Kadri siku zinavyoenda ndivyo mihogo inavyopata umaarufu katika maeneo mengi duniani ikiwemo nchini Tanzania ambapo wapishi wamebuni aina mpya ya kutengeneza kachori kwa kutumia zao hilo.
Ndiyo, mihogo inaweza kutoa kachori tamu unazoweza kuandaa nyumbani kwa urahisi huku ukijipatia faida nyingi za kiafya.
Miongoni mwa faida hizo kwa mujibu wa Taasisi ya Lishe Tanzania (TFNC) ni kuongeza virutubishi muhimu mwilini ikiwemo wanga, makapimlo, protini na mafuta kwa ajili ya kusaidia ukuaji, utengenezaji na ukarabati wa tishu za mwili.
Kama hufahamu mapishi ya kachori za mihogo usijali, sogea karibu ujifunze mapishi rahisi ya kitafunwa hiki ambacho pia unaweza kukiongeza katika orodha ya vitafunwa unavyouza mgahawani au sehemu nyingine yoyote.
Hatua kwa hatua mapishi ya kachori za mihogo
Hatua ya kwanza ni kuandaa mihogo kwa kuimenya maganda kisha kuiosha na kuikausha maji tayari kwa ajili ya kuanza mapishi.
Maji yakikauka washa jiko na uibandike jikoni kwa dakika 15 au zaidi mpaka uhakikishe imeiva na kuwa laini.
Baada ya mihogo kuiva itoe mizizi (kama ipo) na kuponda mpaka iwe laini kisha ihamishie katika bakuli kubwa na uongeze pilipili hoho iliyokatwa vipande vidogo vidogo, karoti iliyosagwa kiasi, majani ya dania na uchanganye mpaka viungo vyote vichanganyike na mihogo iliyopondwa.
Endelea na mapishi kwa kuongeza mayai, chumvi, pilipili manga pamoja na unga wa ngano ili kusaidia mchanganyiko kushikana vizuri wakati wa kukaanga katika mafuta.
Baada ya hapo tengeneza maumbo ya kachori kwa kutumia mikono ambapo utachukua kiasi kidogo cha mchanganyiko wa mihogo na kuunda umbo la duara lililoshikana vizuri. Hakikisha duara lako sio kubwa wala dogo sana ili iweze kuiva vizuri.
Hatua hiyo ikikamilika hamia katika kutengeneza uji mzito wa ngano utakaotumika kufunikia kachori zako kwa juu na kuzipa rangi ya mvuto. Utakachotakiwa kufanya ni kumimina maji kiasi, unga wa ngano, rangi kama unapendelea na chumvi kiasi kisha changanya mpaka upate mchanganyiko mzito.
Mpaka kufikia hapo unakuwa umemaliza maandalizi ya awali na hatua inayofuata itakuwa ni kukaanga kachori ambapo utaanza kwa kuwasha jiko kwa ajili ya mapishi na itapendeza zaidi ukitumia nishati safi kama gesi,umeme au majiko banifu ili upike kwa haraka huku ukiepusha kachpri zako kunuka moshi.
Baada ya kuwasha moto bandika sufuria jikoni na kabla mafuta hayajapata moto sana pitisha donge moja moja kwenye ujii mzito wa unga wa ngano uliouandaa kisha uweke jikoni. Rudia hatuahiyo kwa kachori zilizobaki na ukaange mpaka ziwe na rangi ya kahawia ambapo hapo zitakuwa tayari zimeiva.
Hakikisha wakati wote wa kukaanga kachori unatumia moto mdogo ili zisiungue na kukuharibia muonekano wa kitafunwa chako.
Ukimaliza kukaanga madonge yote hapo kachori zako za mihogo zitakuwa tayari, kuwa huru kuongeza kachumbari au aina yoyote ya kinywaji wakati wa kuzitenga mezani.