“Nilikuwa nikinunua majiko ya kawaida natumia lakini baada ya muda mfupi yanaharibika nalazimika kununua mengine jambo ambalo lilikua linaumiza akili yangu ni wapi nitapata jiko ambalo linaweza kudumu kwa muda mrefu.”
Hiyo ni kauli ya Happyness Boniphace, mjasiriamali anayetengeneza majiko banifu yanayotumia mkaa kidogo Jijini Mwanza.
Happyness (38) anasema majiko hayo siyo tu yanamsaidia kumuingizia kipato bali yanapunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.
Kabla ya kuanza shughuli ya utengenezaji wa majiko hayo alikuwa anajishughulisha na utengenezaji wa viungo vya chai na pilau shughuli ambayo ameifanya toka alipohitimu elimu ya kidato cha nne.
Nini kiliwasukuma kutengeneza majiko hayo?
Happyness, mkazi wa Nyakato jijini hapa anasema kutokana na changamoto ya majiko ya kawaida kutumia mkaa mwingi lakini pia kuharibika haraka, yeye na mume wake Dominian waliamua kutafuta mzizi utakaosaidia kutibu changamoto ya uharibifu wa majiko mara kwa mara lakini pia kupunguza matumizi makubwa ya kuni na mkaa.
Baadaye walijiunga na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Mwanza mali kupata elimu ya utengenezaji wa majiko banifu yanayotumia nishati mbadala wazo ambalo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa na kuwa watengenezaji wakuu wa majiko yanayotumia gesi na mkaa kidogo.
Walianza kazi ya utengenezaji wa majiko hayo mwaka 2018 wakati huo wakiwa na mtaji wa kumudu kutengeneza majiko mawili tu yanayotumia mkaa kidogo na yenye kuhifadhi joto kwa muda mrefu.
Majiko hayo yanatengenezwa kwa kutumia chuma, bati na udongo ambao huwekwa katikati ya jiko ili kusaidia kutunza joto.
“Jiko letu linaokoa gharama za maisha ambapo kopo moja la mkaa linalouzwa Sh1, 000 linaweza kutumika kwa siku mbili kwa kuwa mtumiaji atapaswa kuweka mkaa kidogo kisha unawasha kama unavyowasha jiko la kawaida,” anasema Happyness.
Mwitikio wa watu kununua majiko hayo upoje?
Tofauti na miaka ya nyuma ambapo mwitikio wa watu kununua majiko hayo ulikuwa mdogo, Happyness anasema kwa sasa biashara hiyo inauzika maeneo mbalimbali ya nchi na wateja wanawafuata kununua Sido na katika maonyesho mbalimbali ikiwemo Nane Nane.
Yeye na mume wake wanatengeneza majiko hayo kwa ukubwa tofauti ambapo kwa upande wa majiko ya mkaa wanatengeneza majiko kuanzia madogo wanayouza Sh65, 000, ya kati ya Sh75,000 na kubwa kwa sh 100, 000.
Majiko ya gesi nayo inaweza kuwa chaguo lako
Majiko yanayotumia gesi, Happyness anasema pia wanatengeneza kuanzia jiko dogo la sahani moja ambalo huuzwa kwa Sh130,000, jiko la kati Sh250, 000 na jiko kubwa ambalo linaweza kupika sufuria la kilo 50 anauza kwa Sh400,000.
“Kwa sasa majiko haya yanapendwa na wengi hasa wapishi wa mahotelini na mashuleni na matumizi yake kwenye gesi ni madogo tofauti na anayetumia jiko la gesi la kawaida kwani mtumiaji anaweza kupunguza moto pale udongo utakaposhika joto na kumwacha mpishi akiivishia chakula kutokana na joto la udongo,” anasema Happyness.
Anasema mbali na kutumia maonyesho ya sikukuu ya wakulima ya Nane Nane kutangaza bidhaa zao pia wanatumia mitandao ya kijamii kuwafikia wateja wao.
Pamoja na mafanikio aliyoyapata, Happyness anasema kupanda kwa bei za malighafi anazotumia kutengeneza majiko hayo ikiwemo vyuma, udongo maalumu ni changamoto kubwa inayowarudisha nyuma.
Bajiko banifu ni ajira
Happyness amefanikiwa kuajiri wafanyakazi wanne ambao humsaidia katika kutengeneza majiko hayo ambapo kwa siku wanaweza kutengeneza majiko matano hadi 10 kama kuna vifaa vyote muhimu vinavyohitajika.
Malengo yake ya baadaye ni kuwa na kiwanda kikubwa cha kutengeneza majiko ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na matumizi ya mkaa na kuni.
Ni maono yake kuwa siku moja Tanzania iachane na matumizi makubwa ya nishati ya kuni na mkaa na badala yake waanze kutumia majiko gesi au yale yanayotumia mkaa kidogo ili kutunza mazingira.