Baada ya kufafanua kwa kina faida za matumizi ya mlonge kiafya leo tutaendelea mbele zaidi kujifunza jinsi unavyoweza kutumia mmea huu katika lishe ya kila siku.
Sehemu muhimu za mmea huu ambazo ziinaweza kutumiwa katika lishe na kuimarisha afya ni pamoja na majani, maua, mbegu na mizizi.
Kwa mujibu wa Afisa Lishe Pendo Majengo kutoka Halmashauri ya jiji ya mkoa wa Tanga, sehemu hizo za mlonge huwa na kiwango kikubwa cha virutubishi muhimu ikiwemo vitamini.
Majengo anaeleza kuwa sehemu muhimu kama majani imekuwa ikitumiwa kwa miongo mingi kurekebisha mifumo mbalimbali mwilini.
“Majani haya husaidia katika kuimarisha kinga ya mwili, na pia yana virutubisho vinavyosaidia katika mifumo tofauti ya mwili,’’ ameongeza Majengo.
Majani hayo yakikaushwa huweza kutumika kama kiungo cha mboga au kupikwa kama mboga kamili kama ilivyo kwa mchicha au sukuma wiki.
“Yanaweza pia kutumika kama mboga kabisa ukachuma majani malaini madogo yale mateke ukatengeneza kama mboga,’’ameeleza Majengo.
Aidha, majani yaliyokaushwa huweza kusagwa na kutumika kama unga unaochanganywa kwenye chai au uji.
Kwa upande wa tovuti ya Continental Hospital matumizi ya mlonge katika chakula ni rahisi na yanaweza kujumuishwa kwa njia tofauti ikiwemo katika supu, wali, au vinjwaji vya asili.
Unga huu unaweza pia kuchanganywa kwenye ‘smoothies’ na juisi ili kuongeza virutubisho mwilini.
Kwa mujibu wa National Libray of Medicine Mlonge hutumika pia kama dawa ya asili kwa mfano, juisi ya majani mabichi inaweza kunywewa kama tiba ya malaria au homa ya matumbo, huku mizizi na magome yake hutumika kwenye tiba za magonjwa ya ndani kama ini, figo na matatizo ya uzazi.
Mafuta yatokanayo na mbegu za mlonge hutumika kwa matumizi ya nje kama kupaka ngozi, nywele, au kutibu maambukizi madogo ya ngozi.
Njia hii ni bora kwa watu wenye changamoto ya kula majani mabichi au waliopo safarini.
Aidha, majani mabichi ya mlonge yanaweza kuongezwa kwenye saladi, kukaangwa na mboga.
Kwa wale wanaotafuta ubunifu zaidi, mchanganyiko mzito wa ya mlonge unaweza kutengenezwa kwa kuchanganya majani na karanga, vitunguu saumu na jibini.
Tahadhari katika matumizi ya mlonge
Ingawa mlonge ni salama kwa matumizi ya kawaida, si kila mtu anafaa kutumia kwa kiwango chochote bila ushauri wa daktari.
Tovuti ya Healthline inafafanua kuwa watu wanaotumia dawa za shinikizo la damu au kisukari wanashauriwa kuwa makini kwani mlonge unaweza kuathiri namna dawa hizo zinavyofanya kazi.
Aidha, wanaume wenye viwango vya chini vya testosterone wanapaswa kujadili matumizi ya mlonge na daktari kwani inaweza kuathiri homoni hizo.
Testosterone kulinga na tovuti ya Harvard Health ni homoni kuu ya jinsia kwa wanaume ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa mwanaume na maendeleo ya sifa za kiume.
Pia, matumizi ya mlonge kwa wingi bila kipimo huweza kusababisha madhara madogo kama kichefuchefu au mabadiliko ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.
Ingawa mlonge umehusishwa na manufaa mbalimbali ya kiafya lakini ushahidi wa kisayansi bado ni mdogo kuthibitisha usalama na ufanisi wake kwa matumizi mengi ya binadamu.
Kama ilivyo kwa virutubisho vingine vyote, Mamlaka ya Chakula na Dawa (FDA) haisimamii ubora wala usalama wa bidhaa za mlonge.
Hivyo basi, mtu hawezi kuwa na uhakika wa kiwango chake cha usafi au ubora. Ni muhimu kununua virutubisho kutoka kwa vyanzo vinavyoaminika na kufuata maagizo kwa uangalifu.