Kuku wa kupaka: Mahitaji na namna ya kuandaa

Na Lucy Samson
30 May 2022
Unahitaji vipande vya kuku, kitunguu maji, kitunguu saumu, tangawizi, pilipili manga kijiko, korosho, samli na maziwa.   Nyama ya kuku ina mapishi mbalimbali kulingana na mahitaji ya mlaji. Nyama hii ni tamu na ukiipika unavyotaka inakuwa bomba.  Umaarufu wa kuku pia unachangiwa na wataalamu wa afya kupendekeza ulaji wa nyama nyeupe yaani ya kuku, samaki na […]
article
  • Unahitaji vipande vya kuku, kitunguu maji, kitunguu saumu, tangawizi, pilipili manga kijiko, korosho, samli na maziwa.  

Nyama ya kuku ina mapishi mbalimbali kulingana na mahitaji ya mlaji. Nyama hii ni tamu na ukiipika unavyotaka inakuwa bomba. 

Umaarufu wa kuku pia unachangiwa na wataalamu wa afya kupendekeza ulaji wa nyama nyeupe yaani ya kuku, samaki na nyama ya sungura.

Tusonge mbele. Leo jikoni tunaenda kujifunza namna ya kuandaa kuku wa kupaka au kwa lugha ya kimombo “creamy garlic chicken” ambaye unaweza kula na ugali, tambi au hata chipsi na bado ukafurahia pishi hili.

Kwa kawaida kuku mzima anatakiwa kuliwa na watu wanne ila kibongo bongo hata watu nane wanaweza kugawana vipande ili mradi tu mlo wa wakati huo upite.

Andaa kuku wako kwa kumuosha na kumkata vipande vya saizi unayotaka, kisha weka kitunguu saumu, tangawizi na ndimu. Iache nyama yako kwa dakika 20 au zaidi kabla ya kuanza kupika (marination).

Baada ya hapo anza kwa kuwasha jiko lako la gesi au umeme na injika sufuria kisha weka samli kidogo au mafuta na ukaange kuku wako kwa moto wa wastani mpaka awe na rangi ya kahawia (asiive sana)

Kisha kaanga kitunguu maji, ongeza na kitunguu saumu a tangawizi iliyosagwa kiasi cha kijiko kidogo cha chakula.

Kwenye sufuria nyingine chemsha maziwa kiasi ili kutengeneza cream (malai) utakayoitumia kuongeza uzito kwenye rosti ya kuku wako.

Weka vipande vya kuku na cream ya maziwa uliyoiandaa,  kwenye sufuria uliyokaangia vitunguu huku ukiendelea kupika kwa moto mdogo, weka punje kadhaa za kitunguu saumu na korosho kiasi, kama unapendelea.

Weka chumvi ili kuleta ladha kwenye mboga kisha angalia kama rosti lako lina uzito wa kutosha kama bado unaweza kuongeza cream ya maziwa kiasi.

Koroga na acha rosti lako lichemke, kuku akishaiva vizuri basi rosti ya kuku wa kupaka itakuwa tayari kwa kuliwa. Furahia chakula chako na uwapendao.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa