Makange ya ndizi ni miongoni mwa msosi ya chap chap uyoweza kuandaa nyumbani hususani siku za mwisho wa wiki ambazo unahitaji muda mwingi wa kupumzika kuliko kukaa jikoni.
Mbali na urahisi wa kuandaa mlo huu utakusaidia kubadilisha menyu ya chakula nyumbani badala ya wali au ugali uliozoeleka.
Ikiwa wewe ni mpenzi wa ndizi basi makala hii ni kwa ajili yako ambapo tutaangazia hatua kwa hatua jinsi ya kupika makange ya ndizi pamoja na nyama ya kuku.
Maandalizi
Anza kwa kumenya ndizi kwa stailiupendayo kisha uzikate mara nne yaani uzigawe kiurefu na ukate mara moja kiupana kisha uzikaange zikauke vizuri, zichuje mafuta na uziweke pembeni
Baada ya hapo andaa nyama ya kuku, nyama ya ng’ombe au aina nyingine ya kitoweo kwa kuichemsha na kuikaanga tayari kwa ajili ya kuichanganya na ndizi.
Menya viungo utakavyotumia kwa urefu kama kitunguu maji, karoti na hoho (ukipata za rangi ya njano na nyekundu itakuwa vizuri zaidi) tayari kwa mapishi
Andaa nyanya na viungo vikavu unavyopendelea vitakavyonogesha msosi wako ikiwemo mchuzi masala, soya sosi na binzari nyembamba
Hatua inayofuata ni kuwasha jiko kisha weka sufuria jikoni na uanze kuweka mafuta kiasi ikifuatiwa na kitunguu ambacho utakikaanga mpaka kilegee au kuwa na rangi ya kahawia.
Weka nyanya ulizosaga kisha ufunike ziive na baada ya hapo weka pilipili hoho na karoti ikifuatiwa na ndizi ulizokaanga pamoja na nyama.
Koroga vizuri kwa ungalifu usije ukazivunja vunja au kupnda ponda ndizi kisha ongeza chumvi kiasi, viungo vikavu, nyanya ya pakti, limao, pilipi na maji kidogo utengeneze mchanganyiko mzito.
Funika kwa dakika tatu na makange ya ndizi yatakuwa tayari kwa kuliwa.
Furahia chaula chako na juisi, soda au maji baridi.