Jinsi ya kupika wali wa manjano 

Na Lucy Samson
30 Jul 2022
Utakachokihitaji ni mchele, manjano vijiko viwili, kitunguu swaumu, kitunguu maji na chumvi. Pishi hili unaweza kula kwa mboga yoyote iwe nyama, kachumbari au mboga za majani.
article
  • Mbali na rangi yake wali huu una faida nyingi mwilini.
  • Unachohitaji ni mchele, manjano na kitunguu swaumu.
  • Mahitaji mengine ni kitunguu maji, chumvi na mafuta.

Manjano ni kiungo cha asili ambacho kinatumika kwenye mapishi ya aina mbalimbali na urembo wa ngozi na nywele.

Uwepo wa kiambata cha calcium hukipa kiungo hicho rangi ya njano ambayo huenda ndiyo chanzo cha jina la kiungo hicho kufanana na rangi yake.

Mbali na faida kwenye nywele na ngozi jarida la habari za kitabibu la Medical News today, linasema kiungo hicho kina viambata vya  kuzuia uvimbe, kuzuia magonjwa ya moyo na kansa pamoja na kuongeza kinga ya mwili.

Basi nikukaribishe jikoni, nikupe usukani wa kupika  pishi hili ambalo mbali na kukupatia shibe na ladha ya kipekee, litaboresha afya yako na kukusaidia kupambana na magonjwa.

Utakachokihitaji ni mchele, manjano vijiko viwili, kitunguu swaumu, kitunguu maji na chumvi. Pishi hili unaweza kula kwa mboga yoyote iwe nyama, kachumbari au mboga za majani.

Maandalizi

Chambua mchele, uoshe na uuchuje maji, kisha menya kitunguu swaumu na utwange mpaka kilainike. Osha na ukatekate kitunguu maji kwa saizi ya urefu.

Washa jiko na uchemshe maji kwa ajili ya kupikia wali, yakichemka yaipue na uyahifadhi. Katika sufuria nyingine weka mafuta kiasi kaanga kitunguu swaumu pamoja na kitunguu maji mpaka viwe na rangi ya kahawia.

Ongeza manjano, koroga ili yachanganyike vizuri kisha ingeza chumvi, mchele na maji uliyoyachemsha kiasi cha kuweza kuivisha wali wako.

Funika na usubiri wali uive, hapa unaweza kuongeza iriki au mdalasini kama unapendelea.

Wali ukiiva, rangi itabadilika na kuwa ya njano na hapo wali wa manjano utakuwa kwa tayari kwa kuliwa. 

Wali huu unaweza kuliwa na mboga yoyote, ikiwemo nyama , samaki na mboga za majani.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa