Jinsi ya kupika rosti la kibambala

Na Fatuma Hussein
9 Oct 2024
Kibambala ni samaki aina yoyote aliyekaushwa kwa njia mbalimbali kama vile kwa jua, moshi, chumvi, kukaanga, au kugandishwa kwa barafu.
article
  • Ni muhimu kuwa na tui la nazi zito na jepesi pia.

Kibambala ni samaki aina yoyote aliyekaushwa kwa njia mbalimbali kama vile kwa jua, moshi au chumvi.

Aina hizo za uhifadhi huwafanya samaki hao kudumu kwa muda mrefu na kuwarahisishia wafanyabiashara kuwasafirisha kwa umbali mrefu kuwafikia walaji.

Kwa mujibu wa Ajibu Bakari muuza samaki katika soko la Mwananyamala bei ya samaki kibambala  huanzia Sh3,500 hadi Sh7,000 wakiwa wadogo huku bei ya kibambala mkubwa huanza kuuzwa kwa Sh10,000 hadi Sh13,000.

Licha ya samaki hao kupendwa sana na walaji  Bakari amebainisha kuwa kuwa upatikanaji wake ni wa msimu kulinganisha na aina nyingine ya samaki.

“Kuna muda unaweza kukaa miezi mitatu  huoni hawa samaki hasa mvua zikiwa nyingi sana huwezi kuwaona samaki kulingana na baadhi ya samaki kutegemea njia asili za ukaushaji,” amesema Bakari.

Aidha, samaki hao waliokaushwa hutunzwa katika masanduku maalumu yanayowawezesha kuhifadhiwa kwa muda wa takribani mwezi mmoja bila kuharibika.

Leo ndani ya Jiko Point tutajifunza namna ya kuandaa rosti tamu kwa kutumia kibambala.

Maandalizi

Hatua ya kwanza osha samaki wako mkavu vizuri kwa kutumia maji ya moto ili kuondoa mchanga au uchafu wowote kisha mloweke samaki huyo kwa dakika 10  hadi 15 ili alainike kidogo.

Baada ya kumtoa kwenye maji, mchemshe kidogo maana kuna baadhi ya samaki huwa na chumvi nyingi sana hivyo fanya hivyo ili kuondoa chumvi nyingi, kisha mtoe  jikoni baada ya dakika tano.

Hatua inayofuata ni kuandaa viungo vya kupikia kwa kuosha na kuvikatakata bila kusahau kukuna nazi na kuichuja ili kupata tui jepesi na zito.

Anza mapishi yako kwa kuwasha jiko kisha bandika sufuria na uweke mafuta kiasi yasiyozidi vijiko viwili,  yakipata moto weka vitunguu kisha vikaange hadi viwe na rangi ya kahawia.

Ongeza nyanya na uache ziive kisha uweke  paprika kiasi, samaki masala, nyanya ya kopo na chumvi  kisha ufunike mchanganyiko huo uchemke kwa dakika tatu.

Baada ya mchuzi kuchemka kidogo, ongeza samaki kwenye sufuria koroga polepole ili samaki apate ladha ya viungo, kisha acha mchuzi uchemke kwa moto wa wastani kwa dakika 10, au hadi mchuzi uanze kuwa mzito kidogo.

Baada ya dakika 10 weka tui jepesi la kwanza na uache mchanganyiko huo jikoni kwa dakika zisizopungua 20.

Dakika 20 zikiisha angalia rosti kama tui la kwanza limekauka, weka tui la pili na ukae dakika tano hadi 10 ili mchanganyiko ukolee nazi baada ya hapo onja chumvi ukiridhika na ladha ulioipata baada ya hapo unaweza kuipua mchanganyiko  huo.

Ikitokea ukawa ni mpenzi zaidi wa viungo unaweza kuongeza pilipili mbichi kama unatumia,  kotimiri au dhania juu baada ya mchuzi kuiva ila usisahau kuweka hoho mwishoni maana hoho ikiiva sana inapoeza ladha yake.

Mpaka hapo rosti la kibambala litakuwa tayari kwa kuliwa hivyo unaweza kula na ugali wa mhogo, dona, sembe, ndizi za kukaanga, wali ama chapati ni wewe tu utakavyopendelea.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa