Ni nishati wanga inayotumika katika utengenezaji wa mkaa huo.
Mkaa huo ni rafiki kwa mazingira na afya za binadamu.
Haikumchukua muda kubaini uwepo wa shughuli ya uzalishaji pembezoni mwa njia aliyozoea kupita mara kwa mara wakati anaenda sokoni kufuata mahitaji ya nyumbani.
Mabango yaliyobandikwa kwenye jengo hilo ndiyo yalimhamasisha kwenda kuomba kazi katika kiwanda kidogo kilichopo Vikindu katika Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Ni Stella Mayaya, mwanamke mjasiriamali na mkazi wa Mtaa wa Magomeni uliopo Vikindu. Hivi sasa ni mfanyakazi katika kiwanda cha Gipa kinachozalisha bidhaa mbalimbali zitokanazo na mihogo.
Kazi yake kubwa ni kumenya na kuikata mihogo katika vipande vidogo.
Kazi hii inamuwezesha Stella mwenye umri wa miaka 43 kuwa na uhakika wa kupata Sh3,000 au Sh4,000 kwa siku ambayo kwake si haba kwa sababu humsaidia kukidhi mahitaji ya nyumbani.
“Inanisaidia kulingana na hali yangu, kazi kubwa ni kumenya mihogo na malipo yanategemeana na uwezo wako, kwa siku naweza kupata Sh3,000 Sh4,000,” anasema Stella.
Kiwanda muhimu kwa mkaa mbadala
Kiwanda hiki kilichoanzishwa miezi saba iliyopita kinachakata na kutengeneza bidhaa zinazotokana na zao la muhogo ambazo ni unga, nishati wanga (Tapioca Starch) pamoja na vyakula vya wanyama huku bidhaa inayouzwa zaidi ni wanga.
Gideon Kalimanzila ni Mkurugenzi wa kiwanda hicho anasema nishati wanga inauzwa zaidi kutokana kuhitajika kwa kiasi kikubwa katika shughuli mbalimbali ikiwemo utengenezaji wa mkaa mbadala.
“Hii starch ina matumizi mengi sana hasa viwandani. Viwanda vya madawa, nguo, pia viwanda vinavyotengeneza mkaa mbadala wanashauriwa kutumia starch ya muhogo ili kuzalisha mkaa bora unaouzika kimataifa pia inaweza kutumika kama chakula,” anasema Kalimanzila.
Nishati wanga kwa ajili ya kutengeneza mkaa mbadala huuzwa kwa Sh2,200 kwa kilo moja, ambapo tangu kuanzishwa kwake, kiwanda hicho kimezalisha wanga tani zisizopungua 10.
Uwepo wa kiwanda hiki umekuwa msaada mkubwa kwa wanawake wanaoishi katika maeneo yanayokizunguka kwa sababu wamepata ajira.
Bernadetha Khatibu, mama wa watoto watano, tofauti na Stella ambaye hukaanga mihogo kama kazi yake ya ziada, yeye hutegemea kiwanda hicho kama sehemu muhimu kupata kipato..
“Ninapokuja hapa unafuu kidogo upo, ninapopata hiyo Sh2000 au Sh3000 unaenda kupata unga hata nusu au kilo nakula na watoto, kuliko kukaa tu nyumbani,” anasema Bernadetha (48).
Uchakataji wa malighafi za nishati wanga ya muhogo hauanzii kiwandani hapo pekee kwani hata katika mashamba wanakonunua mihogo huwatumia wanawake.
“Kwa hapa pwani tunanunua zaidi mihogo katika mashamba yanayomilikiwa na wanawake, hata katika shughuli za uchimbaji na kupakia tunawatumia wao pia wale wanaoleta wenyewe hapa kiwandani wengi ni wanawake,” anaeleza Kalimanzila.
Hii inadhihirisha kuwa wanawake wana mchango mkubwa katika uzalishaji wa malighafi hiyo ambayo hutumika kutengeneza mkaa mbadala unaosaidia kutunza mazingira kwa kupunguza ukataji miti na athari za kiafya kwa watumiaji.
Kiwanda hicho kina wafanyakazi 15 ambapo kati yao, wanawake ni 10.
Nishati wanga inatumikaje kwenye mkaa mbadala?
Mkaa mbadala ni mkaa ambao hutengenezwa kwa muunganiko wa taka mbalimbali zilizochomwa na kusagwa na kisha kuchanganywa na kiunganishi ambacho hugeuza unga wa taka kuwa hali yabisi mfano wa ugali ambao baadae hugawanywa katika maumbo madogo madogo.
Kwa mujibu wa Kalimanzila, watengenezaji hutumia unga wa ngano, mahindi au wa muhogo kama kiunganishi lakini nishati wanga ya muhogo imeonekana kutoa mkaa bora zaidi na kiwango kikubwa.
“Mkaa mbadala uliotengenezwa na starch ni bora zaidi kuliko uliotengenezwa na unga mwingine kwa sababu huwa na chembe chembe chache za makapi yanayoweza kusababisha moshi pia starch inatumika kidogo sana hivyo inapunguza matumizi,” anasema Kalimanzila.
Inatengenezwaje?
Hatua ya kwanza ni mihogo humenywa na kuoshwa hupelekwa katika mashine ambayo hutenganisha kirutubishi cha wanga (starch) pamoja na makapi.
Nishati wanga ikiwa katika hali ya kimiminika hutenganishwa kwanza na maji kisha huanikwa ili ikauke.
Pasiansi Abeli mwanzilishi mwenza wa kiwanda cha Gipa anasema mchakato huo hufanywa na watu wapatao 20 kwa siku na kilogramu 300 za mihogo huzalisha kilogramu 100 mpaka 150 za wanga.
“Kutokana na teknolojia yetu tunatumia saa nane kukamilisha mchakato huo,” anasema Abeli.
Bado kuna kilio
Licha ya kiwanda hicho kuwa msaada kwa kutoa ajira kwa wanawake na kuhamasisha matumizi ya mkaa mbadala kwa kuzalisha kiunganishi kinachotumika katika utengenezaji wa mkaa huo bado kinakabiliwa na changamoto.
Stella Liyaya, mfanyakazi wa kiwanda hicho katika kitengo cha umenyaji wa mihogo anasema licha ya malipo kuwa siyo ya kuridhisha, miundombinu ya kiwanda hicho ni kikwazo katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Kiukweli malipo hayana maslahi, tunakuja tu kufanya kazi kwa sababu tuna njaa, malipo yanaumiza, kazi ni ngumu malipo ni hafifu, tunafanya kazi ya hatari tunajikata na visu hapa, ikiwezekana waongeze malipo,” anasema Stella.
Wakati Stella akilalamikia kuhusu malipo kwa upande wake Bernadetha Khatibu anasema zana zinazotumika katika umenyaji sio rafiki na kueleza kuwa anatamani jamii ielewe kuhusu bidhaa wananazozalisha ili zinunuliwe kwa wingi na wao wapate ajira ya kudumu.
“Natamani bidhaa zitoke mara kwa mara na sisi tupate ajira tusiwe tunakaa muda mrefu nyumbani tunazidi kuteseka kwa sababu bidhaa zinapotoka na sisi tunapata muda wa kufanya kazi na kupata pesa,” anasema Bernadetha.
Malengo ya kiwanda hicho ni kutoa elimu ya matumizi ya starch ya mihogo kwa jamii ili kuongeza uelewa ambapo itawasaidia wanaotengeneza mkaa mbadala kuongeza kasi ya uzalishaji hivyo kuinua kipato na kutunza mazingira.