Majiko banifu yanayopunguza gharama za maisha

Na Mariam John
15 Jul 2022
Majiko hayo yanayotumia gesi ya majumbani (LPG) yanapunguza gharama za kununua kuni na mkaa, hivyo kutunza mazingira.
article
  • Anatengeneza majiko yanayotumia mkaa kidogo na gesi ya majumbani.
  • Yanasaidia wanawake kuokoa gharama za kununua kuni na mkaa. 
  • Anapenda kuona jamii inahamia katika matumizi ya nishati safi na salama ya kupika.

Wakati Serikali ikihamaisha jamii kupanda miti na kutunza mazingira ili kurudisha ikolojia ya nchi, Zainabu Barabara (51) ni miongoni mwa watu walio mstari wa mbele kutekeleza sera hiyo ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Zainabu ni mama watoto wanne aliacha shughuli ya kuuza mkaa miaka 13 iliyopita na kujiajiri katika kazi ya utengenezaji majiko banifu yanayotumia gesi.

“Mfano unaweza kuagiza gunia 10 za mkaa unapoanza kuuza unakuta chini kuna chenga chenga hivyo gunia lenye debe nane utakuta mkaa wa debe sita huku zilizobaki ni chenga hivyo kwenye kila gunia unakuta unapata hasara, hivyo nikaamua kuacha,” anasema Zainabu.

Katika karakana ndogo ya Pangoni maarufu kwa jina la Makarai iliyo chini ya usimamizi wa Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) Mkoa wa Mwanza, hapo ndipo Zanaibu anapofanyia shughuli zake za kutengeneza majiko hayo kwa kutumia mapipa yaliyotumika. 

Zainabu mkazi wa Ibada jijini hapa anasema alianza kazi hiyo mwaka 2010 ambapo hununua mapipa yaliyotumika kisha kuunda majiko ya mkaa na gesi, masunduku ya shule, vikaango vya mandazi na vitumbua.

Kwa upande wa majiko ya mkaa, Zainabu anasema anaunda kuanzia jiko dogo la kilo moja hadi kubwa la kilo 25 ambayo yanatumia mkaa kidogo ikilinganishwa na majiko ya kawaida. 

Hata hivyo, ubunifu wake unajikita zaidi katika majiko yanayotumia gesi ya majumbani (LPG) ili kuwawezesha watu kutumia nishati safi na salama inayotunza mazingira na afya ya binadamu.

Pia hutengeneza masufuria mazito yanayotumika kupikia katika majiko ya gesi ya majumbani kuanzia la kilo 5 hadi 32. Majiko hayo yameundwa kutumia gesi kidogo na hivyo kumpunguzia gharama mtumiaji. 

Zainabu akiwa katika oveni ambayo inatumia gesi ya majumbani (LPG). Gesi hiyo inaweza kutumika kubanika nyama. Picha| Mariam John.

Mchakato wa utengenezaji majiko hayo

Zaina aliyeajiri vijana katika kiwanda cheke, hutengeneza majiko hayo kila apatapo oda kutoka kwa wateja wake wakiwemo wanawake wanayoyatumia kupikia nyumbani na migahawani.

Anasema hununua vifaa vyote vinavyohitajika kwenye jiko hilo la gesi ikiwemo kifaa cha kuwashia moto (banner) kuanzia size ya jiko dogo hadi jiko kubwa au la sahani mbili.

“Tunatengeneza majiko ya gesi kwa oda, mtu akija tunamtengenezea kulingana na size anayotaka lakini pia tunatengeneza ovena za kienyeji ambazo zinaweza kuchoma kuku kuanzia watano, mbuzi mmoja hadi nusu ng’ombe,” anasema Zainabu.

Kwa sababu kazi hiyo anaona kama wito, hulazimika kutumia nguvu nyingi yeye na wafanya kazi wenzake kwa sababu huusisha kukata, kuponda na kuunganisha mapipa katika saizi tofauti tofauti.

Anasema njia zinazotumika ni za kienyeji hakuna mashine inayotumika kuponda na kulainisha mapipa hayo tofauti na kutumia nguvu ambapo wanawake wengi hawawezi hivyo inawalazimu kuajiri vijana kwa ajili ya kufanya shughuli hiyo.

Majiko hayo ya gesi yanauzwa kuanzia Sh130,000 hadi Sh550,000 na kuwa itategemea na saizi ya jiko ambalo mteja anahitaji.

Hata hivyo, majiko hayo huuzwa kwa msimu kutokana na kudumu kwa muda mrefu baada ya mtu kununua, licha ya kuwa kwa siku una uwezo kupata Sh50,000.

Kibarua alichonacho

Pamoja na mafanikio ya kutengeneza majiko hayo, Zainabu anakumbana na changamoto ya mtaji ili aweze kununua mlighafi kwa ajili ya kutengeneza majiko mengi ya gesi yatakayosambazwa vijini na mjini.

“Changamoto ni ukosefu wa mitaji ambapo hivi sasa tumepata taarifa fedha za halmashauri zinatolewa, hivyo tungepata mitaji ya kutosha tungeweza kutengeneza majiko mengi ya nishati mbadala,” anasema Zainabu. 

Zainabu anatamani kupata mkopo wa Sh15 milioni ili aweze kuongeza mtaji wake ambapo ataagiza mapipa mengi ambayo yatatumika kutengenezea majiko na vifaa vingine vinavyotumia gesi ya majumbani.

Pia ana ndoto ya kuanza kutengeneza masufuria ambayo yanaweza kutumika kwenye jiko la umeme lakini pia bidhaa zingine ambazo zitasaidia katika kulinda na kutunza mazingira.

Zainabu siyo tu anatengeneza majiko banifu bali vifaa vingine vya nyumbani ikiwemo vikaango, vinavyomsaidia kujipatia kipato cha kuendesha maisha. Picha| Mariam John.

Nini anajivunia kwenye kazi yake

“Ni kazi ambayo najivunia ukiacha suala la kuhudumia familia pia nimeweza kusomesha watoto wangu ambapo mmoja anamalizia Chuo cha udaktari Muhimbili na mwingine yuko mwaka wa pili stashahada (diploma) ya madini,” anasema Zainabu.

Mbali na watoto kusoma pia kwa kushirikiana na mumewe ameweza kujenga nyumba yenye vyumba vinne ambayo anaishi na familia yake kutokana na biashara hiyo.

Anashaurije wananchi kutumia nishati mbadala

Zainabu anasema yapo madhara makubwa kwa matumizi ya mkaa na kuni ambapo licha ya vifo vinavyoweza kutokea lakini pia yanaweza kusababisha magonjwa ya ngozi na mfumo wa hewa.

Anasema pamoja na shughuli hiyo kutengeneza majiko yanayotumia gesi pia anashauri wananchi kuendelea kutumia gesi kwa kuwasasa upatikanaji wake ni mkubwa tofauti na miaka ya nyuma.

“Wananchi wahamasishwe kuendelea kutumia gesi, hii itasaidia kupunguza matumizi makubwa ya kuni na mkaa,” anasema.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa