Mfahamu mjasiriamali anayetengeneza mkaa mbadala kwa vumbi

Na Mariam John
26 Aug 2022
Anatumia vumbi la mkaa mbadala, maji na udongo wa mfinyanzi kutengeneza mkaa huo unaopunguza ukataji wa miti na kumsaidia kuingiza kipato.
article
  • Anatumia maji, udongo wa mfinyanzi na vumbi la mkaa wa kawaida.
  • Mkaa huo unapunguza ukataji wa miti na kufungua milango ya ajira.
  • Ni rahisi kuutumia na utunza afya za watumiaji wake.

Wakati wengine wakifikiri vumbi la mkaa ni taka, kwa mama huyu ni tofauti. Ni fursa ya kuboresha maisha na mazingira yanayomzunguka.

Abigael Martin (65), mkazi wa jijini Mwanza anatumia mabaki hayo ya mkaa  kutengeneza mkaa mbadala ambao wataalam wa mazingira wanaeleza kuwa unapunguza kasi ya ukataji wa miti ili kupata nishati ya kupikia ya kuni na mkaa.

Abigael alianza kazi hiyo miaka miwili iliyopita baada ya kujifunza kwa kuangalia  video fupi ya mtandaoni  ya kijana mmoja ambaye alikuwa anatengeneza mkaa mbadala kwa kutumia taka.

Awali mjasiriamali huyo wa nishati safi ya kupikia alianza kutengeneza mkaa mbadala unaotokana na pumba za mpunga lakini baadaye alipata wazo la kutumia vumbi la mkaa.

Alifikia uamuzi huo baada ya kushuhudia kutapakaa kwa mabaki ya mkaa ikiwemo vumbi katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo. Changamoto hiyo ikawa fursa kwake kutunza mazingira kwa kupunguza taka hizo mitaani na masokoni.

“Nilianza kutengeneza mkaa wa kupikia mwenyewe nyumbani baada ya kujiridhisha kuwa unawaka ndipo nikaanza kutengeneza kwa ajili ya kuuza ili niweze kupata fedha ya kujikimu,” anasema Abigael.

Mkaa huo unatengenezwaje?

Kwa kutumia mchanganyiko wa udongo wa mfinyanzi, vumbi la mkaa na maji tayari unaweza kutengeneza mkaa huo. Hakikisha kuna uwiano mzuri wa vipimo kwa kila malighafi ili kupata mkaa uliokamilika.

Anasema baada ya kuchanganya vizuri mchanganyiko huo, unakata madonge kiwango unachotaka kisha unauanika juani kwa muda siku tatu na utakuwa tayari kwa kupikia.

“Changamoto ni kwenye masika ambapo jua huwa ni la shida hivyo tunashindwa kutengeneza mkaa mwingi kwa kuhofia kuwa utanyeshewa na mvua,” anasema Abigael.

Alianza na mtaji wa kiasi gani?

Kiasi cha Sh3, 000 ndicho kimemfikisha hapa, ambapo alianza kwa kununua debe mbili za vumbi la mkaa pamoja na udongo na shughuli ya kutengeneza mkaa huo ilianza.

Abigael anakiri kuwa kazi hiyo sio sawa na mkaa bure kwa sababu hakosi fedha ya kujikimu na kulipia kodi.

“Inategemea na siku yenyewe lakini kwani kuna wakati nauza debe sita hadi saba, mfano jana nilipeleka ndoo sita za lita 10 eneo la Mkuyuni niliziuza zote na nikapata Sh12,00 lakini pia wateja wa kuja nyumbani kununua kila siku wapo,” anasema Abigael, mama wa watoto wanne.

Kwa siku mauzo katika biashara yake ambayo inakua kila siku ni Sh20,000.

Mkaa wake anauzaje?

Kiwango cha chini cha mkaa huo huanzia Sh500 ambapo mteja huhesabiwa madonge 18 ya mkaa huo, huku kwa debe moja kwa mteja aliyefuata nyumbani ni Sh1,500 huku anayeukuta sokoni huuziwa Sh2,000.

 Kilichomsukuma kufanya shughuli ya kutengeneza mkaa mbadala ni kutunza mazingira na kuacha kazi yake ya kwanza ya kutengeneza sabuni, mishumaa, batiki ambayo anaamini ilikuwa inamletea madhara kiafya.

“Niliacha kazi hiyo ingawa nilifuzu vizuri mafunzo hayo na ilikuwa inaniingizia fedha, na sababu kubwa ni kutokana na matumizi ya kemikali lakini pia mtaji wake ni mkubwa hivyo sikuweza kumudu,” anasema.

Abigael Martin akiangalia mkaa mbadala alioanika kabla ya kuanza kuutumia. Picha | Mariam John.

Anatumia njia gani kutangaza biashara yake?

Abigael anakiri kuwa mkaa huo kwa sasa unajiuza wenyewe tofauti na zamani walipokuwa wanatafuta wateja. 

Mtu anapouchukua kwenda kuutumia mwingine anapouona na yeye anatamani kuunnuua hivyo wanaenda wanapokezana mmoja baada ya mwingine.

Anasema moja ya sifa za mkaa huo unapunguza uharibifu wa mazingira kwa aji ya  kuni au mkaa wa kawaida.

Faida ya mkaa huo kwa wapishi ni kuwa unakaa muda mrefu jikoni hasa kama mtu anatumia jiko banifu. Kwa wastani unakaaa saa nane, hivyo unaweza kupikia chakula chochote ikiwemo makende na maharage.

Kibarua alichonacho

Pamoja na faida za mkaa huo, Abigael anakumbana na changamoto ya kukosa mtaji na kwamba matamanio yake ni kupata mtaji mkubwa ili aweze kutengeneza mkaa mwingi na kuuza.

Pia anatamani kupata fedha kwa ajili ya kununua mashine ya kukaushia mkaa huo wakati wa mvua ambayo inauzwa Sh20,000.

“Natamani wanawake tungejiunga na kuanzisha kikundi cha kutengeneza mkaa huo ili tuweze kwenda halmashauri kuomba mkopo usiokuwa na riba ili tuweze kukuza mtaji,” anapendekeza Abigael.

Kutokana na mtaji wake kuwa mdogo, mjasiriamali huyo hajaajiri mtu yeyote bali ana vibaura wanaomtafutia udongo au kumbebea mkaa wake anapoenda sokoni kuuza.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa