, hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo ya ukanda wa pwani ya kaskazini pamoja na nyanda za juu kaskazini mashariki,” alisema Dk Chang’a.

Vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza mwezi Juni na Julai huku vipindi vya baridi kali vinatarajiwa katika maeneo ya miinuko ya nyanda za juu kusini magharibi hususan nyakati za usiku na asubuhi.

Katika kipindi cha miezi ya Juni na Agosti, 2022 vipindi vya upepo mkali vinatarajiwa kushamiri katika maeneo mengi nchini.

 Msimu wa Juni hadi Agosti 2022 unatarajiwa kuwa na upepo utakaovuma kutoka kusini-mashariki na mashariki (Matlai) katika ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu hususan mwezi Agosti, 2022.

Dk Chng’a alisema magonjwa ya mifugo yanayoambatana na baridi kama vile homa ya mapafu yanaweza kujitokeza

“Hali ya vumbi inayoambatana na upepo mkali katika baadhi ya maeneo inatarajiwa kujitokeza na inaweza kuathiri afya ya binadamu na wanyama,” alisema Dk Chang’a. 

Kutokana na hali ya baridi ambayo watu wanaipata kwa sasa, Jiko Point (www.nukta.co.tz) tumekuletea vinywaji vitano vya kutumia kipindi hiki cha baridi:

Chai ya tangawizi

Chai ya tangawizi ni nzuri katika kipindi cha baridi, kwani ina vitamini C kwa wingi na madini ya chuma ambayo huupa mwili joto zaidi. Kwa mujibu wa jarida la healthline, chai ya tangawizi inaweza kutumika pia kutibu magonjwa ya mafua na kikohozi yanayotokea sana wakati wa baridi.

Chai ya tangawizi inaweza kuongezwa viungo vingine kama karafuu na mdalasini. Kinywaji hicho husaidia kuongeza joto mwilini.

Juisi ya chungwa.Picha|Farhat Yummy.

Juisi ya chungwa

Chungwa lina kiwango kikubwa cha asidi, ambayo huchangia kuzalisha joto mwilini.

Mtaalamu wa usindikaji chakula na kuchakata vinywaji, Kivyera Banduka, anasema chungwa lina asidi nyingi, inayoweza kusaidia mwili kupata joto kipindi cha baridi.

“Asidi iliyopo kwenye chungwa inawezesha mfumo wa mwili kuzalisha joto zaidi, hivyo kuuwezesha mwili kustahimili baridi,” amesema Banduka.

Juisi ya limao

Banduka anasema kipindi cha baridi watu wengi hupata michubuko ya midomo na mafua mepesi, juisi ya limao inaweza kuwa kinywaji bora kwa kipindi hiki kwani vitamini zilizopo kwenye kinywaji huupa mwili uwezo wa kuzuia mipasuko ya midomo na mafua mepesi.

Juisi ya tufaa(Apple)

Juisi ya tufaa ni moja kati ya matunda yenye vitamini na viambata vya kulinda seli mwilini (antioxidants) 

Juisi ya tufaa pia ina wingi wa madini, ambayo yote ni muhimu kwa kudumisha afya njema na kuzuia maambukizi ya magonjwa.

“Juisi ya tufaa huongeza kinga ya mwili hivyo si rahisi mafua au homa za kipindi cha baridi kumpata mtu anayetumia tunda hili,” anasema Banduka.

Juisi ya zabibu

Zabibu ni miongoni mwa matunda yenye wingi wa vitamini C na asidi, hivyo hata juisi ya tunda hili pia itafaa wakati huu wa baridi.

“Matunda yenye kiasi kikubwa cha asidi au uchachu ndo mazuri katika kipindi hiki cha baridi,” amesema mtaalam huyo.

Matunda haya yanaweza kuchanganywa na matunda mengine, lakini ni vyema  matunda mengine yawekwe kwa kiasi kidogo..

Wakati ukinywa vinywaji hivyo, kumbuka, kuchukua tahadhari nyingine ikiwemo kuvaa nguo nzito au kutumia viyoyozi vinavyongeza joto kwenye nyumba.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa