Nishati ya bayogesi ilivyobadilisha maisha ya mwalimu wa shule ya msingi

Na Esau Ng'umbi
13 Aug 2022
Ni Mwalimu Efgenia Sirito, mkazi wa Tabata jijini Dar es salaam aliyefanikiwa kupunguza gharama za maisha kwa kutumia nishati hiyo ya kupikia.
article
  • Imemuondolea kabisa gharama za kununua mkaa na kuni.
  • Imeimarisha afya yake na kutunza mazingira yanayomzunguka.
  • Awataka wanawake wengine kuanza kutumia bayogesi.

Awali alikuwa anatumia gharama kubwa kununua mkaa pamoja na gesi ya majumbani (LPG), nishati aliyokuwa anatumia kutayarisha chakula cha familia yake.

Kila baada ya miezi miwili alilazimika kuwa na Sh60,000 kwa ajili ya kununua gunia la mkaa ambao licha ya kuwa na gharama kubwa ulikuwa unachafua mazingira na kuhatarisha afya yake.

Pamoja na kununua mkaa kila baada ya miezi miwili bado alilazimika kununua gesi ambayo angeitumia kwa dharura endapo mkaa ungemuishia na hivyo alipaswa kuwa na Sh50,000 nyingine kwa ajili ya kununua gesi.

Miaka miwili iliyopita Mwalimu Efgenia Sirito, mkazi wa Tabata jijini Dar es salaam aliazimia kugeukia matumizi ya nishati mbadala. Alivutiwa na nishati ya  bayogesi kutokana na unafuu wake pamoja na namna inavyotunza mazingira.

“Niliona kwanza inasaidia usafi wa mazingira  na vile vile ni nishati yenye gharama nafuu, ukishalipa wakati wa kufunga hakuna gharama nyingine yoyote ni unaendelea kutumia muda wote, imenipunguzia gharama sana,” anasema Efgenia, mwalimu wa katika moja ya shule za msingi jijini hapa.

Hivi sasa hana wasiwasi wa kuishiwa nishati ya kupikia wala kuwa hatarini kiafya  kwa sababu anatumia gesi anayozalisha mwenyewe kwa kutumia mtambo wa bayogesi unaotumia taka za mabaki ya vyakula.

Wakati akifurahia kupunguza gharama za nishati, mama huyo ameimarisha pia mazingira ya nyumbani kwake kwa sababu uchafu hauzagai tena kama awali kwa sababu unabadilishwa kuwa taka.

Kwa sasa anatumia muda mfupi kuandaa chakula kwa sababu ana nishati ya uhakika ambayo anatumia gharama ndogo sana kuipata, jambo lililosaidia kuimarisha upendo katika familia yake. 

“Mtungi wa gesi nilikuwa nanunua Sh48,000 hadi Sh50,000 na gunia la mkaa nalo ni karibu Sh60,000 gharama ilikuwa kubwa sana tofauti na sasa hivi ninavyotumia bayogesi kwa kweli imenipunguzia gharama,” anasema Efgenia.

Bayogesi ni nini?

Kwa mujibu wa tovuti ya mazingira ya EcoMaisha biogesi ni mojawapo ya gesi zinazoungua ambayo hutokana na uchafu wa kikaboni uliochachushwa (fermented)  ambao huwekwa katika mazingira yasiyo na hewa ya oksijeni na kumeng’enywa na aina fulani ya bakteria ambao hutoa gesi inayoitwa Methane.

Pamoja na mchanganyiko wa gesi nyingine Methane ndiyo gesi inayoungua ikiwashwa, hivyo hutumika kama chanzo cha nishati kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kupikia.

Moja ya jiko liliungwanishwa na mtambo wa bayogesi ambalo anatumia Mwalimu Efgenia wa Tabata jijini Dar es Salaam. Picha| Efgenia Sitiro.

Mchakato wa utengenezaji wa bayogesi

Zipo malighafi mbalimbali  zinazotoa bayogesi ila hutofautiana katika kiwango cha gesi inayotoka, EcoMaisha wanabainisha kuwa kinyesi cha wanyama kama vile ng’ombe na nguruwe hutumika zaidi na watu wengi kutengeneza nishati hiyo ya kupikia.

Mabaki ya taka za jikoni kama maganda ya ndizi, maji taka na baadhi ya mimea ikiwemo magugu maji na “algae” nayo hutumika kutengeneza nishati ya bayogesi.

Mwalimu Efgenia hutumia mabaki ya vyakula kama maganda ya matunda au masalia yanayobaki wakati wa kupika ambayo hukusanywa na kuwekwa katika mtambo unaochakata gesi nyumbani kwake.

“Tukila matunda, tukimenya nyanya  yale maganda tunayakusanya ndiyo hayo tunayaweka kwenye mtambo wa bayogesi unaotuzalishia gesi,” anasema Efgenia ambaye ni mama wa watoto watano.

Matumizi mengine ya bayogesi ni yapi?

Pamoja na matumizi ya kupikia, nishati hiyo inaweza kutumika kuzalisha umeme wa majumbani, viwandani pamoja mbolea kwa ajili ya wakulima kupandia na kuotesha mazao shambani. 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Ichi Energies Eucalyptos Malle, kampuni inayojihusisha na ubunifu wa mitambo ya biogesi, mitambo ya kufua gesi hiyo inatumiaka zaidi majumbani kupikia na kuwasha taa 

“Kuupata mtambo huu unahitaji Sh990,000, hiyo ni gharama ya mtambo pekee kuna gharama zingine ikiwemo ufungaji na usafirishaji ambazo zinahimilika,” anasema Malle. 

Mtambo huo wenye ukubwa wa mita 2.5 kwa 2.5  sawa na mita za mraba 6.25 unaweza kuzalisha gesi ya kupikia kwa saa nne kwenye jiko moja baada ya kujazwa taka za lita 15 kwa siku moja.

Wito kwa akina mama wengine

Kutokana na kuendelea kuongezeka kwa gharama ya nishati nyingine kama mkaa na kuni, mwalimu Efgenia amewataka akina mama kugeukia matumizi ya biogesi kwani licha ya malighafi zake kupatikana kwa urahisi pia ni salama.

“Hii biogesi  hata ukimuachia  mtu ambaye hajawahi kutumia gesi bado ataweza kutumia kwa sababu haina madhara ya kulipuka kama gesi nyingine,” anasema Efgenia.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa