Jinsi ya kupika dagaa wa “mchanga” kwa haraka

Na Mwandishi Wetu
9 Feb 2022
Kupika dagaa unahitaji dagaa wenyewe, nyanya, vitunguu, swaumu, karoti, hoho na mafuta ya kupikia.
article
  • Unahitaji dakika 10 tu jikoni.
  • Mboga hii inasindikiza wala na ugali.
  • Mahitaji ni machache na bei yake ni nafuu.

Pata picha umeenda ugenini ukakuta ugali na rosti matata ya dagaa ambayo ina limao kwa mbali. Aisee, hisia yake siyo ya kitoto.

Achana na mawazo ya kuwa unaweza kupata msosi huo ugenini pekee. Unaweza kuandaa ugali na rosti ya dagaa ukiwa nyumbani kwako tena kwenye jiko lako la mtungi wa gesi. 

Ugali ni somo la siku nyingine. Kwa leo, sogea karibu na jiko nikupe madini ya kupika dagaa na ni uhakika kuwa hautaacha kupika pishi hili hata kama una mboga nyingine.

Kwa leo, dagaa tunazopika ni zile ambazo wengi tunapenda kuziita ‘dagaa mchanga’ au dagaa wa Mwanza. 

Katika mapishi ya mboga yetu hii tunahitaji viungo vichache tu kwa sababu leo tunapika robo kilo tu ili uonje na siku nyingine upike nyingi kwa ajili yako na masela.

Haya ndiyo mahitaji yetu muhimu;

Tuandae dagaa wetu

Sasa tuandae pishi letu ili tuingie jikoni kupika chap kwa muda wa dakika 10 baada ya hapo, tunakula sotojo letu.

Anza kwa kukata kata vichwa vya dagaa, wengine huwa mnaunga dagaa bila kukata vichwa ni sawa pia ila mimi napendelea kukata vichwa kwa sababu inasaidia kupunguza mchanga.

Baada ya hapo, bandika maji kidogo jikoni kwa ajili ya kuoshea dagaa, wakati maji yakiwa jikoni, saga nyanya zako vizuri, andaa hoho, kitunguu maji na karoti kwa kuzikata kata kwa mtindo mzuri kisha menya vitunguu swaumu punje tatu na uvitwange.

Unaweza kuongeza tangawizi kama utahitaji.

Sasa weka maji ya moto pembeni uliyoweka ukisubiri yawe ya uvuguvugu. Baada ya hapo osha dagaa zako kwa maji hayo vizuri na uzisuuze na maji ya baridi lengo ni dagaa ziwe safi lakini pia zisivunjike vunjike.

Hata wewe unaweza kupika msosi unaovutia kama huu. Picha| Jiko na Jane

Twende kikaangoni

Hapa tunaanza na kuinjika sufuria yenye mafuta ya kupikia jikoni weka kitunguu maji na  ukikaange mpaka kiwe cha kahawia kisha weka dagaa zako ulizoziandaa na uzikaange kwa muda wa dakika moja.

Baada ya hapo weka kitunguu swaumu kisha ukoroge kukichanganya kwenye dagaa zako. 

Weka nyanya ulizosaga kwenye dagaa na uziache mpaka ziive kabisa. 

Weka karoti ulizozikatakata kisha koroga kuzichanganya na mchanganyiko wako wa mwanzo. 

Baada ya hapo weka maji robo ya kikombe cha chai na kisha weka pilipili ili upate harufu nzuri kwenye mboga yako.

Kabla haujafunika mboga yako, kamulia kipande cha limao kisha uweke chumvi kiasi na ufunike mboga yako kwa muda wa dakika nne hadi tano ili viungo viive vizuri.

Ukitoa mfuniko tu kwenye sufuria harufu nzuri itatawala jiko lako lote na hata majirani itawafikia, hapo dagaa zako ziko tayari. 

Zima jiko, weka hoho ulizozikata na kisha changanya, funika  mboga yako. Mboga hii inaweza kusindikiza ugali na hata wali. Enjoy!. 

Je, kuna kitu kingine unatamai kujifunza kukipika kwa mbinu nyingine mpya? Tufahamishe tukuhudumie na tujifunze kwa pamoja. Namba ni moja tu! +255 677 088 088.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa