Jinsi ya kupika makange ya kuku

Na Maria Acley
26 Jan 2022
Nikutoe hofu hiyo. Makange ni kati ya mboga rahisi kupika na utashangaa kujua kuwa huenda ulikuwa unajichelewesha kuandaa mboga hiyo nyumbani kwako.
article

  • Hauhitaji viungo vingi kama ulivyokuwa ukidhani.
  • Kikubwa ni umakini wako jikoni na utayari wa kujifunza.
  • Chakula hiki unaweza kukifurahia na ugali au wali.

Huenda umetamani kupika mboga ya makange kwa muda mrefu lakini ukadhani kwa namna ulivyowahi kuiona kwenye sahani, siyo mboga rahisi kupika.

Nikutoe hofu hiyo. Makange ni kati ya mboga rahisi kupika na utashangaa kujua kuwa huenda ulikuwa unajichelewesha kuandaa mboga hiyo nyumbani kwako.

Na ninaposema makange, najumuisha ya kuku, ya samaki pamoja na ya nyama au yoyote unayoyajua wewe.

Kama ilivyowazi kuwa Jiko Point ni sangoma wako kwenye suala zima la mapishi basi leo nataka nikutibie homa ya makange wewe mgangwa wangu.

Tiba yetu ya mapishi ya makange itaanza na makange ya kuku. Kwa siku zijazo tutaendele kujifunza hayo mengine.

Katika kuandaa makange ya kuku tunahitaji viungo muhimu ili tupate sotojo la kwenda ni pamoja na nyanya na mazaga mengine kama unavyoyaona kwenye picha hiyo chini.

Tufanye maandalizi

Tutaanza pishi letu kwa kuandaa kitunguu maji, karoti na hoho kwa kuvikata kata vizuri kwa maumbo unayoyapenda wewe ila kwa karoti na hoho zikate kwa maumbo ya urefu kama ilivyo desturi ya makange.

Baada ya hapo andaa kitunguu swaumu na tangawizi kwa kuvimenya kisha kuvisaga vizuri, unaweza kutwanga kitunguu swaumu pembeni na baadae ukasaga tangawizi au kuvisaga kwa pamoja.

Osha njegere zako nusu kikombe cha chai vizuri na uzichemshe wa muda wa dakika 10 tu, kisha usage nyanya tatu kama idadi ya kwenye mahitaji inavyotutaka. Mwandae kuku wako (robo) anaweza kuwa wa kuchoma au hata aliyekaushwa kwenye mafuta.

Tupike sotojo letu.

Baada ya kuvuka hatua ambayo wengi inatuchukua muda mwingi basi tuingie jikoni kujifunza namna ambayo tutachanganya viuongo vyetu na makange yatokee.

Kwa kuanza weka sufuria yenye mafuta jikoni kisha uweke vitunguu na uvikaange mpaka viwe vya kahawia. Weka kuku wako uliomkausha kwa mafuta au kumbanika.

Weka karoti, njegere  na hoho ulizoziandaa mwanzoni kisha koroga kuchanganya viungo vyako. Weka nyanya ulizosaga  kisha ongeza kijiko kimoja cha chakula cha nyanya ya pakti.

Baada ya hapo, koroga kuvichanganya na kisha uweke kitunguu swaumu na tangawizi ili kukata shombo ya nyanya ya kopo/pakti. Kisha weka nusu kijiko cha masala na chumvi kiasi na ufunike kuruhusu nyanya iive vizuri.

Unashauriwa kukata viungo vyako kwa saizi kubwa kubwa ili vionekane baada ya pishi kuiva. Picha| Video Hive.

Baada ya muda wa dakika moja funua mboga yako kuitazama kisha weka maji robo kikombe na ufunike kwa muda wa dakika tatu mpaka nne.

Ukianza kunusa harufu nzuri kama ile ya kwenye mgahawa wa nyota tano, jipige kifua na ujiambie mimi ni mpishi maridadi kwani makange yako yapo tayari.

Unaweza kufurahia mboga hii na wali au hata ugali.

Unataka kujifunza nini tena? Sema na sangoma wako akupe tiba ya unachotamani kukipika. Usisite kutupigia kupitia namba +255 677 088 088 au katika kurasa za mitandao ya kijamii, @jikopoint

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa