Waliosema ‘mchele mmoja mapishi mengi’ hawakukosea, siku hizi kuna aina mbalimbali za mapishi yanayoweza kubadili ratiba yako ya mlo uliyoizoea kila siku.
Wengi wetu tumezoea kula zabibu kama miongoni mwa matunda yenye ladha tamu na virutubisho mbalimbali, lakini umeshawahi kula wali wa zabibu?.
Wali huu ni mtamu na unaweza kutumika pia kama mbadala kwa watu wasiopenda pilau la zabibu lenye viungo vingi.
Si hayo tu, zabibu inayotumika kwenye chakula hiki imesheheni vitamini A,B, C, na K inayoweza kuimarisha afya ya macho na mifupa.
Kama hujawahi kula wali wa zabibu upo mahali sahihi, twende pamoja mpaka mwisho wa makala hii tunapojifunza jinsi ya kupika wali huu.
Maandalizi
Mapishi ya wali wa zabibu yanaanza kwa kuchambua mchele na kuandaa zabibu kavu ambazo ndizo hutumika katika aina hii ya mapishi.
Zabibu kavu zinazotumika katika pishi hili zinapatikana katika ‘super markets’, kwenye maduka ya nafaka na sokoni.
Kama utapendelea kuweka njegere na vitunguu swaumu huu ndio wakati sahihi wa kuviandaa pia ili kutumia muda mchache wakati wa kupika.
Baada ya kuandaa mahitaji yote washa jiko na uchemshe maji utakayoyatumia kupika wali, yakichemka yaweke pembeni na ubandike sufuria nyingine.
Sufuria ikipata moto weka mafuta ya kupikia kiasi kisha uweke kitunguu swaumu ulichokiponda pamoja na kitunguu maji kama utapendelea kisha ukoroge kwa dakika moja.
Ukiona vitunguu vyako vimeiva na kutoa manukato mimina mchele, njegere, chumvi kiasi na kijiko kimoja cha manjano yatakayofanya wali wako uwe na rangi ya kuvutia kisha koroga na ufunike uive.
Kwa wanaotumia nishati safi ya kupikia kama gesi au jiko la umeme hakuna ulazima wa kupalia makaa, funika wali wako vizuri na mfuniko usiopitisha hewa, punguza moto na uache uive taratibu.
Kama unatumia ‘rice cooker’ au ‘pressure cooker’ basi vuta kiti ukae maana ukifunika tu na kuseti kiwango cha moto wali wako utaiva wenyewe kwa haraka bila kuhitaji uangalizi wa mara kwa mara.
Wali wako ukikaribia kuiva mimina zabibu kiasi chako kisha ufunike wali uive vizuri na ladha ya zabibu iiingie kwenye chakula.
Baada ya muda tazama chakula chako kama kiveiva, geuza ili zabibu zisambae katika chakula chote kisha msosi wako utakuwa tayari kwa kuliwa.
Unaweza ukala chakula hiki na maini, nyama, samaki au mboga yoyote ya mchuzi.