Mapishi yanayowafaa mabachela msimu wa sikukuu

Na Mwandishi Wetu
24 Dec 2021
Unaweza kupika pilau la nyama. Chakula ambacho hakihitaji mambo mengi.
article

 • Ni pamoja na pilau lenye viungo vya kutosha.
 • Chakula hiki huliwa na kachumbari au juisi.
 • Unaweza kula mwenyewe au ulaakila masela.

Hauna mwaliko? Isiwe kesi. Unaweza kupika chakula chako nyumbani na ukajivinjari mwenyewe na kama mfuko uko poa, unaweza hata kuwaita washkaji zako mshiriki pamoja.

Hayo yote yanawezekana ukiwa na zana muhimu za mapishi ya fasta kwani bachela yeyote hapendi kutumia muda mwingi jikoni. 

Pia, wengi hupenda kuingia jikoni kutumia vyombo vichache iwezekanavyo ili wasitumie muda mwingi wakati wa kuosha.

Mahitaji muhimu kwa mapishi ya haraka:

 1. Jiko la gesi
 2. Mchele
 3. Mafuta ya kupikia
 4. Viazi mviringo
 5. Maji ya moto
 6. Viungo (pilau masala, karoti, nyanya, hoho, tangawizi, vitunguu swaumu na vitunguu maji).
 7. Nyongeza (zabibu kavu, magome ya mdalasini, iriki).
 8. Mashine ya kukunia viungo (grater), masufuria na kisu.

Tuingie jikoni

Baada ya kuona mahitaji ya vifaa, tujue hivyo vyakula vya kuandaa

Pilau ni chakula kinachofaa kuliwa mchana na hata usiku. Picha| Paleo Low Carb Natte.

Pilau la kuumiza pua za majirani.

Sikukuu ni nini bila pilau? Kupika wali huu unachohitaji ni nyama uipendayo iliyochemshwa na kuiva vyema, viazi, karoti, nyanya, hoho, vitunguu, viungo vya pilau (pilau masala) na wengine huongeza zabibu kavu.

Cha kufanya ni kukaanga vitunguu hadi viwe vya rangi ya kahawia, ongeza karoti na kisha nyanya. Vikaange kwa muda kadhaa hadi utakapoona vimelainika kabisa. 

Unaweza kuongeza viungo vingine ikiwemo vitunguu swaumu, tangawizi kiasi, magome ya mdalasini, hiriki na pilipili manga (ukihitaji ladha na harufu zaidi).

Baada ya hapo weka nyama iliyoiva, zabibu kavu na mchele uliooshwa na viazi, kisha changanya vizuri. Hakikisha viazi umevikata saizi ya wastani ili viive.

Ongeza maji ya moto kwenye mchanganyiko huo lakini hakikisha maji hayazidi sana kimo cha mchele ili isipate pilau bokoboko.

Maji yakikauka, punguza moto wa jiko lako kisha funika pishi lako na mfuniko usioruhusu mvuke kutoroka. Unaweza kutumia aluminium foil pia.

Lipatie pishi lako dakika tano hivi kisha onja kama umeivisha. Kama ndiyo, zima jiko lako tuendelee.

Wengine huongeza mayai, parachichi na mengineyo kuongeza ladha kwenye kachumbari. Picha| Precious Core.

Vikorombwezo vya kulia ubwabwa

Pilau linaweza kuliwa na vitu vingi ikiwemo juisi na kachumbari. 

Kuandaa kachumbari, unahitaji mashine ya kukunia viungo (grater) ambayo utakuna karoti kwa saizi unayotaka, tango, hoho, embe bichi au lilioiva kidogo, nyanya na wengine huongeza matunda kama zabibu na tofaa (apple).

Kata vitunguu kwa saizi uipedayo na kisha vioshe kwa kutumia maji yenye mchanganyiko wa chumvi (Hii huondoa harufu na ukali wa kitunguu kwa wasioipenda), kwa wengine sio lazima.

Weka viungo hivyo vyote kwenye chombo kimoja na kisha ongeza maji ya limao au ndimu na changanya.

Kama una mashine ya kusaga matunda, nunua nanasi na karakara (passion). Ukiosha na kumenya, saga kwa maji kiasi. Ongeza sukari, tangawizi na kisha saga tena. Chuja na weka kwenye friji. 

Imesiha hiyo!

Pakua pilau yako kwenye sahani au sinia, weka kachumbari, mimina juisi kwenye glasi na kisha ita jopo la washkaji mshambulie pishi hilo.Kama upo peke yako, washa TV yako ukiangalia filamu ambayo Binti Mkude amekuletea wikiendi hii kupitia Nukta The Podcast kwenye Apple Podcasts, Google Podcasts, Spotify na kokote unapopata podcast zako.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa