Kutana na wanawake wanaobadili taka kuwa mkaa mbadala

Na Daniel Samson
25 Aug 2022
Wanapatikana Kipunguni jijini Dar es Salaam wanatumia taka za majumbani kutengeneza mkaa ambao unaounguza ukataji wa miti.
article

Wanapatikana Kipunguni jijini Dar es Salaam.
Wanatumia taka za majumbani kutengeneza mkaa ambao ni rafiki kwa mazingira.
Kazi hiyo inasaidia kupunguza ukataji wa miti Tanzania.


Utulivu umetawala katika mtaa huu. Watu wachache wanatembea katika barabara zenye usafi wa hali ya juu.

Tofauti na mitaa mingine iliyopo pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam, muonekano wa mtaa huu wa Mkolemba uliopo Kipunguni katika wilaya ya Ilala ni kuwavutia. Hakuna uchafu wowote kwenye barabara na nyumba zake.

Usafi wa mazingira ya mtaa huu ni matokeo ya uwezo mkubwa wa wakazi hawa kudhibiti taka zinazozalishwa katika nyumba zao. Taka hizo huzipeleka katika kiwanda kidogo cha kutengeneza mkaa mbadala kilichopo eneo hilo. 

Kiwanda hiki kinamilikiwa na kikundi cha Sauti ya Jamii ambacho kimesheheni wanawake walio mstari wa mbele kubadilisha taka kuwa mkaa mbadala ili kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti.

Hapa nakutana na mmoja wa wanachama wa kikundi ambaye yuko bize kutoa mkaa kwenye mashine na kuupeleka juani ili ukauke. 

Fatma Abdulrahman Talib (56), Mwenyekiti wa Sauti ya Jamii, anaeleza kuwa yeye na wenzake 18 wakiwemo wanaume wanatengeneza mkaa huo baada ya kupata mafunzo maalum kuhusu mkaa huo kutoka katika moja ya mashirika yanayojishughulisha na maendeleo ya wanawake.

Baada ya kujifunza walianza kutengeneza kwa kutumia mikono lakini baadaye walipata msaada wa mashine ya kuchakata mkaa huo kutoka Shirika la Amref Health Africa. 

Fatma na wenzie wanatengeneza mkaa mbadala ili kutunza mazingira, kuiweka mitaa yao safi lakini kutengeneza ajira kwa wanawake maskini kupata kipato kutokana na mkaa huo ili kuwapunguzia utegemezi. 

Mkaa huo ni mbadala wa kuni na mkaa na unaweza kutumiwa na kila mtu katika shughuli za mapishi kuanzia nyumbani, migahawani hadi katika maeneo yenye watu wengi ikiwemo shule. 

“Tunakusanya hizi taka tunatekeleza sera ya “mtaa poa” tunatunza mazingira baada ya hapo taka ni mali kwa mwanamke na atatunza afya yake nyumbani,” anasema Fatma, kiongozi wa kikundi hicho.

Mkaa huo mbadala ni rafiki kwa mazingira kwa sababu unapunguza ukataji wa miti, uzalishaji wa hewa ukaa na ni njia sahihi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine. 

Ripoti ya hali ya upatikanaji na matumizi ya nishati ya mwaka 2019/20 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa asilimia 88.2 ya kaya za jiji la Dar es Salaam zinatumia nishati ya mkaa kupikia huku zikitumia takriban asilimia 70 ya mkaa unaozalishwa Tanzania.

Hii ina maana kuwa kwa takriban kaya 9 kati ya 10 zilizopo Dar es Salaam zinatumia mkaa kupikia na magunia saba kati ya 10 ya mkaa unaozalishwa Tanzania yanatumiwa ndani ya jiji hili la biashara. 

Elimu hiyo ikiwafikia watu wengi itasaidia kupunguza kasi ya matumizi ya mkaa wa kawaida jijini humo na hivyo kuokoa miti inayokatwa kila mwaka nchini Tanzania.

Malighafi zinazotumika kutengeneza mkaa mbadala ikiwemo chenga za mkaa zikiwa tayari kupitishwa katika mashine maalum. Picha| Esau Ng’umbi.

Jinsi wanawavyotengeneza mkaa huo

Malighafi za mkaa huo ni taka mbalimbali ikiwemo mabaki ya vyakula, taka ngumu ambazo siyo plastiki, matawi ya miti, chenga chenga za mkaa, makaratasi, vifuu vya nazi, chenga za mkaa na uji wa muhogo.

“Yote haya tunachukua tunayaweka sehemu moja na kisha kuyatia kwenye tanuru, tunayageuza yanakua meusi kisha tunachanganya na zile chenga za mkaa, mabaki ya mbao na uji wa muhogo, tunatengeneza unakua mkaa mbadala,” anasema Fatma. 

Baada ya hapo mkaa huanikwa juani tayari kwa matumizi ya kupikia. 

Kwa mujibu wa Fatma, mama wa watoto watano, mkaa huo unaweza kuutengeneza kwa kutumia mikono lakini kupata mkaa mwingi kwa wakati mmoja, mashine ni chaguo sahihi.  

Sifa za mkaa huo ni kwamba hautoi moshi, unakaa muda mrefu kwenye jiko. Hadi sasa anasema baadhi ya watumiaji wameupokea vizuri wakieleza kuwa utawarahisishia maisha watu wenye kipato cha chini.

“Kwa hiyo nimemuwezesha mwanamke mwenzangu kiuchumi, ile Sh1,500 aliyokuwa akiitumia kununua mkaa itamsaidia mwanaye kwenda shule kesho asubuhi,” anasema Fatma kwa tabasamu huku akionyesha mafanikio makubwa. 

Uwezo wa uzalishaji

“Hii mashine inazalisha tani moja hadi mbili kwa siku. Tukishazalisha tunauanika, soko letu sisi mpaka sasa hivi liko ndani ya jamii, tunataka tusogee kwa wauza chipsi, majirani, mahoteli,” anasema Fatma ambaye amesomesha watoto wake kupitia kazi hiyo ya mkaa mbadala.

Hadi sasa wanatarajia kujitanua zaidi kimasoko kwa kuongeza uzalishaji ambapo kwa sasa kilo moja ya mkaa huo wanauza kwa Sh500 unaomwezesha mtu kutumia kwa siku moja kama ana familia ya watu wasiozidi wanne.

Fatma anasema katika kikundi cha kila mtu ni mchapa kazi kwa sababu kina idadi kubwa ya wanawake ambao wameamua kuweka utegemezi pembeni.

“Unaona katika zile kazi ngumu na sisi tunazifanya kwa sababu leo wanaume wapo kesho hapo, kwa hiyo na mimi lazima nijitahidi niweze kuzalisha hii kazi,” anasisitiza.

Hata hivyo, ili mkaa huo ulete matokeo mazuri unahitaji jiko maalum ambalo linapitisha hewa vizuri.

“Ninapompa mtu elimu ya jiko hili inabidi nimpe na elimu ya jiko,” anasema mama huyo na kubainisha kuwa kikundi chao kikiimarika wataanza kutengeneza majiko banifu. 

Mkaa mbadala wabadilisha maisha

“Mimi mwenyewe nimeweza kupata ajira nimeshajiajiri kutokana na kikundi changu. Manufaa ninayopata mkaa natumia, nimejiwezesha mimi na nimemuwezesha mwanamke mwenzangu nimemkomboa katika hali ya uchumi.” anasema Fatma akiendelea na kazi kutoa mkaa kwenye mashine kwa ajili kuanika juani.

Kupitia mkaa huo, Fatma anasema wameweza kumtua mzigo mwanamke wa nishati ya mkaa na kuni ambayo huaharibu mazingira lakini upatikanaji wake huihitaji muda na pesa.

“Wasikate miti waache miti ni uhai inatupatia afya. Tuwe tunatumia taka kuzalisha mkaa,” anasema Fatma ikiwa ni wito wake kwa jamii kuhusu kutunza mazingira.

Fatma Abdulrahman Talib, Mwenyekiti wa kikundi cha Fahari Yetu akionyesha tanuru linalotumika kuchomea taka za majumbani ambazo ni malighafi muhimu ya utengenezaji mkaa mbadala. Picha | Esau Ng’umbi.

Kibarua walichonacho kuongeza uzalishaji

Kikundi hicho cha Sauti ya Jamii, kinakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kuzalisha mkaa mbadala ikiwemo ukosefu wa eneo kufanyia shughuli zao.

“Tungekuwa na eneo letu tungekuwa na kiwanda kikubwa sana,” anasema Fatma kuwa wakipata eneo kubwa watatanua wigo wa kuzalisha mkaa huo na mbolea inayotokana na maji machafu ya mtaani.

Fatma anasema taka za majumbani ni fursa “nawaambia wamama fursa zipo nyingi. Unapopata changamoto ujue mbele iko fursa. Waje wajifunze kisha waende wakafanye majumbani mwao hata kama huna mashine.”

Unaweza kuwasiliana na Mwenyekiti wa kikundi cha Sauti ya Jamii, Fatma Abdulrahman Talib kupitia namba 0713865804.

JikoPoint inaunga mkono watu wanaochochea matumizi ya nishati safi ya kupikia

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa