Kinara wa kuhamasisha matumizi ya gesi ya majumbani Tanzania

Na Esau Ng'umbi
12 Jul 2022
Ni Wema Grey anayetumia kazi yake ya kuuza gesi ya majumbani kutoa elimu kuhusu nishati hiyo ili kupunguza ukataji wa miti.
article
  • Ni Wema Grey alifanya kazi hiyo kwa muda wa miaka nane. 
  • Asisitiza wanawake kutumia nishati ya gesi ya majumbani (LPG)kama ajira.

Misitu ndiyo chanzo rahisi na kikuu cha nishati nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, zaidi ya asilimia 90 ya nishati ya kupikia inayotumika nchini inatokana na miti. Miti inayokatwa hutumika kupata nishati ya kuni na mkaa kwa matumizi ya kupikia.

Mwongozo wa mafunzi ya awali wa mpango wa kujihami katika kukuza mifumo endelevu ya nishati ya miti uliofanywa na Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Kilimo Misitu (ICRAF) na Chama cha Wadau wa Nishati Jadidifu (TAREA mwaka 2018, unaeleza kuwa Tanzania inashika nafasi ya saba kwa uzalishaji wa mkaa duniani.

Huchangia asilimia 3 ya uzalishaji wa mkaa wote duniani, kwa kiasi cha zaidi ya tani milioni 1.6 kila mwaka.

Ikiwa kama chanzo kikubwa cha ajira na kipato mjini na vijijini ICRAF na TAREA wawanaeleza mkaa huchangia zaidi ya Dola za Marekani milioni 2.7 sawa na Sh6.2 bilioni kwa mwaka katika uchumi wa Tanzania.

Wanawake wanachukua hatua

Ili kukabiliana na hatari ya kutoweka kwa miti Tanzania, wanawake katika maeneo mbalimbali wako mstari wa mbele kuchagiza nishati safi na salama ya kupikia ili kuokoa mazingira na afya za watu. 

Wema Grey ni miongoni mwao. Kwa nafasi aliyonayo katika kampuni ya kusambaza na kuuza gesi ya majumbani (LPG) ya Manjis anasambaza elimu ya matumizi ya nishati hiyo kwa watu mbalimbali wakiwemo wanawake. 

Wema ambaye ni Afisa Masoko wa Manjis amekuwa akizunguka maeneo mbalimbali kutekeleza shughuli za kampuni yake lakini anaitumia fursa hiyo kuwaonyesha wanawake wenzake fursa za kibiashara zilizopo kwenye LPG ambazo wakitumia vizuri zinaweza kuwatoa kimaisha, kulinda afya zao na kutunza mazingira yanayowazunguka. 

“Tumefanikiwa kufika sehemu kubwa ya Tanzania, mfano mikoa ya Mwanza, Tabora, Singida, Njombe, Dodoma, Arusha, Tanga, Manyara, Morogoro, Iringa, Mbeya, Musoma na Mara. Hayo ni baadhi tu ya maeneo tuliyofika, mwitikio ni mzuri ila ulikuwa unatofautiana kulingana na eneo husika kwa hiyo tulikuwa tunawaelimisha kwanza,” anasema Wema. 

Kila wanapokwenda hasa maeneo ya vijijini ambako nishati inayotumika zaidi ni kuni, wanatoa elimu ya manufaa ya kutumia gesi ya majumbani na kuachana na dhana potofu kuhusu nishati hiyo.

“Lazima mtoe kwanza elimu kisha wanaanza kununu, sehemu nyingine mpaka anunue mwenyekiti kwanza ndiyo watu wanaamini,” anasema Wema.

Matumizi ya gesi ya majumbani yanasaidia kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa. Picha| Otosection.

Anavyosambaza elimu ya nishati safi

Licha ya kutumia fursa ya maonyesho na kuzungumza na wateja, Wema katika kitengo chake cha masoko hutumia njia mbili ikiwemo mawakala wa bidhaa zao ambao hupelekewa bidhaa moja kwa moja kutoka kiwandani.

Magari ya matangazo yani ‘PA ’(Public Announcements) ambapo huwafikia moja kwa moja wanajamii na kuwaelimisha kuhusu fursa na faida za nishati hiyo.

Gesi ya majumbani ni fursa 

Kutokana na ongezeko la mahitaji ya nishati ya gesi katika shughuli mbalimbali, Wema anawashauri wanawake kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwa mawakala wa usambazaji wa nishati hiyo au kutumia nishati ya gesi katika shughuli zao. 

“Fursa ipo kwa wafanyabiashara hata sasa hivi kuna mawakala wengi sana wanawake. Gesi hivi sasa imekuwa bidhaa muhimu, nimeshuhudia wafanyabiashara wa kawaida wakikua kutokana na biashara ya gesi kwa sababu faida inayopatikana kwa kuuza gesi ni kubwa kuliko bidhaa nyingine,” anasema Wema na kubainisha kuwa, 

“Uendeshaji wake ni rahisi kwa sababu mteja mwenyewe anakuletea mtungi mtupu wewe unampa wenye gesi na sisi ndiyo tunampelekea dukani kwake na tunamuuzia kwa bei ya jumla ili tumuachie asilimia fulani kwa ajili ya faida na kiwango cha chini kabisa cha faida  ni Sh3,000.”

Mafanikio binafsi 

Amefaniukiwa kumudu gharama za maisha ya kila siku  na kuwa sehemu ya kuinua kampuni anayofanyia kazi. Ni baadhi  ya mafanikio anayojivunia Wema ambaye amefunga ndoa hivi karibuni huku akiwataka wanawake kujitokeza zaidi kutumia nishati ya gesi kama fursa.

“Mafanikio yapo, japo siwezi kutaja moja moja, naishi kwa kutegemea kazi hii, kampuni inapokua inaongeza faida hapo na sisi tunanufaika. Kiufupi kuna mambo mengi ambayo nimeyafanya kupitia kazi hii, kwa hiyo nawakaribisha wale wanaotaka kuwa mawakala wafike ofisi zetu zilizopo vijibweni Jijini Dar es salaam watapewa maelekezo na sifa zinazotakiwa,” anasema Wema.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa