Jinsi ya kupika rosti ya mihogo na nyama

Na Lucy Samson
25 Jul 2022
Pishi hili huwa napenda kulipika hasa katika msimu huu wa mihogo, mihogo ya Sh2,000 inatosha kukamilisha mlo wa usiku wa familia yangu yenye watu sita.
article
  • Pishi hili linafaa sana msimu huu wa mihogo.
  • Mahitaji yake ni mihogo, nyama na nyanya.
  • Linafaa kwa mlo wa familia.

Siku moja katika pitapita zangu maeneo ya Makumbusho jijini Dar es Salaam nilikutana na kundi kubwa la kina mama wakisukumana kila mmoja kashika kiroba na wengine vikapu.

Wanawake hawa wenzangu walikuwa wakigombania mihogo mibichi  iliyokuwa ikuzwa maeneo hayo. 

Kama wewe ni mbongo mwenzangu hapana shaka unafahamu kuwa mihogo ni miongoni mwa vyakula vinavyopendwa sana na Watanzania. 

Huku nikitabasamu nikakumbuka kuwa mihogo wanayogombania naweza kutoa pishi la rosti ya mihogo  na nyama. 

Pishi hili huwa napenda kulipika hasa katika msimu huu wa mihogo, mihogo ya Sh2,000 inatosha kukamilisha mlo wa usiku wa familia yangu yenye watu sita kukamilika.

Siku ya leo ningependa tupike wote pishi hili. Hivyo tusogee jikoni.

Maandalizi

Osha nyama na ukate vipande vidogo vidogo, saga tangawizi, kitunguu sawaumu, kamulia limao, weka maji kiasi  kisha  washa jiko na ubandike mpaka iive.

Wakati unasubiri nyama yako,  menya mihogo na uchemshe kwa dakika 10 usiiache iive sana.

Menya  nyanya na uzisage, menya kitunguu karoti na hoho huku ukiandaa kiungo cha mchuzi  kama Mchuzi mix, mdalasini au ladha yoyote unayopendelea ambayo utaitumia kuunga rosti lako.

Kwenye sufuria nyingine weka mafuta kiasi kaanga vitunguu, vikiwa rangi ya kahawia weka hoho, karoti na nyama uliyoichemsha kisha koroga vizuri na uongeze mihogo na nyanya ulizosaga na uache zichemke.

Rosti yako ikichemka ongeza mdalasini, chumvi, nazi na maji kiasi kisha uache ichemke mpaka mihogo iive.

Mihogo ikiiva, ongeza mchuzi mix na mdalasini na pilipili kama unapendelea.

Baada ya kuacha ichemke kwa dakika tano, rosti yako ya mihogo nyama iko tayari kuliwa na uwapendao.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa