Martha Biseko: Kutoka majiko ya umeme hadi mkaa mbadala

Na Mariam John
1 Aug 2022
Martha Biseko alianza biashara ya kuuza mkaa mbadala unaopunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni baada ya kuibiwa majiko ya umeme.
article
  • Kuibiwa vifaa vya umeme kulimshawishi kuanza kutumia mkaa mbadala.
  • Mkaa huo anatengeneza kwa taka ikiwemo vumbi za mbao.
  • Mkaa huo unatunza na mazingira na kumuingizia mkazi huyo wa Mwanza.

Miaka kadhaa iliyopita, ulikuwa huwezi kumwambia chochote kuhusu kuni na mkaa. Vilikuwa vyanzo vikuu vya nishati ya kupikia nyumbani kwake.

Baada ya kupata elimu kuhusu nishati safi na salama ya kupikia, sasa amekuwa mtumiaji na mwalimu wa wengine wa mkaa mbadala.

Martha Biseko (56), mjasiriamali wa mkoani Mwanza anatengeneza mkaa mbadala unaotokana na taka mbalimbali zisizo za plastiki ikiwemo mabaki ya mimea ikiwemo mpunga.

Anasema taka zinazotupwa ni malighafi muhimu ya kutengeneza mkaa mbadala na kuwa mkaa huo unasaidia kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Mkaa huo pi ukiwaka ni haraka kwenye kupikia na mpishi atalazimika kutumia muda mchache tofauti na yule anayetumia kuni au mkaa wa kawaida.

Anaamini kuwa ni vigumu kumuhamasisha mtu kuachana na matumizi ya mkaa na kutumia gesi au umeme lakini ni rahisi kumuhamisha kutumia mkaa mbadala.

Alianzaje kutengeneza mkaa mbadala 

Kabla ya kuanza kutengeneza nishati mbadala, Martha alikuwa anajishughulisha na uuzaji wa vifaa vya kieloktroniki yakiwemo majiko ya umeme.

Aliacha shughulia hiyo mwaka 2016 baada ya duka lake kuvunjwa na vifaa vyote kuibwa. 

“Sikuwa na ziada ya fedha ya kwenda kununua vifaa vingine nilivunjika moyo hasa nikiangalia sina mtu wa kunisaidia kuendeleza ndoto yangu, mme wangu alishafariki siku nyingi na nilikuwa na madeni sana hivyo ilinikatisha tamaa kuendelea na biashara hasa baada ya kumaliza kulipa madeni yote,” anasema Martha.

Kutokana na changamoto hiyo, Martha iliamua kuangalia njia nyingine itakayosaidia katika kujiongezea kipato lakini pia kuokoa matumizi ya kuni na mkaa kwenye mapishi.

Anasema toka zamani hakuwa anakubaliana na matumizi ya kuni kwenye mapishi kwa kuwa chakula hivyo aliona njia rahisi ni kutumia gesi au mkaa.

Alipata wazo la kuanza kutengeneza mkaa mbadala unaotokana na vumbi au takataka mkaa baada ya kujifunza katika moja ya taasisi zinazofundisha mkaa huo.

Baada ya kutembelea na kujionea mkaa unavyoandaliwa, alijiuliza kwa nini watu wanachoma kuni nyingi na wanapata mkaa kidogo huku uvunaji huo wa miti ukisababisha uharibifu wa mazingira ndipo akaanza kutengeneza mkaa mbadala.

Mkaa mbadala unasaidia kupunguza ukataji wa miti na kuwawezesha wanawake kutengeneza kipato kwa wauzia watu wengine. Picha| Mwananchi

Anavyotengeneza mkaa mbadala

Ili kupata mkaa mbadala, Martha anasema anahitaji mabaki ya mimea mfano maranda ya mbao, maganda ya karanga, pumba hata majani ya mpunga.

“Kwenye uchomaji mkaa wa kawaida, mtu anahitaji miti ambayo akichoma kuna sumu inabaki mule tofauti na inavyokuwa kwenye maandalizi ya mkaa mbadala unaotumia mabaki ya mimea ambayo hujumuisha vitu vidogo vidogo ambavyo vikichomwa kwenye tanuru vinaungua na kubaki vumbi jeusi,” anasema mama huyo.

Vumbi hili ndilo hutumika kutengenezea mkaa mbadala, hii ni baada ya sumu zote kuwa zimeondoka ambazo hata baada ya matumizi ya muda mrefu, mtumiaji hawezi kupata athari za kiafya kama maradhi ya kifua.

Kupatikana kwa vumbi hilo ambalo huchanganywa na gundi ambayo kwa kawaida, hutumia udongo mfinyanzi na kukoroga kwa pamoja kugundisha vumbi la mabaki yaliyochomwa.

Pia unaweza kutumia unga wa muhogo uliochanganywa na maji huku mkaa huo akiuza Sh 2,000 kwa kilo moja.

Anasema uwakaji wa mkaa mbadala ni kati ya saa tatu hadi nne kwa jiko la kilo moja linalomuwezesha mama kuivisha vyakula vyote bila kuongeza mkaa hivyo kupunguza kiasi kinachotumika ikimaanisha fedha kidogo zinatumika kwa kila familia au kaya.

Kwa hesabu zake, anasema kilo moja ya mkaa mbadala ni sawa na kilo nne hadi tano za mkaa wa kawaida.

Kipato chake kipoje

Biseko anasema kutokana na kutengeneza mkaa huo umeongeza kipato chake na kuweza kuhudumia familia.

Wakati marehemu mume wake alipofariki aliwaacha kwenye nyumba ambayo walikuwa wamejenga hivyo kipato anachopata sasa ni kuhudumia familia kwenye mahitaji ya shule na kula.

Anasema mwitikio wa watu kununua mkaa huo siyo mkubwa kama ule wa mkaa wa kawaida au kuni na kwamba kwa siku anaweza kuuza kilo 5 hadi 10.

“Mkaa unakaa muda mwingi kwa mfano ukichukua kilo moja huwezi kutumia zote unaweza kupanga mikaa mitatu hadi minne kwenye jiko,  likishashika anza kupika chakula chako hadi utakapoivisha,” Martha anaeleza.

Amewahi kutumia nishati nyingine mbadala 

Tofauti na kutumia mkaa mbadala kwenye mapishi nyumbani kwake, Biseko anasema jiko ambalo alikuwa analitumia ni la umeme. Anasema jiko hilo linarahisisha kwenye kupika na kuokoa fedha muda, afya na mistu.

Anasema tofauti na imani za watu kuwa umeme ni ghali anathibitisha kuwa sio sahihi kwa kwa mtumiaji wa jiko la umeme anaweza kutumia chini ya uniti mbili za umeme kwa siku kwenye mapishi yake.

“Si kweli kwamba matumizi yaumeme kwenye kupikia yanamaliza umeme hapana! kabla ya kuanza kutumia nishati mbadala nilikuwa natumia jiko hili kwanza ni haraka, rahisi na linaokoa muda,” anasema Martha.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa