Mwalimu anayetoa maarifa ya kujiajiri kupitia mkaa mbadala Tanzania-1

Na Daniel Samson
25 Jul 2022
Ni Tausi Msangi mkazi wa Kipunguni jijini Dar es Salaam anayetengeneza na kufundisha kuhusu mkaa huo unaotokana na taka za majumbani.
article
  • Ni Tausi Msangi aliyejifunza kutengeneza mkaa huo miaka nane iliyopita.
  • Anatoa elimu hiyo kwa wanawake kulinda afya zao, kuongeza kipato na kutunza mazingira.
  • Mkaa huo ni ule unaotokana na taka za majumbani.

Ni miaka zaidi ya nane sasa tangu ajifunze kutengeneza mkaa mbadala kutoka katika moja ya taasisi inayojihusisha na wanawake na jinsia jijini Dar es Salaam.

Mafunzo hayo aliyopatiwa Tausi Msangi, mkazi wa Kipunguni katika Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, yamekuwa kama mbegu iliyofukiwa kwenye udongo mzuri. Sasa inamea na kusambaa kila mahali Tanzania.

Tausi sasa amekuwa ni miongoni mwa walimu maarufu wanaofundisha wanawake na wanaume jinsi ya kutengeneza mkaa mbadala nchini, ujuzi ambao umetawaliwa na wanaume zaidi. 

Balloon Content

Mkaa unaokoa mazingira

Mkaa huo, anaotenegeneza Tausi, unatokana na taka mbalimbali ikiwemo mabaki ya vyakula, matawi ya miti, chenga chenga za mkaa, makaratasi, vifuu vya nazi, chenga za mkaa,  uji wa muhogo na taka ngumu zisizo za plastiki,

Malighafi hizo huchanganywa pamoja na kupitishwa katika mashine maalum ambayo hukata vipande vidogo vidogo kisha kuanikwa juani kwa ajili ya matumizi.

Kwa wasio na mashine, wanaweza kutengeneza mkaa huo kwa kutumia mikono lakini uzalishaji unaweza usiwe mkubwa kwa kuwa mikono inapunguza ufanisi. 

Mkaa huo, ambao ni rahisi kuutengeneza, unasaidia kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa na kuwawezesha wanawake kama Tausi kujipatia kipato kwa ajili ya kuendesha maisha.

Tausi (39) tangu alipopata mafunzo, hajawahi kukaa kimya bali amekuwa akifundisha wengine ili kuisaidia jamii iachane na nishati chafu inayoharibu mazingira na wajikite katika nishati safi ya kupikia inayoboresha maisha hasa ya wanawake.

“Mimi tukiwa na wenzangu tukasema hapa hili jahazi lazima tulipeleke na ni lazima wanawake tuwakomboe kwenye hili suala la matumizi makubwa ya mkaa na kuni,” anasema Tausi.

Tausi anasema yeye ni mwathirika kiafya na matumizi ya kuni na mkaa, hivyo hapendi kuona wanawake wenzie wanaendelea kupata madhara zaidi. 

“Nilikuwa mhanga wa mimba za utotoni kwa hiyo sitamani tena kumuona msichana anapitia kile nilichopitia, najitahidi kuwekeza nguvu zangu kufundisha,” Tausi anaeleza akiwa pembeni mwa kiwanda kidogo cha kutengeneza mkaa mbadala kilichopo Kipunguni kilomita 19.7 kutoka katikati mwa jiji.

Sehemu ya kiwanda kidogo kilichopo Kipunguni Jijini Dar es Salaam kinachotengeneza mkaa mbadala. Picha| Suleman Mwiru.

Awafundisha zaidi ya watu 400

Mama huyo, mwenye familia ya watoto watatu, anasema mpaka sasa ameweza kuwafikia watu zaidi ya wanawake 400 tangu alipoanza kufundisha mwaka 2018 wakiwemo wanawake waliopo kwenye vikundi vya ujasiriamali. 

“Tumeweza kufundisha zaidi ya vikundi 10 mpaka sasa hivi na asasi za kiraia ndogo ndogo na watu wanaitikia kwenye hili suala la huu mkaa kwa sababu wanaupenda na unawasaidia,” anasema Tausi. 

Tausi anasema wanawake waliofikiwa na elimu hiyo wameanzisha miradi ya kutengeneza mkaa huo kwa ajili ya kujiingizia kipato, jambo lililosaidia kuwapunguzia utegemezi kwa waume zao.

Jambo kubwa analojivunia mwalimu huyo katika kazi yake ya kueneza maarifa ya mkaa mbadala ni kuwa kila atakaposimama kuongea kuhusu nishati hiyo na manufaa yake anasikilizwa na anayosema yanatendewa kazi.

“Nashukuru hakuna sehemu ambapo nimeenda kufundisha sijazalisha walimu zaidi ya watano na watu wanatumia,” anasisitiza.

Mmoja wa wanawake waliopita katika mikono yake ni Queen Steve, Mkazi wa Kipunguni jijini hapa. Queen anasema alipata mafunzo hayo baada ya Tausi kumtembelea nyumbani kwake.

Tangu wakati huo, binti huyo mwenye miaka 24, amekuwa akitengeneza mkaa huo ambao umemsaidia kupata kipato cha kuendesha maisha.

Tausi siyo tu anafundisha kuhusu mkaa mbadala bali amekuwa amekuwa akitoa elimu ya utengenezaji wa bustani, upandaji wa miti na maua ya kibiashara na kuwasaidia wanawake kujiajiri katika shughuli ndogo ndogo za maeneo wanayoishi.

Anafundisha anachokiishi

Mwanamke huyo siyo tu anafundisha kuhusu utengenezaji wa mkaa mbadala bali ni kazi yake ya kila siku inayomuingizia kipato. 

Yeye ni miongoni mwa viongozi katika kikundi cha Sauti ya Jamii ambacho kina wanachama 18 wanaojihusisha na utengenezaji wa mkaa huo ambao wanauza kwa matumizi ya nyumbani, shuleni, migahawani na taasisi mbalimbali. 

Kiwanda kidogo cha kikundi hicho kilichopo Kipunguni kimekuwa kama kituo cha mafunzo kwa sababu karibu kila wiki hupokea wageni wanaokuja kujifunza namna ya kutengeneza mkaa huo. 

“Nimekuwa nikiwafundisha watu tofauti, ambao nao tayari wamekuwa walimu. Watu wanakuja kujifunza, wengine kutoka Zanzibar,” anasema Tausi ambaye ni Katibu katika kikundi cha Sauti ya Jamii.

Unaweza kuwasiliana na mwalimu wa mkaa mbadala Tausi Msangi kujifunza zaidi ili nawe uweze kujiajiri kupitia namba 0713865804.

JikoPoint inaunga mkono watu wanaochochea matumizi ya nishati safi ya kupikia Tanzania kupitia habari. Hata hivyo, si sehemu ya biashara na miamala mtakayofanya na watu tunaowaandikia makala hizi. 

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa