Saa 6:00 mchana katika moja ya nyumba zilizopo Mtaa wa Kipunguni jijini Dar es Salaam sufuria iliyofunikwa juu ya jiko la mkaa unaowaka sawia inapenyeza harufu ya nyama ya ng’ombe.
Mpishi wa chakula hicho Queen Steve anasema tangu aweke mkaa wake jikoni tangu saa 4:00 asubuhi hajaongeza mkaa mwingine na nishati hiyo hiyo awali alipikia chai na sasa anaendelea na chakula cha mchana.
Tofauti na mkaa mwingine wa miti ya porini, nishati anayotumia Queen ni mkaa mbadala unaotokana na mabaki ya taka za nyumbani ikiwemo maboksi, chenga za mkaa, vifuu vya nazi, majani ya miti na taka nyingine za nyumbani isipokuwa zenye asili ya plastiki.
Utengenezaji wake ni rahisi, anasema. Unachanganya malighafi hizo pamoja na uji wa muhogo kisha unaunda maumbo madogo madogo na kuanika juani kabla hujatumia.
Queen (24) anasema ameanza kutumia mkaa huo kwa zaidi ya miaka miwili iliyopita baada ya kupewa elimu na mmoja wa walimu wa mkaa mbadala aliyekuja kumtembelea nyumbani kwake.
Sasa halazimiki tena kutumia kuni au mkaa wa kawaida kwa sababu mkaa anaotumia ni salama kwa afya yake hautoi moshi na unakaa muda mrefu kwenye jiko.
Sifa nyingine ya mkaa huo ni rafiki kwa mazingira kwa sababu husaidia kupunguza uchafu mitaani hasa kuziba kwa mitaro na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.
“Kwa sasa taka zetu tunatengenezea mkaa. Kwa hiyo zile Sh2,000 zimepona (za kuwapa wazoa taka), nachukua takataka yangu naibadilisha kuwa mkaa, mazingira pia yanakua ni safi,” anasema Queen.
Mkaa mbadala ni ajira
Queen, mwenye mtoto mmoja, anatengeneza mkaa huo kwa mikono yake mwenyewe kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kuwauzia majirani ili kujipatia kipato cha kuendesha maisha kwa sababu hana mume.
“Mkaa huu kwangu ni ajira, mwanzo nilikuwa na kipato kidogo, hali fulani duni lakini baada ya kukutana na Sauti ya Jamii tukajifunza kuhusu mkaa mbadala, leo hii naweza kuuza mkaa huu Sh500 mara tatu au nne.
“Kuna vitu ninakuwa nimejikwamua kiuchumi,” anasema Queen.
Mkaa huo anaouza kwa majirani humuingiza wastani wa Sh7,000 hadi Sh8,000 kwa wiki, hivyo kumpunguzia ukali wa maisha.
Kilo moja ya mkaa huo huuza kwa Sh500 ambapo kwa mtu mwenye familia ya kawaida anaweza kuutumia kwa siku moja na hivyo kumpunguzia gharama za kununua mkaa wa kawaida.
Matumizi ya mkaa huo yamempunguzia gharama za maisha Queen kwa sababu zamani alilazimika kutumia Sh2,000 kila siku kununua mkaa wa kawaida. Hii ina maana kwa sasa Queen anaokoa Sh1,500 kila siku kununua mkaa sasa na Sh45,000 kwa mwezi.
Mkaa mbadala anaotengeneza hauna gharama yoyote kwa sababu malighafi zote isipokuwa uji wa muhogo anaokota mtaani au kukusanya kwa majirani.
Kuwapata wateja haikua rahisi kwa sababu “watu walishazoea kutumia mkaa wa kawaida ilikuwa ngumu kukubali, kwa hiyo tulishawishi, wamekua watumiaji wakubwa wanaupenda kwa sababu unabana bajeti na unakaa sana jikoni.”
Mwanafunzi asiyeacha kujifunza
Elimu ya mkaa mbadala aliipata kwa kikundi cha Sauti ya Jamii kilichopo Kipunguni ambacho kinamiliki kiwanda kidogo cha kutengeneza mkaa huo.
Licha ya binti huyo kutengeneza mkaa huo kwa mikono, baadhi ya siku husaidia kazi za kuanika mkaa katika kiwanda hicho ili kujipatia kipato cha ziada.
Binti huyo mwenye ndoto za kufanikiwa kimaisha, anasema anatamani siku moja amiliki kiwanda cha mkaa mbadala kisha aajiri wanawake ambao wanapitia katika kipindi kigumu cha maisha.
“Natamani sisi wakina mama tukaungana tukanunua mashine (ya kutengeneza mkaa mbadala) tukaanza kutengeneza ili tujiendeleze kiuchumi,” anasisitiza binti huyo.
“Mkaa mbadala ni ‘sponspor’ kwa mabinti
Queen anasema wanawake wanaweza kujiajiri kwa kuanza kutengeneza mkaa huo na kuacha utegemezi kwa wapenzi wao na ukawasaidia kuboresha maisha yao.
“Unaweza kuufanya mkaa huu kuwa ‘sponsor’ (mpenzi au mchepuko anayemudu gharama zote za maisha) wako badala ya kumsumbua mtu wako kumuomba hela kila siku. Maisha ni rahisi kwa sababu utengenezaji wa mkaa ndiyo kipato chako,” Queen anasema huku akicheka.
JikoPoint inaunga mkono watu wanaochochea matumizi ya nishati safi ya kupikia Tanzania kupitia habari. Hata hivyo, si sehemu ya biashara na miamala mtakayofanya na watu tunaowaandikia makala hizi.