Ni furaha na vicheko kwa wafanyabiashara mkoani Singida hii leo mara baada ya bei ya jumla ya maharage mkoani humo kuendelea kusalia kuwa Sh400,000 kwa gunia la kilogramu 100.
Takwimu za mazao makuu ya chakula zilizotolewa na Wizara ya Viwanda na Biashara leo Oktoba 11, 2023 zinaonyesha kuwa bei inayotumika katika mkoani Singida ndiyo bei ya juu kuliko maeneo mengine nchini.
Hii ina maana kwa watumiaji wa nafaka hiyo mkoani humo watalazimikia kutoboa mifuko yao ili kuipata.
Hata hivyo, Bei wanayonunua wakazi wa Singida ni zaidi ya mara mbili ya bei inayotumika mkoani Sumbawanga ambao wananunua gunia la kilogramu 100 kwa Sh170,000.
Mbali na Maharage, bei ya mchele mkoani humo nayo haijapoa, ambapo gunia la kilogramu 100 linauzwa Sh350,000 ikiwa ndio bei ya juu zaidi Tanzania, bei ambayo inatumika pia katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.
Wakati huo huo, wakazi wa Morogoro wao ni ahueni, kwa kuwa mchele kwao unapatikana kwa bei nafuu tu ya Sh180,000 kwa gunia la kilo 100.
Hali ilivyo kwa mahindi na viazi
Kama unataka kununua mahindi leo kwa bei nafuu nenda mkoani Ruvuma au mkoani Rukwa na kama unataka kununua viazi kwa bei nafuu nenda mkoani Mtwara.
Bei ya mahindi Songea na Sumbawanga leo ni Sh68,000 kwa gunia la kilo 100, na bei ya viazi mviringo Mtwara ni Sh45,000.
Kwa mujibu wa Wizara ya Viwanda na Biashara hiyo ndio bei ya chini zaidi nchini Tanzania hii leo.
Wakati mahindi yakiuzwa kwa bei nafuu Ruvuma na Rukwa, bei imechangamka mkoani Mwanza huko wananunua gunia la kilo 100 kwa Sh115,000 bei ya juu zaidi Tanzania.
Bei ya juu ya viazi imerekodiwa mkoani Shinyanga ambako gunia la kilo 100 linauzwa Sh120,000 takribani mara tatu zaidi ya bei wanayonunulia mkoani Mtwara.