Jinsi ya kupika ‘rosti’ la  Kabeji

Na Herimina Mkude
20 Jan 2022
Kabeji ni mboga yenye virutubisho vizuri kwa ajili ya afya ya binadamu ikiwemo vitamini.
article
  • Rosti hili litakufanya uache kuiponda mboga ya kabeji.
  • Unaweza kuishusa kwa ugali na hata wali.

Dar es Salaam. Ukiwa nyumbani, halafu mama akasema “leo mboga ni kabeji” bila shaka huwa unatamani hata uhamie kwa majirani siku hiyo.

Kwa wale ambao wamesoma ‘boarding schools’ ndo kabisa usiwakaribishe mboga hiyo kwani inaambatana na historia ya maisha yaoo ya shule.

Lakini nikwambie tu, mboga hiyo ni tamu mnoo! Inategemea tu na jinsi utakavyoipika. Leo hii nataka ujue maujanja ya kupika mboga hiyo ili siku nyingine usiwe miongoni mwa wanaosambaza “memes” za kuisimanga mboga hiyo hasa kwa mwezi Januari.

Ukikata kabeji yako, nusu pika, nyingine hifadhi kwa ajili ya siku nyingine. Picha| Spoken Swahili.

Sasa twende jikoni.

Hatua ya kwanza,  ni kumenya punje tano za kitunguu swaumu. Endapo unatumia vile vitunguu swaumu vikubwa, punje moja inatosha. Unaweza kuongeza tangawizi kipande kidogo na kisha kuvitwanga kwa pamoja.

Osha nyama kisha uikatekate vipande vidogo vidogo na uibandike jikoni. Weka chumvi pamoja na mchanganyiko wa kitunguu swaumu na tangawizi kwenye nyama hiyo.

Wakati ukisubiri nyama iive, Andaa kabeji kwa kubandua sehemu za juu ambazo ni chafu na uioshe. Baada ya hapo, kata kipande nusu. Nusu iliyobaki, hifadhi kwa ajili ya siku nyingine.

Kwa wasioweza kukata kabeji, sikuhizi sokoni zipo kabeji zinazouzwa zikiwa zimeshakatwa tayari hizo unashairiwa kuziosha kama hauna uhakika wa uandaaji wake. 

Usioshe kabeji baada ya kukatakata, kwani utaondoa virutubisho muhimu.

Baada ya hapo, kata kata karoti kwa urefu katika vipande vyembamba na utafanya vivyo hivyo kwa hoho.

Kwa upande wa kile kinachotutoaga machozi jikoni, nazungumzia kitunguu maji, utakikata kwa style unayopenda, ila binafsi napendelea kukikata katika vipande vidogo vidogo vya nusu mduara.

Usisahau kuandaa nyanya kwa kuzikatakata lakini kwa ajili ya pishi hili itapendeza zaidi ukizisaga.

Hadi hapo utakuwa umemaliza kuandaa mahitaji yako.

Pishi lianze

Weka chombo cha kupikia jikoni kisha uweke mafuta ya kupikia kiasi. Walau vijiko vitatu vya chakula vya mafuta ya kupikia.

Binafsi napendelea kutumia sufuria ile ile niliyochemshia nyama. Ninachofanya ni kupunguza supu kidogo, kisha naachaa kiasi ili ikaukie na nyama, baada ya hapo naweka mafuta ya kupikia ili nianze kukaanga nyama.

Niseme tu ukweli hapa ndipo huwa nadokoa nyama haswaa! Maana harufu ya kutamanisha inayotoka hapo inakuwa ngumu kujizuia. Lakini wewe vumilia.

Acha nyama ijikaange kwa dakika 3, kisha weka kitunguu maji. Baada ya sekunde kadhaa ongeza hoho na karoti na ukamulie limao katika mchanganyiko huo.

Usitumie limao zima kwani nyanya ya pakti ina uchachu hivyo utaharibu mboga yako. Subiri kwa sekunde 30, kisha weka robo ya nyanya ya pakti, ikishajikaanga na mchanganyiko ongeza nyanya za kawaida na chumvi kiasi upendacho kisha funika ili mchanganyiko wako uive mapema.

Nyanya za pakti zinasaidia kuongeza uzito wa mchuzi wako na “kuipa rangi” rosti yako.

Nyanya zitakapokaribia kuiva, weka kabeji na uichanganye vizuri na mchanganyiko kisha ongeza pilipili na uache pishi lako lichemke kwa dakika 5 hadi 7.

Onja chakula na kama kabeji haijaiva, weka maji kidogo ili iive haraka. Usiongeze maji mengi kwani itafanya kabeji yako iive sana na kuharibu virutubisho.

Hadi hapo, mboga yako itakuwa tayari. Kama unataka kula  na  iko tayari na ugali utanogesha zaidi mlo wako.

Nikukumbushe kuwa, ulaji wa mboga hii una faida lukuki kiafya, ikiwemo kukupatia vitamin C na K.

Kabeji huongeza kinga mwili na kusaidia katika umeng’enyaji, hasa kwa aina ya kabeji kama ‘Kimchi’ ambazo ni maarufu sana nchini Korea.

Kwa wale wapenda’ diet’ basi Kabeji ni ngumu kuiepuka kwani mboga hiyo hutumika kutengenezea’ salad’ ambazo ni muhimu katika hatua hiyo.

Enjoy’! na usisahau kuwakaribisha wale ambao huiponda kabeji.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa