Mapishi ya donati za‘Icing Sugar’

Na Fatuma Hussein
29 Feb 2024
Katika makala hii tutajifunza jinsi ya  kupika  donati za icing sugar kwa ajili ya familia au kwa ajili ya biashara.
article
  • Maandalizi yake hayatofautiani sana na yale ya maandazi ya kawaida

Donati au ‘Donut’ kwa lugha ya kiingereza ni mionngoni mwa vitafunwa vilivyojizoela umaarufu miaka ya hivi karibuni.

Kitafunwa hiki hutengenezwa kwa unga wa ngano na kuundwa kwa shepu ya duara huku aina mbalimbali za mapambo zikiwekwa kwa juu ili kuvutia zaidi walaji.

Miongoni mwa urembo unaowekwa ni ‘Icing sugar’ ambayo katika makala iliyopita tulijifunza jinsi inavyotengezwa kwa ajili ya vitafunwa au keki.

Katika makala hii tutajifunza jinsi ya  kupika  donati za icing sugar kwa ajili ya familia au kwa ajili ya biashara.

Donati moja huuzwa Sh500 hadi 1,000 katika migahawa yetu ya kawaida lakini katika migahawa yenye majina makubwa mjini unaweza kununua kwa gharama ya Sh2,000 hadi 3,000.

Ili kupunguza gharama hizo unaweza kutengeneza donati nyumbani kwa ajili yako mwenyewe au familia, pia unaweza kujifunza kwa ajili ya kuvutia wateja katika mgahawa au hoteli yako.

Namna ya kupika donati

Maandalizi ya donati hayana tofauti sana na yale ya maandazi ya kawaida, hivyo anza kwa kuandaa unga wa ngano kwa kutoa uchafu wote unaoweza kuwepo, unaweza kuchekecha ikiwa unataka kupika donati nyingi.

Baada ya hapo vunja mayai katika bakuli safi ongeza hamira kijiko kimoja kwa kila kilo ya ngano, hamira nusu kijiko, ‘baking powder’ robo kijiko, vanila na sukari kiasi unachopendelea.

Endelea kwa kuchanganya mahitaji yote kwa kutumia mwiko au mashine maalum ya kuchanganyia kwa muda wa dakika 10 au zaidi.

Baada ya hapo weka siagi kiasi, unaweza kutumia iliyoyeyushwa na kama hauna unaweza kutumia mafuta kiasi kisha ongeza unga na unaze kukanda taratibu huku ukiongeza maziwa au maji.

Ukilainika sukuma na ukate shepu ya duara  kwa kutumia glasi au mfuniko mpana wa chupa kisha utumie chombo chenye umbo la duara dogo kukata katikati.

Ikiwa hauna icing sugar unaweza kutengeneza donati za kawaida kwa kufata hatua tulizokuandalia.Picha|Lola Kitchen

Rudia hatua hiyo kwa ngano iliyobakia kisha uyaache ya umuke kwa dakika 30 zaidi.

Yakiumuka kiasi cha kutosha bandika mafuta jikoni na yakichemka uanze kuchoma donati zako kwa moto mdogoo mdogo mpaka yatakapo badilika rangi na kuwa ya kahawia.

Ukitoa kwenye mafuta yachuje mafuta na kabla hayajapoa yachovye kwenye icing sugar  kwa upande wa juu.

Unaweza pia kuyatandaza mezani au kwenye sinia  na kunyunyiza icing sugar kwa juu ili yaenee katika sehemu zote, ukimaliza acha yapoe na yatakuwa tayari kuliwa.

Mpaka hapo pishi la donati litakuwa tayari kwa kuliwa au kwa biashara.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa