Sauda Mahita: Msomi anayechagiza nishati safi ya kupikia Tanzania-2

Na Lucy Samson
13 Aug 2022
Sauda Mahita katika kampuni anayofanya kazi, anauza majiko banifu yanayotumia kiasi kidogo cha mkaa na hivyo kusaidia kupunguza ukataji wa miti.
article
  • Kampuni anayofanya kazi wanatengeneza majiko banifu.
  • Majiko hayo yanatumia mkaa kidogo na kupunguza ukataji wa miti.
  • Neno lake kwa wanawake, watumia nishati safi kujikwamua kimaisha.

Makala ya jana tuliangazia namna Sauda Mahita alivyoingia katika kazi ya kuuza vifaa vya kielektroniki vinavyotumia nishati safi na salama ikiwemo gesi ya majumbani na umeme.

Leo tunaangazia kwa undani jiko banifu analouza Sauda katika kampuni yake ya Smart Mnada iliyopo jijini Dar es Salaam.

Jiko hilo lililopewa jina la Eco Zoom limetengenezwa na malighafi ya chuma inayowezesha kutunza na kusambaza joto kwa haraka kwenye sufuria au chombo chochote unachopikia.

“Kwa juu limetengenezewa chuma cha pua cha mviringo ili kuwezesha mtumiaji kubandika chombo chake cha kupikia na kukaa vyema kabisa kuhimili mitikisiko inayotokea wakati wa kupika,” anasema Sauda. 

Jiko hili lina mlango mpana wenye kuwezesha hewa kuingia wakati wote linapotumiwa, pia unaweza kuchoma mahindi au viazi kupitia mlango huu na bado hewa ikaendelea kuingia.

Katikati ya jiko hili kuna nafasi ndogo ya kuweka mkaa iliyowekewa wavu kuhakikisha mkaa hauanguki  chini wakati wote wa mapishi.

Kwa mujibu wa Sauda, jiko hilo linaweza kudumu hadi miaka mitano. Pia yana mishikio inayodumu isiyopitisha moto inayoliwezesha kuhamishika kwa urahisi.

“Majiko haya sisi tunayauza Sh50,000 kwa bei ya rejareja na Sh40,000 kwa bei ya jumla,” anasema afisa masoko huyo.

Baadhi ya masufuria yanayouzwa na kampuni ya Smart Mnada ambayo Sauda Mahita anafanya kazi ambayo ni rafiki kwa majiko ya gesi na umeme kwa sababu hayaharibiki haraka. Picha | Smart Manada.

Mbali na majiko ya Eco Zoom, kampuni hiyo inajihusisha na uuzwaji wa sufuria za kisasa zilizotengenezwa kwa malighafi ya alminiamu inayowezesha sufuia hizo kudumu kwa muda mrefu na kurahisisha mapishi wakati unapikia jiko la gesi au umeme.

Faida za kutumia majiko ya Eco Zoom

Kwa kipindi cha mwaka mmoja ambacho Sauda amekuwa akifanya kazi kwenye kampuni hiyo ameweza kubadili mtazamo wake kutoka kwenye matumzi ya majiko ya kawaida yanayohitaji mkaa mwingi na kuharibika mara kwa mara.

“Jiko hili jina sehemu ndogo sana ya kuweka mkaa natumia mkaa mmoja mkubwa…kwa hiyo mkaa wa Sh1,000 naweza kuchemshia maharage na nikaweka zaidi ya mara tatu,” anasema Sauda.

 Sauda anayeishi kwenye familia ya watu sita alikuwa anatumia mkaa wa Sh1,000 kubandika maharage pekee, lakini sasa mkaa huo unatosha kupika mlo wa siku nzima wakitumia jiko hilo la kisasa.

Jinsi anavyowafikia wateja wake

Sauda pamoja na wafanyakazi wenzake waliopo kwenye kitengo cha masoko na mauzo husambaza bidhaa hii mahali popote inapohitajika pia huwahudumia wateja wanaokuja ofisini kwao kununua majiko hayo.

“Wateja wetu tunao kote kote mijini na vijijini, lakini sisi tunauza sana mjini na vijijini ndiyo kwanza tunaanza kuwafikia na wao,” anasema Sauda.

Kampuni hii iliyopo jijini Dar es Salaam,  pia inafanya matangazo kupitia mitandao ya kijamii ili kuweza kusambaza elimu ya kupunguza matumizi ya mkaa, lakini kuonyesha bidhaa walizonazo.

“Ofisi zetu zipo Kinondoni jijini Dar es Salaam, tunafanya delivery (huduma ya kufikishiwa bidhaa) bure kabisa kwa wateja waliopo hapa Dar ila mkoani tunatuma kwa gharama za mteja,” anaongeza Sauda.

“Siyo rahisi hivyo” 

Moja ya changamoto ambayo Sauda anakutana nayo ni kuelimisha wateja kuhusu umuhimu wa bidhaa hizo na utofauti uliopo na majiko ya kawaida 

“Changamoto ninazopata ni za kawaida ikiwemo kuwaelimisha wateja ambao wanakuwa hawaelewi utofauti wa bidhaa hii na majiko ya kawaida,” anasema 

“Gharama ya bidhaa pia imekuwa changamoto kwani wateja wanalinganisha muonekano wa bidhaa na bei, wengi wakaitegemea ifanane na majiko ya kawaida ya kupika nyumbani.”

Ushauri wake kwa wanawake

Sauda anatamani teknolojia hii imfikie kila mwanamke nchini ili kuweza kupunguza ukataji wa miti na uchafuzi wa mazingira.

“Ushauri wangu wanawake tutumie bidhaa hii ina faida kubwa sana kwetu kwa sababu sisi ndo wapishi, pia inatusaidia kubana matumizi,” anasema Sauda.

Unaweza kuwasiliana na Sauda Mahita kujifunza zaidi ili nawe uweze kujiajiri kupitia namba 0686860033.

JikoPoint inaunga mkono watu wanaochochea matumizi ya nishati safi ya kupikia Tanzania kupitia habari. Hata hivyo, si sehemu ya biashara na miamala mtakayofanya na watu tunaowaandikia makala hizi. 

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa