Kutana na wanawake mashujaa watunza mazingira Dar

Na Lucy Samson
30 Jul 2022
Wanatengeneza mkaa mbadala kwa taka wanazokusanya mtaani ili kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa wa kawaida.
article
  • Wanabadili taka kuwa mkaa mbadala.
  • Mkaa huo pia ni sehemu ya wao kujiingizia kipato.

Ni majira ya 12:00 jioni jua likiwa linaelekea kuzama. Ni kawaida kwa muda huu kwa mama lishe katika Mtaa wa Msimbazi, Tabata jijini Dar es salaam kufunga biashara zao na kuelekea majumbani.

Ni tofauti kwa mwanamke huyu. Muda huu anautumia kukusanya mabaki ya vyakula kwenye vibanda vya mama lishe na katika soko la Tabata Muslim.

Siyo mabaki ya vyakula tu, bali hukusanya pia maganda ya viazi, mihogo na madafu ambavyo huvitumia kutengeneza mkaa mbadala kwa kushirikiana na wanakikundi wenzake tisa.

Ni Maimuna Hassan, mwanachama wa kikundi cha Fahari Yetu kilichopo Tabata Muslim katika Halmashauri ya Ilala kinachojishughulisha na utengenezaji wa mkaa mbadala kwa kutumia taka zisizo za plastiki ili kutunza mazingira ya mitaa wanayofanyia biashara na kuishi.

“Kilichotusukuma kuanza kutengeneza mkaa mbadala ni kutunza mazingira.. malighafi tunazotumia ni maganda ya mihogo, maganda ya ndizi, na madifu ya mnazi yakikauka tunachanganya na vifuu kisha tunachoma,” anasema Maimuna.

Taka hizo huzikusanya na kuzipeleka katika kiwanda kidogo cha kutengeneza mkaa kwa ajili kuunguzwa kabla ya kuchanganywa pamoja na uji wa muhogo na kupitishwa katika bomba maalum kupata mkaa. 

Wanachama wa kikundi cha Fahari Yetu wakiendelea na zoezi la kutengeneza mkaa mbadala katika kikundi chao kilichopo Tabata, jijini Dar es Salaam. Picha| Daudi Mbapani.

Walivyorithishwa maarifa ya mkaa mbadala

Kikundi hiki kilianza na wanachama zaidi ya 20 ambao walipatiwa mafunzo ya mkaa mbadala kutoka shirika lisilo kuwa la kiserikali la Forum For Climate Change (FORUMCC) mwaka 2019, ikiwa ni hatua ya kuwawezesha wanawake kutumia nishati safi na salama inayopunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mara baada ya kupata mafunzo hayo wanawake hawa waliamua kuanza kuutengeneza huku lengo kubwa likiwa ni kutunza mazingira ya eneo la Tabata na kujipatia kipato kupitia mkaa huo.

“Tulivyoanza tulikuwa tunatengeneza mkaa wa makaratasi, tulikuwa tunafinyanga karatasi tunatengeneza mkaa kadri tulivyoendelea na kupata mafunzo tulianza kutengeneza mkaa mzito kwa kutumia vifuu, maganda ya ndizi na takataka nyingine,” anasema Warda Omary, Mwenyekiti wa kikundi cha Fahari Yetu.

Hata hivyo, siyo wote waliendelea na safari ya kutengeneza mkaa huo, baadhi ya wanawake waliacha na kufanya shughuli zingine.

“Tulianza wengi lakini kama unavyotuona sasa hivi tumebaki watu 10 tu kwenye kikundi hiki,” anasema mwenyekiti huyo wa Fahari Yetu.

Utunzaji wa mazingira unalipa

Katika kikundi hicho chenye watu 10, kila mmoja anajishughulisha na kazi ya ziada ambayo huifanya kwa siku ambazo hawakutani kutengeneza mkaa huo.

Kwa siku wanaweza kutengeneza mkaa mbadala viroba viwili vya kilo 25, ambapo baada ya kukausha wanauza na pesa inayopatikana inaingizwa kwenye akaunti benki ya kikundi na kugawana mwisho wa mwaka.

“Kwenye kikundi chetu kila wiki tunatoa Sh12,000 kwa ajili ya akiba na kununua malighafi za kutengeneza mkaa mbadala, tukiuuza ile faida tunagawana” anasema Warda.

Mbali na kuwatunishia mfuko mwisho wa mwaka, mkaa huo unawapunguzia gharama za maisha kwani wanautumia kwenye shughuli za kila siku za nyumbani na migahawani.

“Huu mkaa ni mzuri sana unaweza ukajaza jiko ukabandika maharage yako na ukaivisha na kuyaunga kwa mkaa huo huo bila kuongeza tena,” anasema Getruda Nestory mwanachama wa  kikundi wa Fahari Yetu.

Mwalimu, kiongozi mpambanaji.

Kwa kipindi cha miaka mitatu, tangu kuanzishwa kwa kikundi cha Fahari Yetu kiwemeweza kutoa elimu hii ya wanawake zaidi ya 100, ambao kati yao wengine ni mama lishe na wauza mboga za majani.

“Huwa naitwa nikafundishe kwa mfano kama juzi niliitwa kufundisha watoto wa shule, nikaenda, si hivyo tu hata Forum CC wakinihitaji nikafundishe popote naenda,” anasema Warda.

Akiwa pamoja na wanakikundi wengine Warda anasema wanafundisha elimu hii ya ujasiriamali kwa gharama ndogo na kwa muda mfupi , ikiwa ni sehemu ya kuendeleza  utunzaji wa mazingira nchi nzima

“Kama mtu anataka kujifunza tunamkaribisha ada yetu ni Sh50,000 na tunafundisha kwa siku tatu tu mtu unakuwa umeshajua kila kitu, tayari  unakuwa na uwezo wa kutunza mazingira na kutengeneza pesa,” anasema Warda.

Vipande vya mkaa mbadala uliotengenezwa na kikundi cha Fahari Yetu. Picha| Daud Mbapani.

Kazi ya kutengeneza mkaa mbadala si lele mama

Huku akinionyesha sugu zilizopo  mikononi mwake Warda anaongea kwa huzuni na kusema “unaona hizi alama hii ni kwa sababu hatuna vifaa vya kisasa tunatengeneza kwa mikono”.

Wanachama wa kikundi hugawana majukumu licha ya kuwa na mchanganyiko wa umri tofauti wakiwemo vijana, mzee wa makamo mmoja na watu wazima wanne.

Kutokana na kikundi hicho kuwa na idadi kubwa ya watu wazima huwakwamisha kufanya uzalishaji mkubwa kwa wakati mmoja.

“Ni lazima utwange hizo taka taka baada ya kuchoma ili kupata unga mweusi, tunatwanga na mikono kwenye kinu, ukimaliza uchekeche alafu uje usonge  ni kazi ngumu kwakweli ” ameongeza Mwanahamisi Mbegu, mmoja wa wanachama wa kikundi hicho.

Ili kuongeza uzalishaji na soko, wanawake hao wangependa kusaidiwa mashine na vifaa vya kisasa. 

“Yani hapa tukipata tu vifaa sisi tunaweza kuzalisha zaidi ya hivi tunavyozalisha,” anasema Getruda Nestory  mmoja wa wanachama wa kikundi cha Fahari yetu ambacho huuza mkaa huo kwa mama ntilie na majumbani.

Ikiwa wanawake wataelekeza nguvu zao katika nishati hiyo, itasaidia kutunza mazingira na kuboresha maisha yao. 

Unaweza kuwasiliana na kiongozi wa kikundi cha Fahari Yetu, Warda Omary kujifunza zaidi ili nawe uweze kujiajiri kupitia namba 0712343601.

JikoPoint inaunga mkono watu wanaochochea matumizi ya nishati safi ya kupikia Tanzania kupitia habari. Hata hivyo, si sehemu ya biashara na miamala mtakayofanya na watu tunaowaandikia makala hizi. 

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa