Jinsi unavyoweza kupika maini rosti

Na Lucy Samson
29 Sept 2022
Leo nakusogezea mapishi rahisi ya rosti ya maini ya ng’ombe unayoweza kula na wali, ugali, ndizi au hata chapati.
article
  • Mboga hii inafaa kuliwa na wali, ugali, chapati au ndizi.
  • Inafaa kuliwa wakati wowote iwe mchana au jioni.

Iwe wakati wa mchana au jioni suala la kuchagua mboga halijawahi kumuacha mtu salama, lazima uumize kichwa kujua mboga itakayosukuma mlo wako wa siku husika.

Kama kawaida leo nimekusogezea mapishi rahisi ya rosti ya maini ya ng’ombe unayoweza kula na wali, ugali, ndizi au hata chapati.

Basi tusogee jikoni tupike hii mboga yenye ladha ya kipekee, na kwa hakika mpaka umalize kuipika utakuwa umeshapata chakula ambacho kitaisindikiza mboga hii kwenye meza yako ya msosi.

Maandalizi

Osha maini na uyakate kate vipande kiasi, kicha uchuje maji na uyaweke kwenye chombo kisafi.

Ukimaliza andaa nyanya, karoti, hoho kitunguu kwa kuosha na kukata kata saizi uipendayo, kisha twanga tangawizi na kitunguu saumu mpaka vitakapolainika.

Andaa sufuria ya kupikia, ibandike jikoni na uanze kwa kuweka mafuta na vitunguu ulivyokwisha kukata kata kisha ukoroge mpaka vikiwa rangi ya kahawia.

Baada ya hapo ongeza kitunguu swaumu na tangawizi na ukoroge kwa dakika moja uache viive kisha ongeza maini na uache yaive.

Kila baada ya dakika 3 uwe unageuza maini yako ili yasiungue hadi maji yakauke na kuonyesha dalili za kuiva.

Ongeza nyanya ulizokata kata kwenye sufuria unayopikia maini yako na ufunike kwa dakika 5 ili nyanya ziive.

Nyanya zikishaiva koroga vizuri na uongeze vijiko viwili vya nyanya ya kusaga kisha hoho na karoti na kiasi kidogo cha maji kisha uache jikoni kwa dakika tatu.

Baada ya dakika tatu ongeza chumvi na ndimu kipande kimoja, ukihakikisha rosti yako imekuwa nzito vya kutosha unaweza kuepua na pishi lako litakuwa tayari.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa