Mara nyingi nikiwa na njaa kali, chakula cha haraka nitakachofikiria kupika ni ugali, huku upande wa mboga inayonijia haraka ni bamia kwani haihitaji mambo mengi kama mboga nyingine..
Siku moja katika harakati zangu za kutuliza njaa, wazo likanijia akilini, niongeze karanga kwenye bamia.
Kiukweli sikuwahi onja bamia za namna hiyo, lakini nikajaribu.
Pishi nililolitoa hapo lilikuwa ni tamu balaa hadi nikajiuliza kwanini sikuwaza tangu siku nyingi kufanya hivyo.
Utamu wa pishi hilo limenibamba hadi leo, na nimeona nikushirikishe na wewe ukajaribu na ujionee.
Pishi hili lina mahitaji machache ambayo yatakugharimu Sh1,000, kwani unachohitaji ni bamia za mia 3, nyanya 3, unga wa karanga wa mia 3 na kitunguu cha mia, basi mchezo unakuwa umeisha.
Mahitaji hayo yanaweza kuongezeka kutokana na idadi ya walaji.
Maandalizi
Osha bamia na uzikate sehemu ngumu ya chini, kisha uzikate nusu kwa urefu. Kama haupendelei kukata basi unaweza kuziacha nzima.
Baada ya hapo katakakata kitunguu na usage nyanya ili ziive kwa urahisi.
Upishi
Weka mafuta kiasi kwenye sufuria na uyaache yachemke kidogo kisha weka vitunguu. Baada ya sekunde 30 weka bamia na uache zichemke kwa sekunde 45 kisha weka nyanya na chumvi.
Nyanya zikikaribia kuiva, weka unga wa karanga vijiko vitatu vya chakula au kama una siagi ya karanga unaweka kutumia pia.
Ongeza maji kidogo na uchanganye vizuri pishi lako, kisha acha lichemke kwa dakika 3,
Onja kama mchuzi umeiva vizuri, kama bado acha lichemke hadi pale litakapoiva vizuri.
Hadi hapo mboga yako iko tayari, andaa ugali wako na uenjoy!
Kama haupendelei ugali, basi unaweza sindikizia mboga hii na wali.