Maandalizi sahihi ya ugali wa muhogo 

Na Mariam John
12 Feb 2022
Ugali huo unaweza kupikwa peke yake au ukachanganywa na unga mwingine ikiwemo unga wa mahindi ili kuleta ladha ya aina yake.
article
  • Unahitaji maji, unga, sufuria na jiko la umeme au gezi.
  • Hakikisha sufuria lako linamshikio ili usonge kwa urahisi.
  • kujua kama ugali umeiva au laa, utatumia sufuria au vidole.

Unaweza kuwa una ufahamu kama ugali wa muhogo au jina jingine udaga. Chakula hiki ni moja ya vyakula vya asili ambavyo vinapendwa na watu hasa wanaokaa mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Ugali unaopikwa na unga wa muhogo. umepewa heshima kubwa hususani na Wasukuma na ugali huo unaweza kuliwa na mboga ya aina yoyote mfano mlenda au samaki aina ya kibambala. 

Hata katika mila za Wasukuma, mwanamke anayeweza kupika ugali wa muhogo husifiwa na kuonekana “mashuhuli”.

Ugali huo unaweza kupikwa peke yake au ukachanganywa na unga mwingine ikiwemo unga wa mahindi ili kuleta ladha ya aina yake.

Wenyeji wa kabila la Wasukuma wanasema wanapendelea kula chakula hicho kwa kuwa ni chakula kinacholeta nguvu mwilini na hiyo ni kutokana na kazi wanazofanya ambazo ni kilimo, uvuvi na ufugaji.

Siri ya kuchanganya unga wa udaga na unga wa mahindi kusonga ugali ni kupunguza ulaini wa ugali na kumsaidia mpishi aupike vizuri.

Ugali wa muhogo huenda na mboga yoyote. Picha IPP Media.

Unaandaaje ugali wa unga wa udaga na mahindi?

Unachohitaji kukamilisha pishi hili ni unga wa udaga, unga wa mahindi, sufuria, maji na jiko la gesi pamoja na sufuria lenye mshikio ili uweze kusonga vizuri.

Anza kwa kuinjika sufuria la kusongea ugali jikoni na kuhakikisha maji yanachemka yanatokota.

Baada ya maji kuchemka, unaweka unga wa muhogo kwenye maji hayo na kisha unauacha kwa muda wa dakika mbili hadi tatu. 

Hatua hii ni muhimu kwa ambaye anapika ugali pasipo na kuchemsha uji. Ukiweka unga kwenye maji, maji hufyonzwa na unga taratibu na hivyo kupunguza uwezekano wa kupika ugali wenye mabuje.

Hatua inayofuata ni kusonga ugali kwa kutumia nguvu kiasi. Ongeza unga kama unaona ugali bado ni mlaini na endelea kusonga hadi uridhike na matokeo yako.

Kwa wasukuma hatua ya kujua kama ugali umeiva ama laa inaitwa “kukonda”. Hii ni kuvuta ugali kwenye kingo ya sufuria kwa kutumia mwiko.

Endapo ugali utagandana na sufuria, ujue pishi lako bado lakini endapo utaachia kingo ya sufuria, ugali wako utakuwa tayari umeiva.

Njia nyingine ya kupima kama ugali umeiva ni kuumega na kuona kama unaganda vidoleni. Ukiganda ujue kazi haijaisha lakini kama usipogandamia vidole, pishi limeiva.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa