Kuandaa vitafunwa ni miongoni mwa shughuli inaayowashinda watu wengi hususani wakati wa asubuhi wakati wa kupata kifungua kinywa.
Shughuli hiyo, huwafanya baadhi yao kuishia kununua ili kuokoa muda na kuwahi katika majukumu mengine ya asubuhi.
Hata hivyo, bado kuna idadi kubwa ya watu wanaoandaa vitafunwa nyumbani jambo linalowasaidia kula kitafunwa wanachokitaka au chenye viungo wanavyopelea.
Ikiwa suala la kuandaa vitafunwa bado linakusumbua basi makala hii ni kwa ajili yako ambapo tutajifunza jinsi ya kuandaa bagia za kuku na viazi zitakazonogesha mlo wako wa asubuhi.
Hatua za kufuata ili kuandaa bagia za kuku na viazi mbatata
Nunua unga wa dengu ambao ndiyo hitaji la msingi kwenye pishi hili, anza kwa kuchekecha unga kwa kutumia chujio ili kuondoa vijidudu au uchafu mwingine unaoweza kuonekana kisha uendelee na hatua nyingine za mapishi.
Baada ya hapo andaa kuku kwa kumkata kata minofu midogo midogo, unaweza kutumia blenda lakini hakikisha nyama haisagiki sana, saga kidogo tu kisha iweke pembeni.
Hatua inayofuata andaa kitunguu, karoti, hoho, kisha ukatekate kwa saizi ndogo ndogo.
katika bakuli kubwa utakalolitumia kutengeneza mchanganyiko wa unga wa dengu, chumvi kiasi, pilipili mtama, tangawizi ya unga, hoho, karoti na kama unapenda pilipili unaweza ukaikata kata na ukaiweka
Changanya vizuri mchanganyiko ili viungo vichanganyike sawasawa kisha ongeza maji kidogo kidogo huku ukikoroga ili upate mchanganyiko mzito mzito usiokuwa na madonge.
Hatua nyingine ni kuongeza vipande vya kuku, viazi vilivyochemshwa, na vitunguu vilivyokatwa kisha changanya vizuri ili kila kipande kifunikwe na mchanganyiko wa dengu.
Mchanganyiko ukiwa mzito na viungo vyote vimechanganyika andaa sufuria au kikaango kwa ajili ya kuchoma bagia.
Weka mafuta kwenye sufuria na yaache yapate moto wa wastani kwa dakika mbili, chukua kijiko kimoja cha mchanganyiko wa bagia na mimina polepole kwenye mafuta moto.
Baada ya hapo kaanga bagia kwa dakika tano hadi saba huku ukihakikisha zinaiva na kuwa na rangi ya kahawia kwa nje.
Toa bagia kutoka kwenye mafuta na ziweke kwenye karatasi ya jikoni ili zichuje mafuta ya ziada na zitakuwa tayari kuliwa.
Bagia za kuku na viazi zinapendeza zaidi zikiwa za moto, na hapo unaweza kula na kachumbari, ‘chutney’ ya pilipili au hata mchuzi wa nyanya.
Unaweza pia kuzitumia kama sehemu ya mlo mkuu pamoja na chai au juisi ya matunda.