Una mgeni na hujui umpikie chakula gani cha haraka? Karibu tujifunze.
Kuna vyakula vingi vya kupika chap chap mfano ugali na mboga ya mayai au chipsi lakini leo, nakutambulisha kwa chakula kingine.
Ni wali wa manjano ambao wala hauhitaji mambo mengi na uzuri ni kuwa, hautotumia muda mwingi jikoni.
Faida nyingine ya wali huu ni kuwa mgeni wako ataufurahia na huenda ikawa ni sababu ya yeye kugonga hodi mlangoni kwako mara kwa mara.
Wali wa manjano unahitaji viungo vichache tu na unaweza kuupika kwa muda mfupi.
Ua ndege wawili kwa jiwe moja
Msosi ninaokufunza leo ni kati ya vyakula vinavyoweza kukupa wewe fursa ya kuua ndege wawili kwa jiwe moja, nikisema hivyo ninamaanisha ukipika wali huu suala la mboga wewe husumbuki nalo kabisa.
Chakula hiki kinaweza kuliwa na kachumbari tuna wakati mwingine kama ukipenda waweza andaa na juice unayoipenda ukasindikizia mlo wako.
Pia, endapo utapenda, unaweza kupika mboga nyingine pembeni.
Tuingie jikoni
Kwa kuanza, andaa na kuosha mchele vizuri kisha pima unga wa manjano vijiko vitatu vya kulia chakula. Tengeneza na kutwanga kitunguu swaumu, kata kata kitunguu maji na kama unapenda, ongezea viazi mviringo vilivyo katwa katwa (robo) ili viive haraka.
Bada ya hapo, osha na andaa karoti na hoho kwa kuzikata kwa maumbo unayopenda na yanayopendeza kwenye chakula. Andaa tui la nazi zito kikombe kikubwa kimoja au zaidi.
Tukarangize
Injika sufuria kisha weka mafuta ya kupikia. Yakipata moto weka kitunguu maji na kikaange mpaka kiwe rangi ya kahawia. Ongeza kitunguu swaumu na viazi mviringo kisha endelea kukaanga kwa dakika moja na uweke vile vijiko viwili vya unga wa manjano.
Baada ya hapo, weka mchele wako kisha uanze kukaanga vitu vyote kwa pamoja kwa dakika kadhaa (angalau dakika 3 ).
Weka tui la nazi uliloandaa na kisha uongeze maji ya moto kiasi cha kutosha kuivisha wali au endapo umeandaa nazi fresh ya nyumbani ni vyema ukaweka tui zito la mwanzo na tui la pili kiasi cha kutosha kuivisha pasipokutumia maji.
Unasahauje chumvi sasa? Weka chumvi kiasi na kisha funikia chakula chako kwa dakika tano au hadi maji yakauke..
Funua chakula chako kwa ajili ya kutazama maendeleo yake kama maji yamekwisha kauka weka karoti na hoho ulizoziandaa kisha funika tena chakula chako na upike kwa moto wa wastani.
Ukianza kusikia harufu nzuri ujue mambo yameshaanza kujipa. Angalia pishi lako na kama wali umelainika, hauna kiini na umeiva poa, geuza wali wako sogeza kachumbari yako karibu, pakua msosi wako na wa mgeni nendeni “mkaenjoy”.
Unataka kujua kupika nini tena? Tuulize kupitia +255 677 088 088